Kikwete kubebeshwa tuhuma


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 10 February 2010

Printer-friendly version
Lengo asigombee urais 2010
Waziri wake ashupalia mafisadi
Rais Jakaya Kikwete

UWEZEKANO wa Rais Jakaya Kikwete kugombea bila mpinzani ndani ya chama chake, umeanza kutoweka, MwanaHALISI limeelezwa.

Mkakati mpya wa kumuhusisha na kashfa mbalimbali na hivyo kufanya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuona umuhimu wa kuwa na mgombea mwingine, tayari umeandaliwa.

Gazeti hili lina taarifa kwamba wapinzani wa Kikwete, ndani ya chama chake, wanaandaa taarifa za kusambaza katika vyombo vya habari na vipeperushi kueleza kuwa “hata Kikwete ana kashfa; hafai.”

“Kinacholengwa ni kuonyesha kuwa watuhumiwa wa ufisadi ni pamoja na Kikwete na kwamba kinachohitajika ni kuwaweka wote mbele ya wapigakura ili wachague wanayemtaka,” ameeleza mtoa taarifa.

Mtoa taarifa anasema kutakuwa na kashfa mbili kuu ambamo Kikwete atahusishwa.

Kwanza, atabebeshwa kashifa ya mkataba wa kuzalisha umeme wa kampuni ya IPTL ambao ni moja ya mikataba inayokamua uchumi wa nchi kwa kiwango kikubwa.

Taarifa zinasema itatangazwa, “kwa njia zozote zile,” kwamba Kikwete alishiriki kufanikisha mkataba wa IPTL wakati akiwa waziri wa nishati na madini.

Pili, Kikwete atabebeshwa tuhuma kwamba ameshindwa kushughulikia kile alichoita “mpasuko” wa Zanzibar na hivyo kusababisha mazingira yanayoweza kuvunja Muungano wa Tanzania.

Kwa mwaka mmoja sasa wanaoitwa wapinzani wa Kikwete ndani ya CCM wamekuwa wale waliotuhumiwa ufisadi.

Imekuwa ikiripotiwa mara kwa mara kuwa wabunge waliotuhumiwa ufisadi, hadi wengine kufikia hatua ya kujiuzulu nafasi zao serikalini, wamekuwa wakilalamika kuwa Rais Kikwete aliwatelekekeza.

Wanaofahamika kwa kutuhumiwa ufisadi hadi sasa ni aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa, Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, mawaziri watatu wa zamani Andrew Chenge, Dk. Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi.

Mbunge mmoja kutoka kambi ya Lowassa amekiri kufahamu mbinu hizo na ameliambia gazeti hili, “Huu ndiyo mkakati wa kambi ya upinzani ndani ya CCM. Kama kila mmoja ni mchafu basi tuwaachie wananchi wenyewe wachague.”

Mkakati wa sasa umekuja baada ya kufumuka kwa taarifa za siri zilizomo ndani ya ripoti ya Kamati ya rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi iliyoundwa na CCM kutafuta chanzo cha mpasuko katika Bunge na Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Taarifa zinasema ndani ya ripoti ya Kamati ya Mwinyi, kuna tuhuma nzito walizoshushiwa Lowassa na Rostam kuhusu ushiriki wao katika kuleta mpasuko ndani ya Bunge na serikali.

Imeelezwa hatua ya sasa ya kumkabili Kikwete katika uchaguzi wa Oktoba mwaka huu, inatokana na hasira za marafiki na wapambe wa watuhumiwa wanaoona shutuma dhidi ya wenzao zinalenga kuwamaliza kisiasa.

MwanaHALISI lina taarifa kwamba waziri mmoja mwandamizi katika serikali ya Rais Kikwete ndiye aliyemwaga tuhuma tisa, kwa maandishi, mbele ya Kamati ya Mwinyi.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka makao makuu ya CCM, Lumumba na ikulu, karibu tuhuma zote tisa zimeelekezwa kwa Lowassa na swahiba wake mkuu Rostam.

Kwa mfano, miongoni mwa tuhuma walizotwishwa Lowassa na Rostam kwa pamoja, ni ile inayowahusisha na kutumia vyombo vya habari, wahariri wa magazeti na waandishi wa habari mmojammoja, kuandika habari na makala zinazolenga kuvuruga serikali.

Sehemu ya taarifa ya waziri kwa Kamati inasema, kwa muda wa miaka miwili sasa, Lowassa na Rostam wamekuwa wakitumia vyombo vya habari kuvuruga serikali.

Na kwa kila tuhuma ambayo waziri huyo alitoa, alihitimisha kwa kusema ana ushahidi na anachowasilisha.

Tuhuma nyingine ambayo Lowassa na Rostam wanatuhumiwa kwa pamoja, ni ile ya “kushughulikia” wabunge wenzao katika majimbo ya uchaguzi wanayotoka, kwa kudai kuwa ndio walishiriki “kuwaangusha.”

Tuhuma nyingine ni kwamba Lowassa na Rostam wamekusanya makundi ya watu mbalimbali, wakiwamo wabunge, viongozi wandamizi katika chama na serikali, kwa lengo la kujenga makundi ya kuwatetea kutoka katika kashfa za ufisadi zinazowakabili.

Baadhi ya mawaziri na wabunge wanaotajwa kuunga mkono Lowassa na Rostam ni pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Sophia Simba; mbunge wa Nyamagana, Laurence Masha; mbunge wa Ukonga, Makongoro Mahanga; mbunge wa Songea Mjini, Emmanuel Nchimbi na mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba.

Kamati ya Mwinyi imeelezwa pia kwamba Lowassa amekuwa kiongozi wa kwanza nchini kujiuzulu, lakini papo hapo akaongoza harakati za kujenga makundi ya kujisafisha.

Taaarifa zinasema hilo la Lowassa kujenga mtandao wa kujisafisha lilitajwa na wabunge wengi na kuhoji, mbona Dk. Hassy Kitine na Iddi Simba walijiuzulu lakini hawakuwahi kuunda makundi ya kujisafisha.

Mtoa taarifa kwa Kamati ya Mwinyi alijenga hoja nyingine nzito mbele ya Kamati hiyo.

Alimtuhumu Lowassa kushindwa kuchukua hatua madhubuti kulinda serikali wakati wa sakata la Richmond; badala yake anatumia nguvu kubwa kujitakasa.

Alisema Kikwete alitimiza ahadi yake ya kumpa Lowassa nafasi ya pili ya juu katika uongozi wa nchi na kumfanya Rostam mweka hazina wa CCM; lakini akadai kuwa walizitumia vibaya nafasi hizo.

Mbunge mmoja aliyeongea na Kamati ya Mwinyi amenukuliwa akisema, “Katika mazingira haya, nani wa kulaumiwa? Lowassa ametoboa mwenyewe jahazi lake na Rostam ameondolewa kutokana na tuhuma zinazomkabili.”

Mbunge huyo ameongeza kuwa Rais Kikwete aliona ni vema Rostam akakaa pembeni “ili kusafisha chama.”

Kwa vyovyote vile, Rostam asingekubaliwa kuendelea na wadhifa wake wa mshika mkoba wa CCM, kutokana na kukabiliwa na lundo la tuhuma.

Maelezo ya waziri mbele ya Kamati yanashabihiana, kwa kiwango kikubwa, na yale yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge, Biashara na Uwekezaji, sasa Nishati na Madini, William Shelukindo.

Shelukindo aliiambia Kamati ya Mwinyi kuwa Kamati yake ilifanya juhudi za kutaka serikali ijisafishe katika sakata la Richmond, lakini ilikosa ushirikiano kutoka kwa Lowassa.

Kwa mujibu wa taarifa, bunge lilitaka serikali ieleze hatua zilizofikiwa katika kushughulikia mchakato wa zabuni ya Richmond, lakini Lowassa kwa muda wote wa miezi tisa, anadaiwa kugoma kutoa taarifa.

Taarifa za ndani ya Kamati ya Mwinyi zinasema baadhi ya wabunge walieleza kuwa Lowassa amekuwa mbinafsi kupindukia na kwamba vurugu na minyukano inayotokea bungeni imesababishwa na ubinafsi wake.

Gazeti hili limeambiwa kuwa kwenye hitimisho la ripoti yake, Kamati ya Mwinyi inamtaka Spika Samwel Sitta kuwa “makini.”

Haikufahamika haraka ni kuwa makini katika lipi na wapi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: