Kikwete kufanya maamuzi mazito


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 11 August 2010

Printer-friendly version
Rais Jakaya Kikwete

MKAKATI wa “kuwatosa” viongozi wanne waandamizi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), akiwemo waziri mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa umekamilika.

Mbali na Lowassa, wengine wanaotajwa kutaka kutoswa ni mfanyabiashara na mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, aliyekuwa mwanasheria mkuu wa serikali, Andrew Chenge na waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi.

Hoja ya kutaka Lowassa, Rostam, Chenge na Karamagi watoswe imepangwa kuwasilishwa kwenye vikao vya juu vya CCM vitakavyofanyika mjini Dodoma wiki hii.

Vyanzo vya taarifa hizi vinasema, mkakati wa kuwaondoa katika chama vigogo hao, umelenga kumsaidia Rais Jakaya Kikwete katika kampeni zake za kuwania urais katika uchaguzi ujao.

Inaelezwa kwamba baadhi ya vigogo wanaosuka mpango huo, wanajenga hoja kwamba hatua hiyo itasaidia kumdhoofisha kisiasa mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa.

Dk. Slaa ambaye amekuwa mwiba kwa CCM na serikali yake, inahofiwa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu, atatumia karata ya ufisadi iliyokigubika chama hicho na serikali yake.

“Hatua hii imelenga kumwahi ili asiweze kutudhoofisha. Tunataka ile helkopta yake iishiwe mafuta kwa yeye kukosa la kusema,” alidokeza kiongozi mmoja wa ngazi ya juu ambaye ametajwa kuwamo katika mkakati huo.

Vyombo vya habari vimenukuu taarifa za ndani ya CHADEMA, zikisema Dk. Slaa amepanga kulipua mabomu 20 wakati wa kuelekea uchaguzi.

Viongozi hao wanne walikuwa miongoni mwa watuhumiwa 11 waliotajwa na Dk. Slaa kuwa “watafuna nchi.”

“Mkakati hapa ni kuona Kikwete anashinda kwa kishindo uchaguzi huu. Ili kufanikisha hilo, tunakusudia kuwaondoa Lowassa, Rostam, Karamagi na Chenge,” kilisema chanzo cha habari cha gazeti hili.

MwanaHALISI limefahamishwa kuwapo kwa viongozi wandamizi waliojiandaa kuwasilisha hoja hiyo ndani ya vikao vya chama.

Aidha, Kamati Kuu (CC), inatarajiwa kujadili kwa kina mchakato mzima wa kutafuta wagombea ubunge kupitia chama hicho ulivyokwenda.

Kwa mfano, wabunge wa Mkoa wa Tabora walioshindwa katika kura za maoni wameelekeza lawama zao kwa Rostam, wakidai kuwa “ndiye anayemiliki siasa za mkoa huo.”

Katika kura za maoni zilizopigwa Agosti mosi, ni wabunge wawili tu, Samwel Sitta (Urambo Mashariki) na Rostam mwenyewe walioshinda katika kinyang’anyiro hicho.

Wabunge wengine sita, Said Nkumba (Sikonge), Siraju Kaboyonga (Tabora Mjini), Teddy Kasela-Bantu(Bukene), Dk. James Nsekela (Tabora Kaskazini) na Lucas Selelii (Nzega) hawakufanikiwa kipenya.

Katika jimbo la Urambo Mashariki, kwa mfano, Samwel Sitta, aliponea chupuchupu kwa nguvu za Kikwete na umahiri wake katika siasa.

Mara kadhaa Sitta amekuwa akituhumu wapinzani wake, kwamba wamemwaga zaidi ya Sh. 120 milioni kwa lengo la kumwangusha.

“Ni umakini wa Sitta mwenyewe pamoja na wananchi wa Urambo uliomsaidia kubaki. Uzuri ni kwamba hata mwenyewe analijua hilo kwani amekuwa akisema wazi ingawa hataji wale anaowaita ‘wapinzani wangu wenye nguvu kubwa kitaifa,’” alisema mwana Urambo aliyezungumza na gazeti hili.

Mchakato wa kura za maoni umeibua malalamiko kila kona. Katika jimbo la Monduli mkoani Arusha, Dk. Salash Toure amelalamika kufanyiwa faulo na wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Lowassa.

Dk. Toure anadai kuwa Lowassa alianza kampeni kabla ya wakati kwa kugawa simu na vitu vingine kwa viongozi wa vitongoji na vijiji.

Aidha, anadai kuwa ushindi wa kura 37,000 alizopata Lowassa dhidi ya 300 zake, umegubikwa na utata.

Anadai, “Ukiangalia idadi ya wapiga kura wa Monduli, hizo ni kura nyingi sana. Ni sawa na kusema watu wote wenye umri wa kupiga kura ni wana CCM.

“Na idadi inakaribiana sana na ile ya waliopiga kura mwaka 2005 kwenye uchaguzi mkuu. Swali la kujiuliza ni lini hawa Wamasai wote kutoka Monduli waliohamia Arusha Mjini na Dar es Salaam kutafuta maisha walirudi kupiga kura?” Kilihoji chanzo cha habari.

Mkoani Dar es Salaam, CC inatarajiwa kuingia katika mjadala mzito kuhusu matokeo ya uchaguzi katika majimbo yote ya uchaguzi.

Hata hivyo, gazeti hili limeambiwa kuwa “macho makali” zaidi yatawekwa na wajumbe wa CC kwenye majimbo ya Kinondoni, Kawe na Ubungo ambako kulikuwa na malalamiko mengi ya wanachama.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Shamsa Mwangunga inadaiwa kuwa alihujumiwa na baadhi ya viongozi wa juu wa chama wilayani humo.

Anayetuhumiwa kumhujumu Mwangunga ni kiongozi mmoja wa ngazi ya juu wilayani humo.

Kwa mfano, katika baadhi ya vituo matokeo halisi yalibadiliswa. Inadaiwa kuwa katika Kata ya Sinza, Mwangunga alipata kura 6695, lakini matokeo halisi yalionyesha alipata kura 702.

Naye, Nape Nnauye anatuhumu kuchezewa kile kinachoitwa, “mchezo mchafu” na baadhi ya viongozi wake. Aliyeshinda katika jimbo la Ubungo, ni Hawa Ng’umbi.

MwanaHALISI limeelezwa kuwa kutokana na malalamiko ya kura za maoni kuwa mengi, hata katibu mkuu wa chama hicho, Yusuf Makamba atakuwa katika wakati mgumu kujibu tuhuma mbalimbali za kuvurugwa mchakato huo.

Makamba anatuhumiwa na wenzake katika chama kubeba baadhi ya wagombea; kubadilisha utaratibu wa kura za maoni kwa kuruhusu wanachama wote kupiga kura, badala ya wenye kadi za CCM na shahada za kupigia kura.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: