Kikwete kuitwa mahakamani


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 04 May 2011

Printer-friendly version
Rais Jakaya Kikwete

RAIS Jakaya Kikwete ametajwa kuwa mmoja wa mashahidi “muhimu sana” wa Profesa Costa Ricky Mahalu anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.

Sasa Rais Kikwete aweza kutinga mahakamani wakati wowote pale mawakili wa Prof. Mahalu watakapoanza utetezi katika kesi anamodaiwa a “kufanya udanganyifu katika ununuzi wa nyumba ya ofisi ya ubalozi” mjini Roma, nchini Italia.

Bali Rais Kikwete ana nafasi ya kutoingia mahakamani moja kwa moja. Anaweza kuwasilisha hati ya kiapo (affidavit) itakayoeleza anachofahamu kuhusu Prof. Mahalu na utendaji wake, kuhusiana na ununuzi wa nyumba ya kibalozi mjini Roma.

Sasa Prof. Mahalu amepata shahidi mwingine muhimu, baada ya wiki iliyopita, rais mstaafu Benjamin William Mkapa kutoa hati ya kiapo akitetea kila kitu alichofanya Mahalu na kumweleza kuwa mtu mwenye tabia thabiti ya “ukweli, uaminifu na uchapaji kazi.”

Taarifa zilizopatikana jijini Dar es Salaam juzi Jumatatu zilisema mawakili wa Prof. Mahalu tayari wamepeleka ombi rasmi kwa Rais Kikwete kutaka afike mahakamani kutoa utetezi au kuwasilisha hati ya kiapo juu ya anachofahamu, kama alivyofanya Mkapa.

Gazeti hili limeona barua iliyoandikwa na mawakili. Inakwenda kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Ikulu. Barua hiyo iliyosainiwa na wakili Mabere N. Marando inasema, pamoja na mambo mengine, “Tumeandika barua hii ili tupate kibali kabla ya kuomba samansi ya mahakama.”

Prof. Mahalu anashitakiwa kwa pamoja na Grace Martin, mmoja wa maofisa ubalozi aliyekuwa Roma. Kesi hii iko mbele ya mahakama ya Kisutu. Imepangiwa hakimu mkuu mkazi Ilvin Mgetta baada ya hakimu wa awali kukataliwa na upande wa utetezi wakidai kutokuwa na imani naye.

Barua ya Marando kwenda kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Ikulu inasema, “Bila shaka unayo habari juu ya kesi ya jinai inayoendelea mahakama ya Kisutu dhidi ya Balozi Profesa, Dk. Costa Mahalu. Sasa imefika wakati wa utetezi.”

Marando anasema katika barua hiyo, “Miongoni mwa mashahidi ambao mteja wetu ametuagiza tuwaite kumtetea, ni Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano. Hii ni kwa sababu nyumba ya ubalozi wetu Italia ilinunuliwa wakati Mh. Rais akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na alikuwa na taarifa zote juu ya mchakato mzima ulivyoendelea.”

Anasema mchakato huo ni kuanzia kupewa mamlaka maalum ya kisheria (Special Power of Attorney) ambayo Kikwete alitia saini tarehe 24/9/2002; na hotuba yake aliyotoa Bungeni tarehe 3/8/2004 akithibitisha kuwa ununuzi wa jengo hilo haukuwa na mushkeli wowote.

“Mteja wetu ametupa pia barua nyingi alizomwandikia Mh. Waziri wa Mambo ya Nje na Katibu Mkuu wa Wizara wakati huo,” na kwamba wanatarajia “Mh.Rais kuzitambua mahakamani.”     
 
Mawakili wa Prof. Mahalu wanasema wamefikia uamuzi huo mzito “…kwa kuwa mteja wetu hana njia nyingine; kwa sababu asipodhihirisha ukweli mbele ya mahakama, anaweza kupatikana na hatia na akapelekwa jela.” 

Sehemu muhimu ya barua hiyo inasema, “Kwa hiyo tunaomba, kwa unyenyekevu kabisa, uweke barua yetu hii mbele ya Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; aisome na akueleze utujibu kama hana pingamizi kuja kueleza ukweli mahakamani.

“Kama muda wake hauruhusu, kulingana na ratiba zake za kitaifa, tunaomba aturuhusu tumwandalie kiapo (affidavit) kitakachoeleza yaliyotokea, ili tukiwasilishe mahakamani badala ya kumwita yeye mahakamani,” inasomeka sehemu ya barua.

Nakala ya barua iliyotumwa ikulu imepelekwa pia kwa mwendesha mashitaka wa serikali (Public Prosecutor In-charge) mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam.

Akirejea kinga ya rais ya kwenda mahakamani kutoa ushahidi, Marando katika barua yake anasema, “Tumeangalia katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuona kwamba hakuna kifungu kinachozuia Mh. Rais kuitwa kutoa ushahidi katika kesi kama hii.”

Anaongeza kuwa wanamhitaji rais “…kwa kuwa mteja wetu hana njia nyingine; kwa sababu asipodhihirisha ukweli mbele ya mahakama, anaweza kupatikana na hatia na akapelekwa jela.” 

Msingi mkuu wa Prof. Mahalu kumwita Rais Kikwete kuwa shahidi wake ni kwamba ni rais, wakati huo akiwa waziri wa mambo ya nje, aliyesaini hati maalum ya kumpa madaraka ya kutenda.

Aidha, ni Kikwete aliyeliambia bunge mwaka 2004 kuwa kila kitu kimefanywa kwa uwazi na utaratibu kama ilivyotakiwa na serikali.

Mashahidi hawa wawili – Mkapa na Kikwete – na Mahalu mwenyewe, wanajenga ngome kuu ya utetezi ambayo mawakili wanatarajia kutumia kubomoa upande wa mashitaka.

MwanaHALISI katika toleo lake lililopita, lilinukuu hati ya kiapo ya Mkapa ikithibitisha kuwa vyombo vya dola vilimjulisha kuwa balozi Mahalu alipewa mamlaka kamili ya kisheria kusimamia na kutekeleza mchakato mzima wa ununuzi.

Katika hati ya 31 Machi 2011, chini ya Sheria ya Usajili wa Nyaraka (The Registration of Documents Act, Cap. 117 R.E. 2002), Mkapa anaweka utetezi kuwa kila kilichofanywa na Mahalu kilikuwa halali.

Aidha, Mkapa anasema kuwa ni yeye aliyezindua jengo la ubalozi tarehe 23 Februari 2003.

Katika kiapo cha Mkapa, kiongozi huyo wa awamu ya tatu anakiri kufahamu mikataba miwili akisema, “…utaratibu wa makubaliano ya aina mbili uliishawahi kufanywa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pale ilipoonekana muhimu kwa kuzingatia maslahi ya taifa.

Kauli ya Kikwete katika kiapo haitazamiwi kuwa tofauti na ile ya bosi wake wakati ule, Mkapa. Kikwete alikuwa waziri wa mambo ya nje chini ya utawala wa Mkapa.

Kwa mujibu wa nguvu ya kisheria ya 24 Septemba 2002, aliyosaini Kikwete kumwezesha Prof. Mahalu kutenda kazi alizoagizwa anasema, “…kwa niaba na kwa maslahi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nampa Profesa Costa Mahalu mamlaka ya kununua kutoka kwa CERES- Societa Responsabilita Limitata (Limited Company) yenye ofisi inayotambulika kisheria jijini Rome, jengo lililoko Rome, 185, Via Cortina d’ Ampezzo.”

Anasema ununuzi huo unahusu nyumba nzima yenye bustani, na ukubwa wa mita za mraba 1865, iliyopo kwenye mtaa wa Via Cortina D’ Ampezzo, ambako ndiko eneo la kuingilia lilipo, pamoja na Condomium of 110, Via della Mendola, Condominium of 7, Via Misurina, Condominium of 183, Via Cortina d’ Amepezzo na mengine, kama yapo.

Mbali na nguvu hiyo ya kisheria aliyopewa Prof. Mahalu na Kikwete, wakili Marando anasema, “Mteja wetu ametupa pia barua nyingi alizomuandikia Mh. waziri wa mambo ya nje na katibu mkuu wa wizara husika.”

Kumbukumbu za Bunge (hansard) ambazo Marando ananukuu katika barua yake ya ikulu, ni zile zilizomnukuu Kikwete akisema, ununuzi wa jengo la ubalozi mjini Roma ulifanyika kwa misingi ya uwazi na ulifuata taratibu zote zilizotakiwa.

Alisema, “Mheshimiwa naibu spika, mwaka 2001/2002 wizara ilinunua jengo la ubalozi counsel katika ubalozi wa Roma katika jitihada za kuondokana na tatizo la kupanga majumba ya watu huko nje na pia kupunguza gharama za kuendelea kulipa pango la nyumba kila mwaka.”

“Ununuzi wa jengo hili ulifuata taratibu zote za manunuzi ya majengo ya serikali kwa kuzishirikisha wizara za ujenzi, ardhi na maendeleo ya makazi, pamoja na wizara ya fedha,” alisema.

Akionyesha unyenyekevu, Marando anaandika ikulu, “Tunarudia kusema kuwa tunaomba hili tukijua nafasi ndogo aliyonayo Mh. Rais, lakini izingatiwe kuwa hapa tuna tatizo linalohusu uhuru wa mwanachi na haki zake mbele ya sheria.”

Kesi dhidi ya Prof. Mahalu imepangwa kuanza kusikilizwa 30 Mei mwaka huu ambapo Mahalu na mshitakiwa mwenzake, Grace Martin wanatarajiwa kuanza kujitetea.

0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: