Kikwete kupangua MaDC


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 18 February 2009

Printer-friendly version

RAIS Jakaya Kikwete anatarajiwa kufanya mabadiliko makubwa katika uteuzi wa wakuu wa wilaya wakati wowote kutoka sasa, imefahamika.

Taarifa kutoka ndani ya Serikali, zinasema rais atafanya uteuzi mpya na kuhamisha wengine kutoka vituo vyao vya kazi vya sasa.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari hizi, uteuzi ulikuwa ufanywe mwishoni mwa wiki iliyopita. Inawezekana ugeni wa Rais wa China ni miongoni mwa sababu za kuahirisha kutangazwa kwa mabadiliko hayo hadi wakati wowote kuanzia sasa.

Haikufahamika mara moja sababu za uteuzi huo ufanywe sasa, lakini wachunguzi wa mwenendo serikalini wanasema ni moja ya njia ya kujipanga upya kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa – vijiji, vitongoji, mitaa na uchaguzi mkuu wa 2010.

Hata hivyo, uteuzi utaziba pengo la wakuu wa wilaya katika wilaya za Bukoba na Kahama. Mkuu wa wilaya ya Bukoba, Albert Mnali alifukuzwa kazi na Rais Ijumaa iliyopita kutokana kitendo cha kuwapiga viboko walimu wa shule za msingi.

Wakuu wa wilaya ambao ni makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni mhimili mkuu wa chama hicho kisiasa kwa ngazi za wilaya, tarafa, kata na vijiji.

Uteuzi wowote wa sasa utakuwa unazingatia uwezo na ari ya wateule katika kutenda kazi za chama; hasa katika kuhamasisha wananchi kukipigia kura chama hicho katika chaguzi zijazo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya CCM, wakuu wengi wa sasa wa wilaya wanaweza kupoteza nafasi zao kutokana na tathmini ya kazi zao kwa kipindi cha miaka mitatu ya utawala wa rais Kikwete.

Miongoni mwa sababu zitakazowaangusha wengi ni utawala wa kibabe, kutosikiliza matatizo ya wananchi, kutowatembelea na kuwa karibu nao, kutokuwa na ubunifu katika kushughulikia changamoto za vijijini na kutokuwa na ushirikiano na viongozi wa CCM kwa ngazi hiyo.

“Wale wote wenye tabia ya Albert Mnali wasifikirie kurejeshwa katika mabadiliko haya,” kimesema chanzo cha habari hizi.

Mnali alipiga viboko walimu wa shule za msingi za Katerero, Kansenene na Kanazi wilayani Bukoba kwa madai kuwa wamemwaibisha kwa wilaya yake kuwa ya mwisho katika matokeo ya mtihani wa Darasa la Saba mkoani Kagera.

Taarifa zinasema baadhi ya wakuu ambao wanaweza kutoswa ni pamoja na Thomas ole Sabaya aliyeko Songea, Pachal Mabiti wa Manyoni na Kapteni James Yamungu.

Wakuu hawa wamekuwa wakilalamikiwa na wananchi katika maeneo walikofanya kazi hasa katika wilaya zenye migodi ya madini.

Katika uteuzi huo, habari zinasema, karibu asilimia 30 ya wakuu wa wilaya huenda wasirejeshwe kutokana na umri mkubwa, kushindwa kazi, kulalamikiwa na wananchi kwa kutojali na vitisho.

Sura mpya zinazotarajiwa kwenye orodha ya wakuu wapya wa wilaya ni pamoja na zile za viongozi wa Umoja wa Vijana (UV-CCM), wanachama wengine wa umoja huo na baadhi ya vijana katika CCM.

Kutokana na ahadi ya Rais Kikwete ya kuongeza idadi ya wanawake katika ngazi za uongozi, inatarajiwa wanawake wengi zaidi watateuliwa kwenye wadhifa huu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: