Kikwete, kura na watuhumiwa ufisadi


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 22 September 2010

Printer-friendly version
Uchambuzi
Mtuhumiwa Edward Lowassa

JAKAYA Mrisho Kikwete, yule mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ameonyesha yuko tayari kumfukua rafiki yake wa siku nyingi, Edward Lowassa kutoka kwenye kifusi.

Vyombo vya habari vimemnukuu Kikwete akisema kuwa hajawahi “kuona mchapakazi kama Lowassa” na kwamba ndiyo maana anamwombea kura.

Angalau magazeti matatu ya kila siku yameandika kuwa Kikwete alisema, “Yaliyopita si ndwere, tugange yajayo;” kwa maana kwamba yaliyomsibu rafikiye Lowassa sasa yawekwe kando.

Katika mazingira ya uandishi wa kushawishi na kushawishiwa, yawezekana Kikwete hakusema yaliyochapishwa; lakini usalama wa mchambuzi ni kwamba si Kikwete wala maofisa wake, wamekanusha taarifa hizo kwa wiki nzima sasa.

Kikwete alikuwa akihutubia mikutano ya kampeni za urais, ubunge na udiwani huko Monduli na Mto wa Mbu, mkoani Arusha.

Kikwete alishika mkono wa Lowassa, akauinua juu kwa staili ya “makomredi,” akionyesha kuwa yaliyokuwa yamemsibu Lowassa “yameisha” na kwamba sasa wamchague kuwa mbunge wao.

Yote haya yana ujumbe maalum; kwamba Kikwete alikuwa anamuibua rafiki yake Lowassa kutoka kwenye kifusi cha lawama, shutuma na tuhuma zilizomwelemea, hasa kuhusiana na kashfa ya mkataba wa kufua umeme kati ya serikali na kampuni ya Richmond.

Kauli za Kikwete juu ya Lowassa na hasa kibwagizo kuwa ni “mchapakazi hodari,” vimethibitisha uvumi uliokuwepo kwamba kabla ya mchakato wa kuwania urais ndani ya CCM, ililazimu Kikwete akutane na Lowassa ili “kusafisha njia yake.”

Uvumi uliokuwepo ni kwamba Kikwete alimwita Lowassa na kumuuliza iwapo atagombea urais. Jibu lililopatikana ni kwamba Lowassa alisema hajafanya uamuzi.

Ni wakati huo baadhi ya viongozi ndani ya CCM walikuwa wakisutana na wengine kusikika wakijiapiza kusimamisha mgombea wao wa urais – Lowassa akitajwa mara nyingi.

Mmoja wa watu wa karibu na Lowassa alinukuliwa akisema kuwa kauli yake kwamba hajaamua iwapo atagombea, ilimlazimu Kikwete atafute suluhu na mwenzake kwa maana ya “nikune hapa, nitakukuna pale.”

Taarifa zinasema ilikubaliwa kuwa hata kama Lowassa hataki au hawezi kugombea, basi akae kimya na asijaribu “kumharibia mwenzake.” Mkataba. Hakika Lowassa hajavunja mkataba huo.

Yaliyotokea Monduli ndiyo yalitokea Rombo, mkoani Kilimanjaro. Kikwete alimwinua Basil Mramba na kumwombea kura kwa maelezo kuwa ni panga la zamani ambalo lingali na makali.

Bila shaka Kikwete amefanya au atafanya hivyo kwa wengine zaidi ya Lowassa na Mramba.

Kikwete alikarabati magereza ya Dar es Salaam na kuyapa hadhi ya makazi hata kama ni kwa kutengwa na ndugu zako. Akawakamata aliochekecha na kuona ni watuhumiwa wa ufisadi. Akawaweka ndani na kuwafungulia mafaili mahakamani.

Bila shaka kuna tofauti kati ya kufungulia mtu faili mahakamani na kufungulia mtu mashitaka. Hilo litajieleza kadri tunavyofuatilia kinachoendelea mahakamani.

Wakati Lowassa alijiuzulu uwaziri mkuu, tena katikati ya tuhuma ambazo bado zingali mbichi kabisa, Mramba anakabiliwa na mashitaka ya kutumia ofisi yake vibaya na kusababisha hasara kwa serikali.

Kwa mujibu wa alichofanya Kikwete, tuhuma ambazo hazijaisha – nje au ndani ya mahakama – hazina uzito. Anawapigia kampeni wahusika waingie bungeni “kama walivyo.”

Bila shaka atafanya hivyo kwa watuhumiwa wengine; kwa mfano Andrew Chenge ambaye, pamoja na tuhuma, anaendelea kuwa katika kamati ya nidhamu ya CCM.

Tukirudi kwa Lowassa, wachunguzi wamekuwa wakieleza, waziwazi na kimyakimya, kuwa mwanasiasa huyo ana ndoto za kuwania urais, kama ambavyo matendo kadhaa yameelekeza huko.

Hata Kikwete anajua vema, kwamba Lowassa ana wakuu wake wa wilaya na mikoa; kwamba ana maofisa utawala na wakurugenzi wa serikali za mitaa. Kwamba ana wafuasi miongoni mwa wabunge. Analenga mbali.

Hii ndiyo inafanya wachunguzi watwambie kuwa Lowassa ana chama na serikali, ndani ya chama na serikali anayoongoza Kikwete.

Kwa hiyo, kunyamza kwa Lowassa – ili Kikwete amalizie ngwe yake – ndiko kunatajwa kuwa sehemu ya mkakati wa Kikwete wa kulegeza wabunge waliokuwa wameshupalia Lowassa kuhusiana na kashfa ya Richmond.

Kilichoitwa muwafaka wa kamati ya Nishati na Madini, kwa upande mmoja, na serikali kwa upande mwingine, ndicho kilizimua ukali wa wabunge waliojitambulisha kuwa “wapambanaji dhidi ya ufisadi,” na hasa juu ya Richmond na Lowassa.

Kupondeka kwa wabunge, kwa shabaha ya kununua upendeleo ndani ya CCM ili wasitemwe katika mchakato wa kutafuta wagombea, ndiko kulitoa ushindi wa kwanza wa Lowassa dhidi ya “maadui” wake.

Hatua hii ndiyo inaitwa “usaliti” wa wabunge wa CCM kwa wananchi na hasa wanaharakati, waliosimama imara na kamati ya bunge kuweka watuhumiwa wote matumbo moto.

Hoja ya ufisadi wa Richmond iliwaunganisha wananchi na kundi la wabunge, hata kama baadaye iligundulika kuwa kundi hilo lilitaka kutafuta upenyo tu wa kisiasa na ndiyo maana likajisalilisha.

Kikwete aliyenyamaza – akiuma na kupuliza – hadi kulaumiwa kuwa anashindwa kuchukua maamuzi makuu na muhimu, leo ndiye anatabasamu na hata kupasua kicheko, huku akiwainua mikono juu na kuwanadi watuhumiwa kwa ajili ya ubunge.

Ule mwafaka kati ya serikali na kamati ya bunge; hadi kamati kujisalimisha kwa serikali kwa madai kuwa serikali tayari imetekeleza au itatekeleza maazimio 21 ya bunge, unatafsiriwa kuwa mkakati wa kuzima tuhuma na kuandaa njia ya Lowassa kurejea kileleni.

Bali, kilichomtoa Lowassa kileleni bado kipo palepale. Kashfa ya Richmond bado mbichi. Kauli ya Kikwete kuwa watu wasahau, wasamehe na waanze kuganga yaliyopo na yajayo, haimwondoi Lowassa katika janga.

Kikwete anapata wapi mamlaka ya kusema yameishakatika suala la Richmond? Mmoja wa wasomaji wa gazeti la MwanaHALISI anaandika katika sms, “…ya Lowassa yamepita kwa Kikwete, siyo kwa Watanzania…tugange yepi zaidi ya umasikini? Kama ni msamaha, basi angetuomba Lowassa mwenyewe.”

Anaandika, “Haiwezekani tupitie maisha haya ya dhiki na umasikini uliotamalaki kwa yeye kushindwa kuwajibika na leo utwambie yaliyopita si ndwele…yanapitaji madhambi yake. Yamepita kwako JK, siyo kwetu.”

Kikwete aliwaambia watuhumiwa wa ufisadi kurejesha kiasi “fulani” cha fedha walizoiba ndipo atawasamehe. Ni yeye aliyeliambia taifa kuwa baadhi wamerejesha. Anajua nani walirejesha na kiasi gani. Anajua alipoziweka.

Hata kama Lowassa ni swahiba wake Kikwete kwa miaka mingi, Lowassa amerejesha nini? Watuhumiwa wengine, “waliofunguliwa mafaili” mahakamani, wamerejesha nini hadi apite akiwanadi kuendelea na yote mawili: Tuhuma za ufisadi na uongozi wa umma?

Kifusi cha lawama, shutuma na tuhuma – zinazomwelemea Lowassa, hasa kuhusiana na kashfa ya mkataba wa kufua umeme kati ya serikali na kampuni ya Richmond – hakisikii sululu wala koleo. Kikwete analia “mafisadi! mafisadi!” wakati huohuo anapita akiwaombea kura. Si wangemaliza moja kwanza?

Wasomaji na wachambuzi wanakubaliana: Kikwete akinyimwa kura, “watuhumiwa wake” watayeyuka. Inawezekana; na ndoto za urais za watuhumiwa mwaka 2015, zaweza kuyeyuka pia.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: