Kikwete kushindwa ahadi zake


Nicoline John's picture

Na Nicoline John - Imechapwa 11 August 2009

Printer-friendly version
Uchambuzi
Rais Jakaya Kikwete

MWAKA kesho ni mwaka wa uchaguzi. Tayari Rais Jakaya Kikwete amenukuliwa akijitapa kwamba yeye na chama chake watatimiza kile walichoahidi kabla na baada ya kuingia madarakani. Anasema atafanya hivyo, kabla ya uchaguzi mkuu mwingine kufanyika.

Kauli ya Kikwete kwamba atatekeleza ahadi zake aliitoa mwishoni mwa wiki iliyopita, mkoani Singida kwenye uzinduzi wa barabara ya Singida – Minjingu.

Lakini inafahamika kwa wengi, kwamba kabla na baada ya Kikwete kuingia madarakani, alitoa lundo la ahadi. Hadi sasa hajatekeleza ahadi nyingi na wala hakuna dalili kuwa anaweza kuzitekeleza.

Hii ni kwa sababu Kikwete bado anaendelea kutoa ahadi mpya, wakati hajazimaliza zile za awali.

Kwa mfano, Rais Kikwete hajatekeleza ahadi ya kushughulikia mafao ya waliokuwa watumishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyovunjika mwaka 1977.

Madai ya waastafu hawa yalikuwapo kabla Kikwete hajaingia madarakani. Lakini ni yeye aliyeahidi kwamba atayashughulikia hadi tamati.

Lakini mpaka sasa, ikiwa imebakia miezi 16 kabla ya kumaliza kipindi chake cha urais, wastaafu wanaendelea kulalamikia serikali yao kuwa imeshindwa kutimiza ahadi yake.

Madai ya wastaafu yamegawanyika katika maeneo mawili. Kuna wale wanaodai kupunjwa mafao yao kwa kulipwa kiduchu na wale wanaosema hawajalipwa kabisa.

Kikwete ameshindwa kutatua matatizo ya wote. Badala yake Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkullo anasema, "Hakuna hata mstaafu mmoja anayeidai serikali."

Lakini hivi karibuni, katika mkutano wa bunge uliomalizika mwanzoni mwa mwezi huu, naibu waziri wa fedha na uchumi, alinukuliwa akisema serikali inakaribisha malalamiko ya mtu mmojammjoja badala ya kundi.

Alitaka wale ambao wanaona bado wanadai serikali, wapeleke madai yao na vielelezo ili waweza kushughulikiwa.

Hapa ndipo kunazuka utata. Rais anaahidi kumaliza mgogoro. Waziri wake anasema serikali haidaiwi. Naibu waziri anasema wadai waende mmojammoja na vielelezo. Nani anasema lipi na nani wa kuamini?

Kutokana na hali hiyo, wananchi hawa wanasema, bila kutafuna maneno, kwamba "Kikwete ameshindwa kutimiza kile alichoahidi." Wengine wanasema Kikwete amewahadaa.

Ukiacha hilo la wastaafu, Kikwete ameshindwa kushughulikia madai ya muda mrefu ya walimu wa shule za msingi, sekondari na vyuo.

Badala yake, serikali imeendelea kukwaruzana na walimu hawa. Walimu kupitia chama chao - CWT, wamekuwa wakituhumu serikali kwamba inawapunja stahiki zao, yakiwamo malipo ya uhamisho, usafiri na mafunzo wakiwa kazini.

Walimu waliitisha mgomo mkubwa wenye shabaha ya kufafanua malalamiko na madai yao na kushinikiza serikali kuchukua hatua. Mgomo uliathiri kwa kiwango kikubwa taaluma ya elimu nchini.

Hata pale serikali ilipotaka majadiliano na walimu, majadiliano yalipofanyika, hayakuzaa matunda yaliyotarajiwa.

Kelele za serikali, kwamba mgomo huo ulikuwa batili, hazikusaidia walimu kufuta mpango wao wa kugoma. Badala yake walisisitiza kutoenda kazini mpaka walipwe wanachotashili.

Hatua ya walimu kung'ang'ania mgomo ilisukuma serikali kukimbilia mahakamani kuzuia mgomo huo. Hiyo ikawa aibu nyingine kwa serikali ya Kikwete.

Nia aibu kwa vile ilikuwa mara ya kwanza, tangu taifa hili lipate uhuru, serikali kukimbilia mahakamani kushitaki wafanyakazi wake kwa lengo la kuzuia mgomo. Mgomo mara zote humalizwa kwa njia ya majadiliano.

Ukiacha hilo, Kikwete ameshindwa kutekeleza ahadi yake ya "Maisha Bora kwa kila Mtanzania." Rushwa, ufisadi vinaendelea kujikita ndani ya chama chake na serikali kwa ujumla.

Bidhaa za viwandani na hata nafaka zimeendelea kupanda bei. Kwa mfano, kabla ya Kikwete kuingia madarakani, kilo moja ya sukari ilikuwa inauzwa Sh. 600. Hivi sasa kilo ya sukari inauzwa kwa Sh. 1500.

Mfuko wa Saruji mwaka 2005 ulikuwa unauzwa Sh. 9,000, lakini sasa bei imepanda hadi Sh. 14,500.

Wala hakuna dalili za hali hii kubadilika kabla ya Kikwete kumaliza kipindi chake cha uongozi. Hii ni kwa sababu serikali imeshindwa kulinda viwanda vya ndani.

Ukiacha hili, Kikwete ameshindwa kutimiza ahadi yake ya kuangalia upya mikataba ya madini, badala yake serikali inaendelea kuambulia kile kinachoitwa, "Mrabaha" huku makampuni ya uchimbaji madini yakiendelea kuchota rasilimali za nchi.

Serikali ya Kikwete imeshindwa pia kulinda raia na uharibifu wa mazingira unaotokana na kuwapo kwa migodi hii. Mfano hai ni tatizo la mgodi wa North Mara ambapo imetaarifiwa kuwa wakazi wa maeneo hayo wameathirika kutokana na kutumia maji yenye chembechembe za sumu kutoka migodini.

Bado serikali haijaonekana kusimamia sheria za mazingira zinazotaka wawekezaji hawa kulipa wahusika fidia. Kutochukua hatua dhidi yao ni kuwakingia kifua tena kwa maelezo hafifu.

Serikali imekuwa ikiwaona wawekezaji hawa kama muiungu watu. Kila kona ya nchi ambako kuna mgodi wananchi wanalalamika.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: