Kikwete, Lowassa ‘wanatesa’ taifa


Kondo Tutindaga's picture

Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 14 March 2012

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

MCHAKATO wa kumpata mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Arumeru Mashariki umeacha makovu ya hatari katika mtandao wa chama hicho.

Baada ya jitihada nyingi zilizoambatana na vitimbi vya rushwa, kijana Sioyi Sumari aliteuliwa na Kamati Kuu ya CCM kugombea akiwakilisha chama hicho.

Mambo mengi yamesemwa kuhusu mgombea huyu na sasa ni wazi kuwa mchakato wa kumpata umekigawa zaidi chama badala ya kukiunganisha.

Kwa kuwa chama hiki kinaongozwa na Rais (dola), ni rahisi kuona waziwazi majonzi yaliyojaa vifuani mwa watu kuhusu uamuzi wa kumsimamisha mgombea huyo.

Mwenyekiti wa chama anapokuwa ndiye rais na mkuu wa nchi, mapenzi yake hutimizwa hata kama watendaji na wanachama wanaona tofauti.

Kwa sasa yanayosemwa na watendaji wa chama nyuma ya mgongo wa mwenyekiti, yanatosha kuonyesha chama kinameguka chama.

Katikati ya mnyukano wa kumpata mgombea Sioyi, wapo watu wawili ambao kwa kadri siku zinavyokwenda, wanakitesa chama, serikali na hata taifa zima. Hawa ni mabwana Edward Lowassa na Jakaya Kikwete.

Wakati Edward Lowassa anajua anataka nini na anasimamia nini katika kila tukio linalojitokeza, Jakaya hajui anataka nini na misimamo yake mara nyingi inajengwa dakika za mwisho kwa kutegemea upepo umekaaje siku hiyo ya kufanya uamuzi.

Kwa hiyo uwazi wa Lowassa na ukimya wa Kikwete ni mateso kwa CCM, serikali na taifa.

Katika mchakato huu wa kumpata mgombea wa CCM, Edward Lowassa alijulikana anataka nani.

Hata alipoulizwa na sekretariati ya chama juu ya ugombeaji wa Sioyi, aliwaambia kuwa Sioyi alienda kwake kumpa taarifa kuwa anagombea, na yeye akamtakia kila la heri.

Kwa bahati njema au mbaya, Sioyi anamuoa binti wa Edward Lowassa aitwaye Pamela. Hivyo, kwamba Sioyi alikwenda kutoa taarifa au kuomba ushauri, si hoja tena.

Hoja ni mwendokasi wa kisiasa unaowajumuisha wazazi, watoto na wakwe; na katika hili, Lowassa aliweka nguvu nyingi kupitia mtandao wake kuhakikisha mkwe wake anapita.

Katika hili, kwa mara nyingine, dola ya CCM ikashindwa na mtandao wa CCM ulioongozwa na kivuli cha Lowassa.

Kikwete ambaye alionekana kutotaka Sioyi, akaamua kumuunga mkono; ama kwa kuzidiwa nguvu na mtandao wa Lowassa au tu kwa sababu wote wawili hawana huruma na CCM pale kinaposhutumiwa na watu kuwa kinakumbatia rushwa.

Kama Kikwete angekuwa na uchungu na CCM asingeruhusu Sioyi awe mgombea wa CCM katika uchaguzi huu kwa sababu hata wateule wa rais walio mkoani Arusha katika vyombo vya dola, wanasema wana ushahidi kuwa mgombea huyo alitumia rushwa katika chaguzi zote mbili.

Madai ya Kikwete kuwa hata baadhi ya wabunge wa Arusha waliwahi kukamatwa na TAKUKURU na baadaye kuachiwa, hayana maana yoyote kwa sababu kuachiwa hakuna maana kuwa rushwa haikutolewa.

Kuteuliwa kwa Sioyi kuna sura nyingine isiyofahamika kwa watu wengi. Kimsingi, Kikwete hakuwa na nafasi ya kutosha kumkataa Sioyi bila kusutwa na dhamiri yake. Ni Jakaya huyuhuyu aliyekuwa mzee rasmi wa “kumtoa” Pamela kwa Sioyi siku walipooana.

Wakati huo hapakuwa na mashaka yoyote kwamba Lowassa na Jakaya ni marafiki. Kwa kumbukumbu hiyo, Jakaya bado ni “baba-mkwe” wa Sioyi.

Katika siasa za taifa letu zilizogubikwa na unasaba, si rahisi kumkataa mtoto anayetafuta kurithi mikoba ya baba yake.

Upo ukweli mwingine usiotajwa hadharani kuwa Kikwete ndiye alimshauri Sioyi kuingia katika kinyanganyiro hiki.

Alipoenda katika mazishi ya baba yake, alimshika mkono na kumshauri avae viatu vya baba yake na kufuata nyayo zake.

Pamoja na kwamba Sioyi kwa haiba yake si mwanasiasa, na kwamba hata masuala madogo ya kisiasa yanampa taabu sana kuyashughulikia, alitiwa moyo sana na maneno ya Kikwete; ndipo akaamua kuingia katika kinyanganyiro hiki kinyume na mapenzi ya baadhi ya wazazi wake waliobaki.

Ukiuchambua mtiririko huu wa uhusika wa Kikwete na Lowassa katika kinyanganyiro cha ubunge wa Arumeru, utagundua, pasipo shaka, kuwa watu hawa wawili hawana huruma kwa chama na taifa kwa jumla.

Watu wamefikia hatua ya kudai kupeana sumu na kuuana; kuchukiana pasipo kusameheana; na hata wengine kuishi maisha ya mashaka kwa sababu ya watu hawa wawili wasiojua kujali maslahi mapana ya kitaifa.

Watendaji wa chama, bunge na serikali wamewekwa katika hali ngumu ya kimaamuzi kwa sababu ya miamba hii miwili.

Usalama wa nafasi za watendaji unatokana na hesabu ya watendaji hao katika kuhakikisha wanawajua watu hawa wawili wanataka nini katika suala husika.

Wale wanaomuunga mkono Lowassa mara zote wamekuwa “salama” mbele ya Lowassa na mbele ya Kikwete; lakini wale wanaomuunga mkono Kikwete hawako “salama” mbele ya Lowassa na mbele ya Kikwete.

Hii ni kwa sababu Kikwete haaminiki katika kuwatetea na kuheshimu misimamo yao; wakati Lowassa yuko tayari kukesha akiwatetea watu wake.

Baadhi ya watendaji serikalini wanadai kuwa imefikia hatua hata Kikwete kulalamikia nguvu ya Lowassa.

Kama hivyo ndivyo, basi Kikwete anagwaya mbele ya Lowassa. Lakini kama bado Lowassa anaonekana kwa Kikwete kuwa “siyo mtu safi,” basi kuna kila sababu ya kuamini kuwa msimamo wa Kikwete kuhusu Lowassa ni wa bandia.

Kama ni msimamo bandia, basi ni ule uliojengwa rasmi kwa dhana ya kupoteza wakati tu, ili baadaye Kikwete aweze kumpisha Lowassa afanye atakalo.

Huu basi ni msimamo unaojenga hisia kuwa hata Kikwete si msafi; na ameambiwa hivyo na Lowassa lakini akashindwa kukanusha.

Kama huu ndio ukweli, usalama na amani ya Watanzania vimewekwa mikononi mwa watu hawa wawili wasio na chembe ya huruma kwa chama, serikali na taifa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: