Kikwete, Lowassa wamekosana nini?


Kondo Tutindaga's picture

Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 20 April 2011

Printer-friendly version
Rais Kikwete na Edward Lowassa

RAIS Jakaya Kikwete ameshutumiwa muda mrefu sasa kwa kuonekana anamkingia kifua swahiba wake wa siku nyingi, Edward Lowassa.

Rekodi yake ya utendaji au ya kutotenda, kwa sehemu kubwa imetiwa doa na urafiki wao unaoanzia mbali.

Historia ya wawili hawa ina mambo mengi yasiyojulikana wazi lakini kwa kuwa urafiki wao, ama unasabisha maumivu kwa nchi au una manufaa kwa taifa, iko haja ya wananchi kutaka kujua undani wa urafiki wao na mipaka ya urafiki wao katika mustakabali wa taifa letu.

Naweza kusema, baada ya kuwa nimezungumza na wote wawili kuwa, Lowassa alikuwa anampenda na kumheshimu sana Kikwete hadharani na nyuma ya pazia, lakini sina hakika kama Kikwete ana sura moja katika mahusiano haya. Historia itatueleza siku moja.

Baada ya kumalizika kwa vikao vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mjini Dodoma wiki mbili zilizopita, vilivyopachikwa jukumu la “kujivua gamba,” yamesikika mambo mengi midomoni mwa wanasiasa kuhusu uhusiano wa watu hawa wawili.

Pamoja na kelele nyingi zinazopigwa sasa na makada wa chama hicho na viongozi wapya katika sekretariati yake, hususani kuhusu hatima ya wanaoitwa “mafisadi ndani ya chama,” ukweli unabaki kuwa anayesakamwa ni Lowassa.

Pamoja na kwamba Rostam Aziz ndiye mtendaji mkuu wa kundi hilo na pengine kubeba lawama nzito zaidi ya wengine; ni Lowassa anayeonekana kuwa tishio la dola na chama chake kwa sababu ndiye pekee katika kundi hilo mwenye historia ya kuutaka urais tangu mwaka 1995.

Hii ina maana kuwa, ni salama kwa yeyote kufanya ufisadi bila kuutaka urais; lakini ni hatari kufanya ufisadi kisha ukataka urais.

Hili ndilo linaleta kizunguzungu ndani ya CCM na hakitakwisha mpaka pale tutakapojua ukweli kuhusu kina na mapana ya uhusiano kati ya Kikwete na Lowassa.

Kujua upana wa mahusiano yao, kutatusaidia pia kujua ni kitu kipi kimewakosanisha kufikia hatua hii tunayoiona.

Kwani licha ya vyombo vya habari kuanza kutabiri mapema sana wakati Kikwete akigombea urais mwaka 2005, kuwa waziri mkuu wake atakuwa Lowassa, Kikwete aliendelea na mpango wake huo.

Ilipotokea kashfa ya mkataba tata wa Richmond na kusababisha Lowassa ajiuzuru, kauli ya kwanza ya Kikwete hadharani juu ya tukio hilo ilikuwa kwamba ni “ajali ya kisiasa.” Kauli hii ilifanya mlima kuwa kichuguu(!).

Kilifuata kimya fulani kabla watu hawa wawili hawajaanza kukutana tena mara kwa mara kwa mpango maalum uliohakikiwa na marafiki zao au wao wenyewe.

Ilibidi washauri wa karibu wa Kikwete waonane na Lowassa kabla hawajamshauri juu ya jambo lolote zito; ilibidi pia Kikwete apate ushauri wa Lowassa hasa kwa masuala ya chama na uendeshaji wa baraza la mawaziri.

Katika matukio ya kifamilia, waliweka utaratibu wa kutembeleana usiku wakati wageni wengine wamepungua; na kwa hakika ilionekana wazi uhusiano wao unashamiri na kuwafanya baadhi ya watendaji serikalini na bungeni kuwa na wasiwasi juu ya hatima ya uhusiano huo.

Vyombo vya habari vilipododosa sana juu ya uhusiano huo, Lowassa alijitokeza hadharani na kudai yeye na Kikwete “hawakukutana barabarani.”

Kauli hii ilifuatiwa na mikakati kadhaa ya Lowassa kutaka asafishwe kwenye chama na ndani ya bunge; na mikakati hii, pasipo shaka, ilipata baraka za Kikwete, lakini ikagonga ukuta na kulazimika kujipanga upya.

Mtiririko huu ulikuja kutiwa dosari na kuwepo kwa Bernard Membe karibu na Kikwete; jambo lililomfanya Lowassa adai kusafishwa kwa spidi ambayo Kikwete asingeimudu.

Kusitasita kwa Kikwete katika suala la kusafishwa kwa Lowassa kuliibua mashaka upande wa Lowassa na kuchochea uhasama kati ya Lowassa na Membe, huku Kikwete akishindwa afanye nini na marafiki zake waliomweka madarakani lakini sasa hawapatani tena.

Haishangazi sasa kuona wote wametupwa nje ya Kamati Kuu (CC) ya chama chake kwa sababu Kikwete anaumudu sana mtindo huu wa “wote wakose”.

Aliutumia kwenye UV-CCM wakati wa kinyanganyiro cha uenyekiti na akautumia pia wakati wa kinyanganyiro cha uspika alipowatosa Samwel Sitta na Andrew Chenge.

Mpaka hapa, ukiondoa mgogoro kati ya Membe na Lowassa, bado hakuna ushahidi wala dalili za ni nini chanzo cha uhasama kati ya Lowassa na Kikwete.

Ili kumpoza Lowassa kwa muda, Kikwete alikwenda Monduli kumpigia kampeni na kutoa maneno mazito ya kumsifia mbele ya wananchi.

Ilisikika kuwa Kikwete alidai, Lowassa ni mtu mwema, mchapa kazi hodari, hakuna kama yeye na kuwa yaliyotokea huko nyuma ni mambo ya kawaida; yamepita na hayana uzito tena.

Alimwinua mikono na kumuombea kura. Jambo hili liliwahudhi wengi na kumshutumu Kikwete kwa nguvu sana.

Kwa upande wake, Lowassa alidai na angali anadai kuwa Kikwete alikwenda Monduli kuomba kura zake mwenyewe kwa sababu hata bila Kikwete bado yeye angeshinda bila taabu yoyote.

Alisema Kikwete anamuhitaji sana Lowassa kuliko yeye Lowassa anavyomuhitaji Kikwete.

Kwa watu ambao wamekaa karibu sana na watu hawa wawili, tangu chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na hatimaye kwenye chama na serikalini, wanadai kuna mambo mawili yanayoweza kuwa yameingilia urafiki wao.

Mambo hayo yanaweza kuwa ni “mgawo” au “uchonganishi” ulioambatana na usaliti katika mambo nyeti.

Jitihada za huko nyuma za  kuwatenganisha ziligonga mwamba kwa sababu wawili hao waliweza kukutana na kuchambua tofauti zao au kuvumiliana.

Hata siku za karibuni katika semina ya wabunge wa CCM iliyofanyika Ubungo Plaza, Kikwete alimrushia kijembe Lowassa kwa kusema kuwa pamoja na kuwa Lowassa anakunywa pombe (konyagi na brandy) wakati yeye Kikwete hanywi pombe, lakini bado wanaweza kukutana maeneo yao na kila mtu akanywa kinywaji chake bila shida yoyote.

Wanaodai mgawanyiko unatokana na  “mgawo,” wanamtuhumu Rostam Aziz wanayedai ni kiranja wa kukusanya kwa niaba ya chama na shujaa wa kugawa.

Hili laweza kuonekana kama jungu, lakini ni mapema mno kulipuuza.

Wanaodai ni uchonganishi na usaliti, wanamtuhumu Yusuf Makamba na Ridhiwani Kikwete kwa kusuka mpango mahsusi wa kumchonganisha Lowassa na Kikwete huku wakiitumia UV-CCM.

Mzengwe wa Makamba kugoma kujiuzulu na kudai waondoke wote, ilikuwa ni sehemu ya sinema iliyoandaliwa kisanii kati ya baba, mwana na Makamba.

Swali la kujiuliza ni hili? Nini gharama ya usaliti, uchonganishi na “dhuluma ya mgawo” kwa taifa letu na chama chetu?

Bila shaka jibu wanalo Lowassa na Kikwete.

0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: