Kikwete, Luhanjo, Jairo ni zimwi likujualo halikuli likakwisha


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 23 November 2011

Printer-friendly version
Tafakuri

WAKATI wa sakata la Richmond watumishi wawili waandamizi wa serikali waliotakiwa kuwajibishwa, hawakufanywa lolote licha ya azimio la Bunge kutaka iwe hivyo mwaka 2008.

Serikali ilivuta miguu kwa makusudi na kuwaacha hadi walipostaafu utumishi wa umma. Hawa ni pamoja aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika na Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, Arthur Mwakapugi.

Safari hii, Bunge limeazimia tena juu ya sakata jipya la Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo. Huyu amehusishwa na uchangishaji wa fedha kwa ajili ya kushawishi upitishwaji wa bajeti ya wizara yake wakati wa mkutano wa Bunge la Bajeti la mwaka huu.

Katika azimio hili, watumishi watatu waandamizi wa serikali wametakiwa wawajibishwe. Hawa ni Jairo mwenyewe, Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh.

Taarifa ambazo zilivuja mapema wakati kamati dhidi ya Jairo iliyoongozwa na Mbunge wa Tunduru, Ramo Makani (CCM) ikiendelea na uchunguzi zilisema, Luhanjo anastaafu utumishi wa umma 9 Desemba 2011.

Sasa serikali inakabiliwa na kibarua kingine cha kutekeleza azimio la Bunge. Swali linalobakia vinywaji mwa wengi ni hili: Je, itaawadhibu watumishi hawa? Kwa uzoefu Richmond ambayo si tu utekelezaji wa maazimio ya Bunge yalisuasua, bali ilionyesha kutokuwa tayari kuwashughulikia wahusika wakuu wa sakata hili baada ya wale viongozi wa kisiasa – aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa na waliopata kuongoza wizara ya nishati na madini, Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha kujiuzulu wenyewe.

Hata hivyo, afari hii, mawaziri William Ngeleja na naibu wake, Adam Malima, wamepitwa kando na kimbunga cha Bunge. Hali hii inatoa nafasi kwa watendaji serikalini kujitazama na kuchukua hatua wenyewe, kabla ya kuwajibishwa.

Wiki mbili zilizopita nilisema, “Kikwete na mtego wa kuamua kati ya Jairo ama Pinda.”

Kwamba Kikwete aliingilia kati sakata la Jairo kwa kumpeleka likizo licha ya ukweli kwamba Luhanjo alikuwa amekwisha kutangaza kwa mbwembwe zote kuwa Jairo anarudi kazini kwa kuwa hana hatia.

Kuibuka kwa Kikwete kumpeleka Jairo likizo, kwa wengi kulitafsiriwa kama juhudi za kunusuru mgongano wa mihimili ya dola – serikali na Bunge.

Ingawa hata hivyo, kwa upande mwingine kulikuwa na kila dalili ya kuepusha mgangano wa wateule wake kwa maana ya Luhanjo, Jairo na Mzengo Pinda, ambaye aliliambia Bunge kuwa Rais alikuwa anashughulikia suala la Jairo, lakini kwa mshangao wa wengi akaibuka Luhanjo na kumsafisha Jairo kwa mbwembwe nyingi za kuudhi si wabunge tu, bali hata wananchi wanaotaka uwazi na uwajibikaji wa matumizi ya kodi zao.

Mgongano huu wa Pinda, Luhanjo na Jairo, ndiyo iliyokuwa shughuli pevu ya Kamati Teule ya Bunge.

Kwanza, watu wamekuwa wanajiuliza, hivi Luhanjo alimwagiza Utouh kuchunguza mambo ya Jairo, kisha akamsafisha bila rais kuwa na taarifa wakati tayari Pinda alikuwa ameshaliambia Bunge kuwa suala la Jairo mwenye nguvu nalo ni Rais.

Kwa maana hiyo, kama awali Pinda alitegemea rais afanye maamuzi kuhusu Jairo kwa tabia yake ya kuchangisha fedha bila idhini na hata matumizi yake yakiwa ya kutiliwa shaka, lakini akashangazwa na maamuzi yaliyochukuliwa na Luhanjo, tena kwa kejeli.

Kwa kuwa sasa ripoti ya kamati ya Makani imewekwa wazi, kilichotokea ni dhahiri kwamba heshima ya Pinda imelindwa na kwa maana hiyo Bunge sasa limejihakikishia kwamba hadhi yake haiingiliwi hivi hivi na wale wanaodhani kuwa ni wateule wa rais au wako karibu na rais.

Ingawa Bunge linajiona kuwa na ushindi katika kipindi cha kwanza cha mchezo kwa kuibuka na ripoti ambao imewatia hatiani Jairo, Luhanjo na Utouh, lakini bado linakabiliwa na kazi inayoelekea kufanana na ile ya Richmond, kwamba joto limekuwa juu wakati kujadili taarifa, lakini baadaye upepo utageuka na hata Spika Makinda anaweza kufuata nyayo za mtangulizi wake, Samwel Sitta, ambaye alijipambanua kama spika wa kasi na viwango, lakini mwishowe akaimaliza hoja ya Richmond kwa aibu.

Sitta alifunga mjadala wa Richmond bila serikali kutekeleza maazimio karibu 17 ya Bunge.

Siku Makani anawasilisha taarifa ya kamati alisema walipata ushauri kutoka kwa Katibu wa Bunge la Uingereza ambaye alisema kuwa serikali iliyoko madarakani ni lazima ijitahidi kufanya mambo ambayo hayataliudhi Bunge lake kwa njia inayoonyesha madaraka yake yanamomonyolewa.

Kwa sasa wabunge wanaona kuwa wamepata kile walichotaka, lakini bado hitimisho la suala hili linategemea zaidi utayari wa serikali kutekeleza maazimio yote.

Je, serikali itatenda kama Richmond ilivyofanywa kwa Richmond au safari hii itaonyesha uwajibikaji na uwazi?

Kwa vyovyote itakavyochukuliwa, Rais Kikwete amejikuta katika mtihani mwingine mkubwa na mzito. Lakini ana furaha moja kwamba ana waziri mkuu mtulivu, angekuwa ni mtu mwenye jazba saa hizi Pinda angekuwa anaitwa waziri mkuu mtaafu kwa kuwa kuna kila ushahidi Luhanjo alimdharau na kumdhalilisha.

Hata hivyo, furaha hii ya wabunge, Pinda na hata Rais, inaweza kuwa ya muda sana kama ugonjwa wa uswahiba, kulindana na kubebana ndani ya mfumo wa utendaji kazi serikalini utapewa nafasi tena safari hii.

 Luhanjo anaondoka 9 Desemba 2011, je, ni mwendelezo wa ya akina Mwanyika na Mwakapugi, au ni mwanzo mpya wa kuwajibishana hata kama utumishi umebakiza saa kadhaa?

Hili linasubiri nguvu na maamuzi ya Rais. Kwa Jairo, ni mwisho wa utumishi wa umma au anaandaliwa ofisi ya ubalozi nje ya nchi. Jairo na Luhanjo ni watu waliokaa karibu na Kikwete kwa kitambo, ingawa Luhanjo ni zaidi sana, kwa maana hiyo kuna uwezekano mkubwa wa mambo kuachwa kama yalivyo kwa kuwa yapo madudu mengine mengi mno yamechwa hivyo hivyo bila kuchukuliwa hatua yoyote na serikali.

Mwenye kubishia hili na atupe majibu ya hatua dhidi ya kampuni ya Kagoda Agriculture Limited iliyokwapua Sh. 40 bilioni kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA); hatua dhidi ya wezi wa rada ya bei mbaya; hatua dhidi ya Meremeta, Mwananchi Gold na Deep Green.

Haya ni mambo ambayo yamegusa ama maswahiba wa wakubwa, au wakubwa nao walionjeshwa. Sijui Kikwete atafanya nini kwa Luhanjo na Jairo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: