Kikwete mbeba mzigo wa kiburi na chenga za Chenge


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 15 April 2008

Printer-friendly version
Andrew Chenge

YAPO mambo mengi aliyozushiwa Andrew Chenge, Waziri wa Miundombinu ambayo mengi watu waliyaona kama mambo ya mtaani tu. Kwa mfano, niliwahi kusikia Chenge alikuwa akisafirisha suti zake kwa DHL kwenda London, Uingereza kufuliwa.

Hii ilikuwa wakati akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akiamini Tanzania kulikuwa hakuna kampuni ya kueleweka ya ufuaji nguo.

Lakini pia lipo jingine la kilimbukeni alihusishwa nalo; kila alipokuwa akisalimiana na watu alitafuta upenyo na kwenda kunawa mikono yake na kupaka mafuta laini.

Chenge alipata kuhusishwa na ukiukaji wa misingi ya utendaji, alipokuwa kiongozi wa Salander Bridge Club. Inadaiwa baada ya kushindwa kwa muda mrefu kuitisha mkutano wa wanachama, baadhi ya wanachama waliamua kujiorodhesha ili kushinikiza mkutano uitishwe.

Wakati orodha hiyo ikiwa ukutani na watu wengine wakihamasishwa kujiandikisha ili kumlazimisha bwana mkubwa kuitisha mkutano, Rais Ali Hassan Mwinyi alimteua Chenge kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Habari zinasema kutokana na unafiki wa Kitanzania, orodha ile ilipotea kitatanishi. Hakukuwa tena na shinikizo la kumtaka aitishe mkutano kwa sababu si tu kwamba ujasiri wa wanachama ulikuwa umeyeyushwa na madaraka mapya aliyopewa, bali sasa wengine walianza kukaa mkao wa kupata lolote kutoka kwake.

Hayo ni simulizi. Haya yanayofuatia, nina uhakika nayo maana niliyashuhudia. Kwamba Chenge amejaa kiburi si jambo la kuuliza! Ni kiburi kikubwa kwani aliwahi kukionyesha kwa wabunge kati ya 1995-2005 akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Nitaeleza machache.

Baada ya Bunge kupitisha sheria ya kuvunjwa iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) na kuundwa NBC 1997 Limited na National Microfinance Bank (NMB) mwaka 1997, pamoja na kuanzishwa kwa kampuni tanzu ya NBC Hodings Limited ili kusimamia mali za iliokuwa NBC ambazo hazikugawiwa kwa NBC 1997 wala NMB, ofisi ya Mwanasheria Mkuu ilicheza faulo.

Faulo hiyo ni kutunga sheria kinyemela kwa kuiondoa iliyokuwa National Bureau De Change kutoka NBC Holdings ili ionekane kama ni taasisi inayojitegemea.

Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ilijipa jukumu la kupora Bureau kinyemela bila shaka, ili kujinufaisha katika harakati za kupora mali za umma zilizopamba moto wakati wa utawala wa Benjamin Mkapa. Wabunge makini akiwamo Philip Magani, wakati huo akiwa ndiye Mwenyekiti wa Bodi ya NBC, na Arcardo Ntagazwa, walishtukia suala hilo na kuwasha moto mkali bungeni.

Baada ya Bunge kuchunguza suala hilo, ilithibitika ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iliingilia kazi za Bunge kwa kurekebisha sheria bila ya kuifikisha bungeni, ikilenga kupora Bureau hiyo iliyokuja baadaye kuwa Twiga Bankcorp. Wabunge walichachamaa wakitaka maelezo ya serikali.

Nakumbuka Waziri Mkuu wakati huo, Frederick Sumaye, alisimama na kuomba radhi kwa niaba ya serikali kuhusu ukiukwaji mkubwa wa taratibu uliotokea na kuahidi kurekebisha kasoro hiyo. Sumaye alikuwa muungwana ambaye kwa mara ya kwanza katika kipindi cha utawala wake nilimuona akiwa mkweli kwa alilokuwa akilisema.

Lakini pamoja na hatua ya Sumaye, Chenge aliibuka. Akasema, "kiti cha Mwanasheria Mkuu wa Serikali kimejaa!" Kebehi iliyoje dhidi ya wabunge pamoja na Waziri Mkuu aliyekuwa ameshasawazisha kasoro.

Kiburi cha Chenge kilijidhihirisha jinsi asivyoheshimu Bunge, wabunge na hata Waziri Mkuu amabye ndiye kiongozi wa shughuli za serikali bungeni.

Katika hali ya kawaida, Sumaye alikuwa na kazi moja tu, kumwomba Rais amuondoe Chenge kwenye wadhifa kwa kuwa alikuwa anafanya kazi yake kuwa ngumu. Hili halikufanyika, Chenge akaendelea kutesa hadi bwana mkubwa Mkapa alipomaliza kipindi chake Novemba 2005.

Baada ya kusikia hivi karibuni Chenge anachunguzwa kwa ukwasi aliojiwekea kwenye kisiwa cha Jersey, Uingereza akiwa na zaidi ya dola milioni moja za Marekani, kwenye akaunti yake, nimeanza kujua kiburi cha ofisa huyu kinakotoka!

Ni kiburi cha mtu aliyeshiba na kuvimbiwa, na unajua ukivimbiwa kuna uwezekano mkubwa wa kuharibu hali ya hewa. Chenge hakumtii Sumaye wala wabunge wa chama chake. Hakuwa na sababu za kuwatii maana yeye na bwana mkubwa walikuwa wanaruka mruko mmoja wa ndege wenye mabawa (manyoya) ya kufanana.

Bwana mkubwa Mkapa naye ukwasi wake haramu umekuwa ni mapambo kwenye magazeti ya Tanzania kwa zaidi ya mwaka sasa. Yeye (Mkapa) ameamua kukaa kimya. Kiburi kile kile cha swahiba wake. Kiburi cha ukwasi, cha kupumua, cha shibe, shibe iliyomlevya kiasi cha kushindwa kujua yeye ni Mtanzania na kwamba kujilimbizia fedha nyingi kiasi hicho ughaibuni ni usaliti kwa nchi masikini kama Tanzania.

Chenge alipochaguliwa kuwa waziri na Rais Jakaya Kikwete Januari 2006, watu walijiumauma na kuuliza, inakuwaje Kikwete ampe uwaziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Chenge wakati zikiwapo tuhuma nyingi mitaani za uchafu unaomgusa.

Mikataba kama ya IPTL, uuzaji wa NBC iliyotolewa kwa Makaburu wa ABSA sawa na bure! Watu waliguna lakini Rais Kikwete naye si tu alipuuza miguno yao, aliwazaba kibao wananchi mwaka jana alipofanya marekebisho madogo katika baraza lake la mawaziri kutokana na kuchemka kwa sakata la Richmond. Chenge aliondolewa Afrika Mashariki na kupelekwa Miundombinu, wizara nyeti na yenye kazi kubwa ya kujenga barabara ambazo ni kilio cha kudumu kwa wananchi na wawekezaji.

Hakuishia hapo tu. Alipolazimika kuvunja baraza la mawaziri ya Edward Lowassa na mawaziri wawili wengine kujiuzulu, kutokana na sakata lilelile la Richmond, Rais Kikwete alimrejesha Chenge pale pale miundombinu katika baraza jipya! Miguno mipya ikaendelea kuzizima.

Sasa Waingereza wametusaidia kumweka hadharani Chenge kuhusu namna alivyopata ukwasi mkubwa. Shaka iliopo si ya kwamba amepataje ukwasi huo, bali pia kwa kuwapo uwezekano wa kuhusiana na mabilioni ya rada iliyouziwa Tanzania kwa bei ya juu na Waingereza haohao wa kampuni ya BAE Systems.

Chenge yuleyule wa kusafirisha suti kwa DHL kwenda kufuliwa Uingereza, hadi kuogopa kuchafuliwa mikono kwa sababu ya kusalimiana mpaka kwa Chenge wa kiburi kwa Waziri Mkuu na wabunge, ni Chenge huyohuyo wa kumiliki ukwasi wa kutosha kula hadi aingie kaburini.

Haya yote yakitokea, Chenge anawajibika kueleza umma alivyopata ukwasi huu. Ni vema akatambua kuwa wakati umefika wa kuwa muungwana na kutambua kuwa ulevi wa ukwasi unaompa kiburi hautamsaidia kitu. Angeamua tu kuachia ofisi ya umma akaendelea na yake. Chenga na kiburi, safari hii havitamponya!

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: