Kikwete mpindishaji wa maana ya takrima


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 19 May 2010

Printer-friendly version
Tafakuri

HAKUNA ubishi kuwa mfumo wa siasa unaotumika nchini ni chimbuko kubwa la rushwa. Ndio njia kuu inayoasisi ufisadi. Kuna kila ushahidi kwamba ufisadi mkubwa na mbaya uliopata kufanywa katika taifa hili kwa miaka ya karibuni umeanzia kwenye uchaguzi.

Umetekelezwa kwa kutumia njia nyingi; mojawapo ni mpango haramu wa dola wa kuchota fedha nyingi katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zilizotunzwa kwenye akaunti ya madeni ya nje (EPA). Ni mpango kwa sababu ulitekelezwa chini ya maandalizi yaliyofanywa kwa ustadi mkubwa na watu walioteua mawakala kwa ajili ya kuchota fedha ili zisaidie mikakati ya ushindi ya chama tawala.

Ipo pia njia ya mgombea mmoja mmoja kwa kutumia ukwasi wake, uliotokana na njia chafu, anajitosa katika kinyang’anyiro lakini sera yake ikiwa ni kuhonga wapigakura.

Hapa, wagombea kura na wapigakura wanakutana kwenye gulio moja la kuchuuza kura! Njia zote hizi zinazalisha viongozi walioingia madarakani si kwa sababu ya ushawishi wao kwa umma wala si kwa kuitwa na wananchi ili wawaongoze, ila kwa sababu waligawa fedha na kushawishi kuingia madarakani.

Wote hawa ni wachafu, wananuka na wamekumbatia uchafu. Ni mafisadi kwa nia na vitendo vyao. Wakati harakati hizi zikiendelea, wapo watu wanaoitakia nchi mema, wakaenda mahakamani kuomba matumizi ya fedha kwa namna ambayo uchaguzi wa mwaka 1995, 2000 na 2005 ulishuhudia, kuwa ni haramu na kimsingi ni rushwa.

Upingaji wa utaratibu huu uliobarikiwa chini ya ‘takrima’ ndio umekuwa chimbuko la wizi na kila aina ya ghilba katika uchaguzi. Ufisadi mtupu. Kwa sasa ‘takrima’ imeharamishwa na kwa kweli ni kitu ambacho kama taifa kila mtu kwa imani yake anawajibika kwenda anakoabudu ili kutubu kwa ajili ya taifa.

Ni kuomba Mwenyezi Mungu azike mbali ufisadi huu ambao umetumika kupata viongozi wetu. Viongozi wa staili ya takrima hawana baraka. Iitwe kwa jina lolote, takrima inabaki kuwa hatari kwenye uchaguzi.

Utaratibu wa kuruhusu takrima katika sheria ya uchaguzi ni ajenda ya watu waliokuwa na fedha chafu na wakataka kuzitakasa kwa kuingia madarakani. Wakatumia fedha nyingi haramu kuhonga wapigakura na nyingine wakabakia nazo kwenye akaunti zao zilizopo mabenki ya nchini na ughaibuni.

Ni hizi zilizoishawishi mahakama ikatengua ushindi wa wabunge wengi walioingia mwaka 1995. Kwa bahati mbaya, pamoja na Mahakama kutengua matokeo ya baadhi ya wabunge, kwa sababu walihonga wapiga kura, serikali na chama tawala wakajipa ujasiri na kutunga sheria na kuitumbukiza kwenye sheria ya uchaguzi kubariki na kuhalalisha uchafu huo.

Haishangazi basi leo kumsikia Rais Jakaya Kikwete akiwaeleza viongozi wa dini eti ni vigumu kupiga marufuku takrima katika mazingira ya uchaguzi nchini.

Kwa maana hiyo, ingawa rais Kikwete anafahamu fika katika mchakato wa ndani ya chama chake takrima hairuhusiwi na amepata kuikemea, inakuwa ni vigumu zaidi kujua inakuwaje basi katika kinyang’anyiro cha kusaka madaraka ya dola iruhusiwe?

Kampeni ya nguvu inafanywa ili kupotosha maana ya takrima, ingawa utetezi unajikita katika ukarimu wa Kiafrika ambao hakuna anayeeleza ukarimu huu unatolewa na nani na katika mazingira gani.

Rais anaposema si rahisi kuwaita wazee wa Kichaga bila ya kuwapa mbege, anasema kweli maana hiyo ni mila yao wanayotumia watakapo kueleza shida zao.

Watu wa makabila mengine Tanzania hapana shaka nao watakuwa na mila wanazozizingatia kila wanapotaka kuwasilisha matatizo yao. Lakini dhana nzima ya ukarimu inatokana na kuitwa kuelezwa jambo; kwa maana hiyo kama ni kusaka urais, ubunge au udiwani ni kazi ya utumishi, yaani wananchi wanatafuta kiongozi wa kuwatumikia.

Hapo ndipo utasikia wanaosaka urais, ubunge, udiwani na hata nyadhifa za serikali za mitaa, wakijinasibu eti “nimefuatwa na wazee au wapiga kura wenyewe.”

Mtu anaposema kwamba ameitwa na wazee au wapigakura kama ni mgombea hajakosea hata kidogo. Ni sawasawa. Mahali pengine tumeona wananchi wakifika mbali zaidi na kuchanga fedha za kumchukulia fomu wanayetaka awatumikie.

Tumeshuhudia kwa mfano uongozi wa CCM kwa mikoa kadhaa wakiwasilisha fedha zinazoitwa za “kuchukua fomu” kwa Rais Kikwete. Hata baadhi ya wagombea ubunge wanapewa fedha na wapigakura wao ili wakubali mzigo wa kuwatumikia wananchi.

Takrima inapaswa kutoka kwa wananchi kwenda kwa mgombea, si vinginevyo. Ieleweke kuwa urais, ubunge na udiwani ni mzigo tena mzito wa utumishi; anayesukumwa kwa nia ya kweli kuubeba hawezi kuwaza kutumia fedha zake binafsi kuhonga wapigakura maana mara nyingi mtumishi hutafutwa na wale wanaomtaka.

Fikiria hivi: Kampuni X imetangaza nafasi za kazi, waombaji wanawasilisha maombi, yanachambuliwa na wanaitwa kusailiwa. Itakuwa ni maajabu ya firauni iwapo anayesailiwa ndiye ataandaa chai, eneo la kikao cha usaili na kulipa posho za jopo la wanaomhoji. Ikitokea mwajiriwa mtarajiwa akafanya hivyo, hizo fedha hakika itakuwa amezitoa kununua wale wanaotaka kumpa kazi. Na huu hauwezi kuwa utumishi wa kweli.

Ni kwa msingi huu, Rais Kikwete alipaswa kuweka mambo sawa alipokutana na viongozi wa dini jijini Dar es Salaam. Kwamba urais, ubunge na udiwani ni utumishi; ni wajibu wa kubeba mzigo; ni kukubali kutumwa kutumika. Katika mazingira kama hayo, ni vigumu kuelewa ni kwa maana gani sasa mtumishi anatumia fedha zake kuwalipa wale wanaomtuma kuja kuwatumikia.

Ingeeleweka sana kama wananchi wangechanga fedha na kumpa mgombea wanayemtaka ili akubali kubeba mzigo wa utumishi wa urais, ubunge au udiwani na si kinyume chake. Kauli ya Rais Kikwete kwamba takrima haiepukiki katika mazingira ya uchaguzi nchini, inaweza tu kueleweka kama wanaitoa wananchi katika kumshawishi mgombea akubali wamtwike mzigo wa kuwatumikia kwa kipindi cha miaka mitano.

Lakini inapokuwa mgombea ndiye anayejaalia takrima wananchi,huko ni kuhonga wapiga kura na ni kuvunja sheria za nchi. Mtenda kosa hili akishinda uchaguzi, anastahili kushitakiwa mahakamani ili anyang’anywe ushindi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: