Kikwete na mtego wa Jairo, Pinda


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 09 November 2011

Printer-friendly version
Tafakuri

MKUTANO wa Tano wa Bunge ulianza mjini Dodoma jana. Ni msimu mwingine wa tambo, vijembe na vibweka vya kila aina. Ni wakati mwingine kwa wananchi kushuhudia mapambano ya hoja miongoni mwa wawakilishi wao.

Mkutano huu utakuwa na mambo mawili makubwa, kwanza ni kupitishwa kwa muswada wa sheria wa kuanzishwa kwa kamati ya kuratibu mchakato wa kuandika katiba mpya.

Lakini pia ni mkutano ambao itawasilishwa ripoti ya Kamati Teule ya Bunge kuhusu Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, David Jairo na Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, juu ya kuchangisha fedha za kupitisha bajeti ya wizara yake.

Kwa kifupi kamati hii iliyoongozwa na Mbunge wa Tunduru Kaskazini (CCM) Ramo Makani, ilikuwa inatafuta undani wa mambo makuu mawili kwa ujumla, kwanza ni kama Jairo ana kesi ya kujibu kwa upande mmoja, na kwa upande wa pili kama Luhanjo ana kesi ya kujibu.

Sakata zima la Jairo kuchangisha fedha kwa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati na Madini kwa nia ya kusaidia mchakato wa upitishwaji wa bajeti ya wizara yake, ni jambo ambalo limegonganisha mihimili miwili ya dola, Bunge na Serikali (utawala).

Jairo alituhumiwa na wabunge kuwa amekusanya mamilioni ya shilingi, akayatumia ‘kuhonga’ wabunge. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Lodovicl Utouh, akakagua fedha hizo zilizokuwa zinapelekwa kwa Taasisi ya Jiolojia na Upimaji, na kumsafisha Jairo.

Ripoti hiyo ndiyo Luhanjo aliitumia ‘kukejeli’ wabunge. Wabunge waligeuka mbogo, na mwishowe waliamua kuundwa kwa Kamati Teule kuchunguza wakubwa hao wawili ndani ya mhimili wa utawala.

Uchunguzi wa Luhanjo unaweka historia mpya nchini kwa kiongozi mkuu katika utumishi wa umma kuchunguzwa na Bunge. Lakini si hivyo tu, utendaji wa Luhanjo kwenye suala hili umeiweka Ikulu njia panda.

Ni kwa mara ya kwanza pia mtu anayefanya kazi ndani ya Ikulu, akiwa ni mkuu wa makatibu wakuu, kwa maana hiyo mkuu wa utumishi wa umma akifanya kazi bega kwa bega na rais, anajikuta akitokea mbele ya Kamati Teule ya Bunge kama mtuhumiwa kusulubiwa.

Pamoja na ukweli kwamba Rais Jakaya Kikwete aliingilia kati kwa kumpeleka Jairo likizo, licha ya ukweli kwamba Luhanjo alikuwa amekwisha kutangaza kwa mbwembwe zote kuwa Jairo anarudi kazini kwa kuwa hana hatia, akapokewa kwa mbwembwe kali wizarani kwake, kama kuvishwa maua na gari lake kusukumwa, bado suala lake limebaki kuwa la kimgongano wa mihimili ya dola kwa upande mmoja, lakini kwa upande wa pili ni mgangano wa wateule wa Rais kwa maana ya Luhanjo, Jairo na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Mgongano huu wa Mizengo Pinda, Luhanjo na Jairo, ndiyo shughuli pevu ya Kamati Teule ya Bunge, lakini pia ndicho kibarua kigumu kuliko vyote alivyowahi kukutana navyo Rais Kikwete.

Ugumu unatoka wapi? Kwanza watu wanajiuliza, hivi Luhanjo alimwagiza Utouh kuchunguza mambo ya Jairo, kisha akamsafisha bila Rais kuwa na taarifa wakati tayari Waziri Mkuu Pinda alikuwa amekwisha kuliambia Bunge kuwa suala la Jairo mwenye nguvu nalo ni Rais kwa kuwa ni mteule wake?

Kwa maana hiyo, kama awali Pinda alitegemea Rais afanye maamuzi kuhusu Jairo kwa tabia yake ya kuchangisha fedha bila idhini na hata matumzi yake yakiwa ya kutiliwa shaka, lakini akashangazwa na maamuzi yaliyochukuliwa na Luhanjo, tena kwa kejeli, safari hii Kamati ya Bunge ambayo inaamini Bunge limedhalilishwa na mteule huyo wa Rais (Luhanjo) labda akimlinda rafiki yake Jairo, au kwa maelekezo ya bwana mkubwa, itamwacha tena Waziri Mkuu kama yatima asiye na mtetezi?

Katika mazingira kama haya, mambo kadhaa yanaweza kutokea kama kweli Rais bado anataka kulinda heshima ya Ikulu, heshima ya Waziri Mkuu na kama kweli bado anataka Bunge liendelee kuheshimu taasisi ya urais.

Moja, kwa kuwa Luhanjo anastaafu baada ya Desemba 9, mwaka huu, anaweza kuambiwa tu awahi kustaafu ili kujinusuru na moto wa kamati ya Bunge.

Kwa maana hiyo atabaki Jairo ambaye kisheria bado ni mtumishi wa umma na hajafikisha umri wa kustaafu kisheria. Huyu anaweza kuambiwa tu ama ajiuzulu, au Rais anaweza kusema ameondolewa rasmi Nishati ili apangiwe kazi nyingine.

Kwa kufanya hivyo, Rais atakuwa amemalizana na wateule waliolikoroga na kwa maana hiyo kumwepusha katika mvutano usio wa lazima na Bunge.

Lakini haya yanawezekana tu kama Rais aanataka kuufikisha mgogoro huu ukingoni mapema. Hata hivyo, kama ataamua kufuata njia ya mgogoro wa Richmond, anaweza kuacha kuchukua hatua yoyote ya haraka dhidi ya Jairo au Luhanjo, kwa kufanya hivyo atakuwa amemfanya Pinda aonekane kuwa mnyonge na dhaifu sana ndani ya serikali.

Atakuwa amefungua mjadala mpya juu ya nguvu na madaraka ya Waziri Mkuu kama kiongozi wa shughuli za serikali bungeni, kiranja wa mawaziri wote, lakini kubwa zaidi mtu ambaye hushauriana na Rais wakati wa uteuzi wa mawaziri wakati wa kuunda baraza la mawaziri.

Kwa bahati mbaya, Pinda ni aina ya pekee ya mawaziri wakuu ambao tumewahi kushuhudia. Inawezekana ni mtu mwenye uwezo mkubwa wa kuficha hisia zake za ndani, inawezekana pia kufanya kazi serikalini kama tekinokrati kwa miaka mingi kumemuumba upya kifikra na anavyofanya maamuzi, lakini katika hili hana pa kuficha uso wake kama Jairo atarudi kwenye nafasi yake.

Huu ndio mtihani wa Rais Kikwete. Je, atataka kuwa na mawaziri wakuu watatu na zaidi katika kipindi chake cha utawala au anataka amalize na wawili aliokwisha kuwateua?

Ni vigumu kujua ndani ya nafsi yake Rais Kikwete anawaza nini. Lakini kitu kingine muhimu kitakuwa kinasumbua nafsi yake, hiki ni vita vya kujivua gamba.

Tayari ana kazi pevu ya kupambana katika vita hii, ama moja kwa moja au kupitia kwa watu anaowatumia kama akina Nape Nnauye. Je, maji ya kujivua gamba yametulia au ndo kwanza yametibuka?

Katika mazingira ya uchaguzi mdogo wa Igunga, ndani ya CCM kuna mwenye ubavu wa kuthubutu kumfukuza mbunge ndani ya CCM?

Mkutano wa wenyeviti wa mikoa wa CCM na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Pius Msekwa, ulionyesha wazi kwamba vita ya kujivua gamba si nyepesi kama ilivyotarajiwa.

Vidonda na ugomvi wa tangu kuundwa kwa kamati iliyoongozwa na Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, ikiwa na wajumbe Msekwa na Abdulrahaman Kinana, kuhusu uhasama miongoni mwa wabunge wa CCM, ulijidhihirisha upya. Huu ni mzigo mzito ungali mabegani mwa Rais Kikwete.

0
No votes yet