Kikwete mtuhumiwa, tufanye nini?


Kondo Tutindaga's picture

Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 30 November 2011

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

UKURASA mpya kuhusu sakata la Richmond, umefunguliwa baada ya mambo mawili kutokea katika vikao vya Chama Cha Mapinduzi (CCM), vilivyomalizika mjini Dodoma Alhamisi iliyopita.

Kwanza, CCM imekubali kiungwana kuwa ile dhana ya kujivua gamba haiwezekani tena. Sababu ni nyingi.

Lakini Wilson Mukama, katibu mkuu wa chama hicho anadai dhana hiyo ilipotoshwa na vyombo vya habari na kuonekana kuwa iliwalenga baadhi ya watu tu wakati ililenga kusafisha chama chote na kwenye ngazi zote.

Wengine wanadai hata muasisi wa dhana yenyewe hajui alimaanisha nini na kama anajua anaogopa kusema hasa alimaanisha nini. Kwa hiyo busara imetawala na CCM ikakubali yaishe kiungwana.

Pili, jambo jipya limetokea, kwamba mwenyekiti wa chama, Rais Jakaya Kikwete – muasisi wa dhana ya kujivua gamba – naye ni mtuhumiwa muhimu wa kashfa ya Richmond.

Haya yameelezwa na rafiki yake Edward Lowassa, kwamba anajua kila kitu kuhusu Richmond na kuwa si tu alikuwa na taarifa bali aliruhusu mambo yaende kama yalivyokwenda.

Lowassa alijiuzuru uwaziri mkuu, Februari 2008. Ilikuwa ni baada ya Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza mazingira yenye utata katika mkataba wa kampuni ya kufua umeme ya Richmond, ilipohitimisha Lowasa apime uzito wa kashfa ile na kuchukua uamuzi yeye mwenyewe.

Aliamua kujizuru kwa kinyongo huku akidai kuwa kuna watu walikuwa wanamuonea wivu kwa nafasi yake ya uwaziri mkuu, lakini pia akadai alifanya hivyo kwa heshima ya chama na serikali.

Kampuni ya Richmond, siyo tu iliivunja serikali na kuiunda upya bali pia iliasisi makundi ya kimaslahi ndani ya CCM, serikalini na hata katika Bunge.

Wahanga wa Richmond ni wengi. Wamo mawaziri, Spika wa Bunge la Tisa, Samwel Sitta, watendaji wa chama, watendaji wa vyombo vya dola na mashinikizo yasiyokwisha katika vyombo ya utoaji haki.

Tangu alipoingia serikalini mdudu huyu, hapajawahi kuwa shwari kwa sababu baada ya Richmond kuiva na kukomaa alibadilika na kuitwa Dowans na kuingia mkataba mwingine tata na TANESCO.

Bunge lilipotaharuki na kushinikiza mkataba huo uvunjwe na ukavunjwa, Dowans alifungua kesi katika mahakama ya kimataifa kudai fidia lakini huku nyuma Dowans akauza mitambo yake kwa Symbion ambalo nalo limeingia mkataba mwingine na Tanesco.

Dowans alishinda kesi na sasa anadai mabilioni ya fedha huku Rais Kikwete akituhumiwa kuwa sehemu ya mdudu Richmond.

Kumbe nguvu ya Richmond iliyoonekana katika jinsi ya kupata mikataba tata kwa haraka na hata kubadilika sura na majina, ilitokana na kusimamiwa na mkuu wa nchi! Haya ni madai mazito dhidi ya mkuu wa nchi. Kwa kuwa rais wetu amekuwa ni mwimbaji mzuri wa wimbo wa utawala wa sheria, anapaswa alione hili suala kwa miwani tofauti.

Kwanza, azione hizi si tuhuma za kawaida. Zile tulizozoea kusikia juu ya maisha binafsi ya rais na familia yake ambazo hata yeye aliwahi kuzipuuza kwa kuziita kuwa ni “kelele za mpita njia.” Tuhuma za sasa zinahusu uhai wa taifa na hivyo, si vema kupuuzwa kwa sababu tuhuma hizi zinagusa mgongano wa madaraka kati ya bunge na serikali.

Pili, kwa mkuu wa nchi kutuhumiwa kuwa mhalifu katika kashfa ya Richmond kunaibua mgongano hatari wa maslahi. Hii ni kwa sababu hatujui kuhusika kwake ni kwa kiwango kipi: Je, ni kwa kiasi cha yeye kuwa mmiliki wa Richmond au ni kwa yeye kujua tu jinsi Richmond ilivyopata mkataba na kuingia nchini?

Yote mawili ni mazito. Rais kuwa mmiliki au sehemu ya mmiliki wa Richmond inakiuka maadili ya utawala bora pale kiongozi anapofanya biashara na taasisi anayoiongoza kwa sababu anajipangia bei na si ajabu hata akakwepa kodi.

Huu unaitwa mgongano wa maslahi; kwa kuwa sasa chini ya mwavuli wa utawala wa sheria Tanesco inapaswa kuilipa Dowans ambayo ni mtoto wa Richmond, ni wazi sasa kuwa Kikwete ni mnufaikaji wa mabilioni hayo ya walipa kodi ikiwa tuhuma za Lowassa zitathibika kuwa ni za kweli.

Kama kuhusika kwa rais ni kwa kiwango cha yeye kujua jinsi Richmond ilivyoingia mkataba na Tanesco wakati imethibitika Richmond ni kampuni ya kitapeli, hili linazua shaka juu ya umakini na usafi wa rais na vyombo vyake.

Suala la umeme linagusa usalama wa nchi na kwa rais kuonekana kuwa mhujumu wa usalama wa nchi na watu wake, ni suala lisiloweza kufumbiwa macho. Ikumbukwe kuwa kelele za watu wengi kuhusu usimamizi wa maadili ya uongozi katika taifa letu yamekuwa hayashughulikiwi na sasa twaweza kuamini ni kwa sababu rais wetu anajishuku kuwa akishughulikia au kusimamia maadili ya uongozi yataibuka masuala mengi na kashfa zinazomhusu katika eneo hili nyeti la maadili ya uongozi.

Kw sababu ya kukosa usimamizi wa maadili ya uongozi, tumeshuhudia viongozi wanaotajwa na sheria ya maadili ya viongozi wakishindwa kujaza fomu za kutaja mali zao; tumesikia mara kwa mara orodha ndefu ya mali za rais wetu na familia yake na tumeona kigugumizi cha rais kushindwa kumgusa mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Aidha, tumeshuhudia hata malalamiko mengi kutoka kwa watendaji na wateule wa ikulu juu ya utitiri wa miradi bubu ya mke wa rais na watoto wake na hata uchangishaji wa fedha kutoka wafadhili  zikiingia  katika mfuko wa WAMA.

Mambo haya yanaweza kuwa ni matokeo au dalili za rais wetu kujihusisha na vitendo vya rushwa na ufisadi uliojikita katika kashfa kubwa nchini. Narudia tena, hizi ni tuhuma nzito kumhusu rais, ingawa bado hazijathibitishwa.

Je, tufanye nini na rais mtuhumiwa katika kashfa ya Richmond? Katiba yetu yenye viraka inatamka kuwa rais hashtakiki mpaka amalize kipindi chake na bado hakuna uhakika wa kushtakika hata baada ya kustaafu kwa kile kinachoitwa “kinga” kwa makosa ya kiutendaji.

Lakini, utamaduni wa utawala wa taifa letu si tofauti sana na tamaduni nyingine za nchi zinazofuata na kuheshimu utawala wa sheria. Napendekeza njia tatu:

Kwanza, chama chake kina nafasi ya kumhoji na kujua ukweli wa tuhuma hizi. Si mara ya kwanza kwa chama hicho kuchukua hatua dhidi ya viongozi wa juu wanapotuhumiwa kujihusisha na kashfa zinazowapunguzia uwezo wa kuongoza taifa.

Ni wazi uwezo wa rais kuongoza chama na serikali umepungua sana kiasi cha baadhi ya watu kuamini amerogwa.

Pili, rais kwa nia njema na uungwana, apishe uchunguzi huru wa suala hili ili kuondoa fikra za kuwa aliyemtuhumu alikuwa mfa maji anayetapatapa ili asizame peke yake.

Ikibainika Lowassa alimtuhumu rais kwa lengo la kumchafulia jina lake, achukuliwe hatua kubwa na liwe fundisho kwa wengine wanaopenda kutuhumu na kujenga fitna dhidi ya watawala wetu.

Lakini ikibainika kuwa tuhuma hizi zina ukweli wakati taifa limeteseka kwa zaidi ya miaka 4 sasa chini ya kivuli cha Richmond, basi rais naye ashauriwe kupima uzito wa madhara ya Richmond kwa taifa na afanye uamuzi wa kiungwana.

Akifanya hivyo, atakumbukwa na vizazi kwa uungwana huo. Tutake tusitake, Richmond ni kashfa mbaya inayoendelea kulitesa taifa. Uzalendo wa rais umepata kipimo kwa tuhuma zilizotolewa dhidi yake na rafiki yake.

tutikondo@yahoo.com
0
Your rating: None Average: 3.5 (2 votes)
Soma zaidi kuhusu: