Kikwete na Ngulla: Nani anajua zaidi sheria za kazi?


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 26 August 2008

Printer-friendly version

NANI anajua zaidi? Rais Jakaya Kikwete au Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Nestory Ngulla?

Kwa mwezi mmoja sasa viongozi wa Tucta wameshikilia mradi mmoja tu: Watumishi wa umma kugoma kwa siku tatu nchi nzima tangu 25 hadi 27 Agosti mwaka huu.

Shabaha yao ni kushinikiza serikali kuwalipa malimbikizo yao ya mishahara ya tangu Janyari mwaka huu.

Alhamisi iliyopita Rais Kikwete alisema mgomo unaopangwa na Tucta siyo halali kwa kuwa haukufuata taratibu. Alitaja utaratibu kuwa notisi ya siku 60 kabla ya kuchukua hatua hiyo.

Kauli ya rais aliyoitoa bungeni iliendana na kauli ya Waziri wa Utumishi, Hawa Ghasia ambaye wiki mbili zilizopita aliwakosoa Tucta akisema hawakufuata utaratibu wa kugoma; na kwamba mgomo wao siyo tu haukubaliki bali pia ni batili.

Lakini Ngulla anasema Rais Kikwete amepotoshwa. Anasema sheria ambayo waziri ananukuu ni ya zamani. Sheria mpya, anasema Ngulla, inaweka  notisi ya siku 30 tu kabla ya kufanya mgomo.

Sheria mpya ya Uhusiano Kazini ya mwaka 2004, anasema Ngulla, inatoa siku 30 za chama cha wafanyakazi kutoa notisi kwa Baraza la Kazi, Uchumi na Ustawi wa Jamii kabla ya kufanya mgomo.

“Sisi tumefanya hivyo. Tumefuata sheria iliyopo. Tumetimiza siku 30 zinazohitajiwa. Rais ameshauriwa vibaya,” anasema Ngulla.

Sasa nani amemshauri rais vibaya? Waziri Ghasia? Hajui sheria hii? Na Nani kamshauri vibaya Ghasia? Wataalaam wa masuala ya wafanyakazi na mwanasheria wa wizara?

Hata hivyo Ngulla anasema wanachotaka wafanyakazi ni malipo yao na kusisitiza kuwa Tucta imeamua wasigome kwa kuheshimu kauli ya mkuu wa nchi na siyo ile ya awali ya mawaziri watatu.

Katika hotuba yake bungeni wiki iliyopita, rais amewaambia wafanyakazi kwamba aangalaua wangesubiri hadi tarehe 3 Septemba na kama hawatalipwa ndipo wafikirie kufanya mgomo.

Hata wafanyakazi wakianza kugoma tarehe aliyosema rais, zitakuwa hazijatimia siku 60 alizosema na zile ambazo waziri wake alitamka.

Aidha, waziri aliwaambia waandishi wa habari wiki mbili zilizopita kuwa serikali ingewalaipa wafanyakazi mwishoni mwa mwezi huu na kwamba viongozi wa Tucta wasitafute umaarufu wa bure huku wakijua serikali imeishaamua kuwalipa.

Katika mkutano na waandishi wa habari, mawaziri watatu – Ghasia, Waziri wa Fedha Mustapha Mkullo na Profesa Jumanne Maghembe, walisema wamo katika hatua za mwisho kuwalipa wafanyakazi.

Serikali ilitangaza nyongeza ya mishahara kwa kima cha chini kutoka Sh. 84,000 kwa mwezi hadi Sh. 100,000, lakini hadi sasa haijalipa kiwango hicho kipya na kusababisha wafanyakazi kuandaa mgomo wa kudai walichopewa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: