Kikwete ni zaidi ya Mkapa na Mwinyi


Dunia Ibrahim's picture

Na Dunia Ibrahim - Imechapwa 01 September 2009

Printer-friendly version
Mwinyi, Kikwete na Mkapa

MAKALA sita zilizochapishwa mfululizo katika MwanaHALISI wiki tano zilizopita, ndizo zilizonisukuma kupata ujasiri wa kumtetea Rais Jakaya Kikwete, dhidi ya hoja za wapinzani wake wa kisiasa.

Mjadala katika makala hizo unatokana na hoja iliyoibuliwa na Mwenyeiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, kwamba Rais Kikwete ameshindwa kazi.

Hoja ya Profesa Lipumba imepingwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Salva Rweyemamu na mwanasiasa na mbunge wa zamani wa Temeke (CCM), John Kibaso.

Kwanza, watu wanazungumzia kutokufanikiwa kwa serikali ya Kikwete kwa kutumia hoja za jumla, ambazo nyingi zinapambwa na takwimu za uwongo.
 
Kwa mfano, mwandishi David Kafulila anadai, kwamba mwaka 2005, wakati Kikwete anaingia madarakani mfuko mmoja wa saruji ulikuwa ukiuzwa Sh. 11,000, sasa unauzwa Sh. 21,000.

Ukweli ni kwamba bei ya mfuko huo kwa sasa, ni kati ya Sh. 11,500 na Sh. 12,500.
 
Pili, inafahamika kuwa Kikwete ameingia madarakani na kukuta nchi ikikabiliwa na ukame. Taarifa ya serikali mwisho wa mwaka 2006, ilisema takribani ng’ombe 250,000, mbuzi 133,000, kondoo 122,000 na punda 744 wanaokadiriwa kuwa na thamani ya Sh. 45.3 bilioni, walikufa kutokana na ukosefu wa maji na malisho.
 
Ukame ulipopungua, bei ya mafuta ilipanda katika soko la dunia na kusababisha ongezeko la bei ya bidhaa na nauli kupanda kwenye sekta ya usafiri na uchukuzi.
 
Mwaka uliopita, ulitokea mtikisiko wa kiuchumi duniani, ambao umeathiri mataifa yaliyoendelea na yanayoendelea.
 
Uimara wa Kikwete umeiwezesha Tanzania kutokuyumba. Bei zimeshuka na nauli kupungua. Licha ya hilo, wamiliki wa makampuni binafsi ya kuagiza mafuta waling’ang’ania kupandisha bei, wakati bei ya mafuta imeshuka katika soko la dunia.
 
Leo nauli ya daladala imebaki kuwa Sh. 250. Nadhani akina Mohamed Yusuf wangetamani kuandika, kuwa “mafanikio ya Kikwete hayaonekani kwani nauli imepanda maradufu.”
 
Kubeza kauli ya Salva Rweyemamu, kuhusu mafaniko makubwa yaliyopatikana katika elimu, kwa madai kwamba shule za kata ni vijiwe vya kukulia na kuvutia bangi, ni kejeli kwa kila Mtanzania.
 
Ubora wa elimu unaopigiwa kelele hauwezi kupatikana kwa kufumba na kufumbua macho, suala analodai Mruta, kuwa shule nyingi ni mbovu.

Takwimu zinaonyesha idadi ya wanaonufaika na mpango huu wanaongezeka kila mwaka. Tayari serikali, kwa kuzingatia hili, inakamilisha awamu ya pili ya Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES), ambao utazingatia changamoto zote zilizotokana na MMES1, zikiwemo ukamilishaji wa madarasa, kujenga maabara na nyumba za walimu.
 
Wakati Lipumba na “watetezi wake” wakisema kile wanachoita kushindwa kwa Kikwete, vijana nchini wanaendelea kunufaika na mpango wa serikali kugharamia elimu ya juu kila mwaka.
 
Mwaka 2005/06 wanafunzi 42,729 walinufaika kwa kupata mkopo wenye thamani ya Sh. 56.2 bilioni. Hivi sasa wanafunzi 69,442 watakopeshwa zaidi ya Sh. 190 bilioni. Hili ni ongezeko la zaidi ya asilimia 50. Haya kama siyo mafanikio ni kitu gani hasa?
 
Kwa upande mwingine waandishi wanaomshambulia Salva, wakikejeli uteuzi wake, kiasi cha kufikia kutoamini kuwa Salva aliyeko Ikulu si yule waliyemfahamu awali.
 
Kuhusu madai ya kuwapo viongozi waliolipwa fadhila ya uongozi kuwa kikwazo cha utekelezaji wa ahadi za Kikwete, ni hoja nyingine dhaifu. Kikwete ana haki ya kuteua watu anaowaamini wanafaa.
 
Hata Rais  Barack Obama wa Marekani alipoingia madarakani aliteua wasaidizi wake mwenyewe, watu aliowaamini na kuwajua. Hata angekuwa Lipumba, ambaye hoja yake inatetewa, angefanya hivyo.
 
Kisiasa, serikali ya Kikwete imeonyesha ujasiri kwa kusimamia mazungumzo ya mwafaka kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na CUF, kabla ya CUF kususia.
 
Hatua hiyo inatupa picha ya “mpasuko wa kisiasa wa Zanzibar” kuwa CUF imeugeuza kuwa mtaji wake wa kisiasa. Hoja iliyokuwapo mezani ilikuwa ni kupata maoni ya Wazanzibari kuhusu umuhimu wa serikali ya mseto. Je, kilichofanya waogope kwenda kwa wananchi ni nini?
 
Inashangaza kuona kuwapo uhalifu na kile kinachoitwa ufisadi, kinakuwa kigezo cha Kikwete kushindwa kazi. Yote mawili ni matokeo ya kumomonyoka kwa maadili wakati sote tunawajibika kuhakikisha ufisadi unatokomea.

Kikwete ameonyesha njia. Watuhumiwa wa ufisadi wamefikishwa kortini. Ulinzi shirikishi, ulioanzishwa na jeshi la polisi, ni sehemu ya mafanikio ya Kikwete.

Uadui kati ya askari na raia unapungua. Utawala wa “mwenye nguvu mpishe” unapungua. Baadhi ya vigogo wamelazwa mahabusu. Ni Kikwete ambaye Lipumba na watetezi wa hoja yake, wanambeza. 
 
Utawala wa Kikwete umezuia uuzaji holela wa  nyumba za serikali.  Serikali imeinua hadhi ya nchi katika michezo. Kwa upande wa soka, nchi imepanda chati katika ramani ya Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA). Sasa taifa linajivunia timu ya taifa. Si kichwa cha mwendawazimu tena. 

Michezo iliyokufa katika shule za msingi na sekondari imerudi. Inatoa fursa kwa watoto wa kuendeleza vipaji.Kuna hoja ya upole wa Rais Kikwete. Unachukuliwa kama udhaifu. Hilo si kweli. Ni muungwana. Ni mtu wa watu. Anasikia kilio cha kila mtu, bila kujali dini, kabila, utajiri au nasaba. Ni rahisi kwa mtu yeyote kumfikia kuliko wakati wa marais Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa. Hapendi makuu wala kujikweza. Inawezekana hilo ndilo linalomponza.

Lakini ni Ris jasiri. Anaweza kusimamia maamuzi mazito ya nchi. Ni mtu asiyependa kukurupuka. Ni mwanasiasa shupavu na mwenye msimamo  usiyoyumba.

Mwandishi wa makala hii, Dunia Ibrahim, amejitambulisha kuwa msomaji wa siku nyingi wa MwanaHALISI, anayeishi mkoani Morogoro. Anapatikana kwa simu Na. 0652 855 666, e-mail: duniaibrahim@yahoo.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: