Kikwete njia panda


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 25 January 2011

Printer-friendly version
Ukimya wake sasa wamponza
Wabunge CCM wamkoromea
Rais Jakaya Kikwete

SUALA la kampuni ya kufua umeme ya Dowans limemweka Rais Jakaya Kikwete njiapanda, MwanaHALISI limeelezwa.

“Sasa anapewa masharti kutoka kila upande – huku vijana wa umoja wa chama chake, kule kamati ya wabunge wa CCM,” ameeleza mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho.

Njia pekee ya kujinasua na kujirejeshea hadhi, amesema kiongozi huyo, ni rais kuvunja ukimya juu ya makampuni ya kufua umeme ya Richmond na Dowans.

Wiki iliyopita umoja wa vijana (UV-CCM) ulitaka serikali isilipe Dowans; badala yake wakataka suala hilo lirejeshwe bungeni kujadiliwa upya.

Dowans wanadai Sh. 94 bilioni kutoka Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kwa kukatisha mkataba wake, kama inavyodaiwa kuamuliwa na mahakama ya kimataifa ya biashara (ICC). 

Juzi Jumatatu, kamati ya wabunge wa CCM iliyoketi mjini Dar es Salaam “iliitolea uvivu” serikali kwa kuelekeza kuwa Dowans wasilipwe na kwamba kinachoitwa mzigo wa fidia kwa kampuni hiyo wasibebeshwe wananchi wa Tanzania.

Tangu kuibuka kwa sakata la kukatisha “mkataba” wa Dowans hadi kampuni hiyo kushitaki Tanesco, Rais Kikwete amekuwa kimya.

Kwa upande mwingine maswahiba wawili wa rais, Edward Lowassa na Rostaam Aziz  wamekuwa katika hekaheka mbalimbali.

Rostam amekuwa akijitambulisha kuwa ndiye alipewa nguvu za kisheria kuwakilisha kampuni ya Dowans.

Wakati huohuo Lowassa amekuwa akifanya juhudi za “kujisafisha” na kashfa iliyomwondoa uwaziri mkuu – wapambe wake wakitaka suala la Richmond lirejeshwe bungeni.

Katika hali isiyo ya kawaida, Ijumaa iliyopita Katibu Mwenezi wa CCM, John Chiligati aliwaambia waandishi wa habari kuwa Kamati Kuu (CC) imekubali kuwa serikali iilipe Dowans.

Chiligati alisema chama chake kimesema kinasubiri kesi iliyofunguliwa na asasi za kijamii kupinga ulipaji imalizike; vinginevyo hakina pingamizi na ulipaji.

Hata hivyo, kauli ya Chiligati, ikija baada ya vijana kutaka Dowans wasilipwe, imestua hata wajumbe wa CC.

Taarifa kutoka serikalini na CCM zinasema, ndani ya kikao cha CC, hakukuwa na ajenda yeyote iliyojadili suala hilo, badala yake suala hilo lilitamkwa ndani ya kikao na Rais Kikwete.

“Hayo mambo ambayo Chiligati ameyatangaza si yetu. Ni yake. Kamati Kuu haikujadili suala la malipo ya Dowans,” ameeleza mjumbe mmoja wa CC kwa sharti la kutotajwa gazetini.

Alisema, “Kwanza, hatukujadili jambo hilo kwa kuwa suala lenyewe liko mikononi mwa serikali na hivyo sisi kama chama hatuwezi kuliingilia.”

Lakini mtoa taarifa anasema, “Yote haya ni ya kujitakia. Rais angekuwa ametoa tamko tangu awali kuhusu haya, tusingekuwa katika hali hii. Ukimya wake unamponza.”

Hivi sasa hatma ya Chiligati imo mikononi mwa Kikwete hasa baada ya wajumbe wa CC kukana kauli yake na wabunge wa CCM kuelekeza tofauti na aliyosema.

Kauli ya Chiligati kutaka Dowans ilipwe ilikuja siku moja baada ya UV-CCM kumtuhumu aliyekuwa spika wa Bunge, Samwel Sitta kuwa anatoa kauli zinazokizana na uwajibikaji wa pamoja.

Katika tamko lao mbele ya wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, viongozi wa umoja huo walitaka suala hilo lirejeshwe bungeni ili kujua “mbivu au mbichi.”

Taarifa kutoka ndani ya kamati ya wabunge wa CCM inasema naibu waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima aliwasilisha taarifa kuhusu Dowans na madai yake.

Ilikuwa wakati wa mjadala, taarifa zinasema, aliyekuwa mwenyekiti wa kamati teule ya bunge juu ya Richmond, Dk. Harisson Mwakyembe aliibuka na “kumwaga nyongo.”

Taarifa zinamnukuu Mwakyemba akisema, “…mnahangaika nini? Aliyetufikisha hapa ni mtu mmoja tu; anaitwa Rostam Aziz. Serikali ifanye kila linalowezekana kuhakikisha fedha hizi hazilipwi.”

Wakati Mwakyembe akisema hayo, taarifa zimeeleza, Rostam hakuwa ukumbini. Haikufahamika alikokwenda.

Mwenyekiti wa kikao hiki, ambamo mjumbe mmoja baada ya mwingine aliyeamka alitaka Dowans wasilipwe, alikuwa waziri mkuu Mizengo Pinda.

Mwakyembe alikiambia kikao cha wabunge kuwa kamati yake ililijiridhisha kuwa Dowans ni kampuni hewa; walichoambulia nchini Costa Rica ni kutajwa kwa jina la Bernal Zamora Arse, anayemiliki kampuni zaidi ya  100 zenye kuishia na SA.

Anasema Zamora haelezi mahali zilipo ofisi za kampuni yake, jengo gani, nyumba au gari anayomiliki, pikipiki au baiskeli.

Mara baada ya Mwakyembe kueleza kwa kirefu mkataba wa Richmond kuwa ni batili na kusema kuna njia nyingi za kuzuia malipo, ndipo Crtistopher ole Sendeka alipoinuka na kumzuia Mwakyembe kutaja njia za kuzuia malipo.

Sendeka alisema, “Wenyewe wako hapa hapa. Mnataka aeleze kila kitu, ili kesho wakakutane na kueleza watatumia njia hizi kuzuia malipo,” jambo ambalo lilifanya wabunge wengi kuangua kicheko.

Kauli ya Sendeka ilitokana na baadhi ya wabunge kumtaka Mwakyembe kueleza hatua za kupitia kuzuia malipo kufanyika.

Akichangia hoja hiyo, Sitta alitaka serikali isililpe na akasema kama serikali inataka kulipa sisi “tuatajiunga na wanaharakati waliomba mahamama kuu isiruhusu malipo kwa Dowans.

Kauli ya Sitta ilionekana kuibua hisia kwamba wanaharakati wakishinda, “serikali itaingia matatani.”

Hatimaye lilitoka azimio la kamati kuwa Watanzania wasibebeshwe mzigo wa Dowans.

Awali Sitta alipohojiwa na gazeti hili juu ya mashambulizi ya UV-CCM alisema, “Mimi nazuia wizi kufanyika. Kwamba kuna watu wanataka kufungua zizi na kuiba ng’ombe. Sasa mimi nimekwenda kwenye zizi na kufunga zizi hilo.”

Alisema, “Hawa wanataka niache zizi limefunguliwa na ng’ombe waibiwe, kisha ndio mimi nipige kelele?” anahoji.

Alisema,  “Waziri wa nishati anataka kulipa Dowans bila kufuata taratibu. Suala lenyewe halijafikishwa katika baraza la mawaziri, halafu mtu anazomoka na kusema, tutalipa eti kwa kuwa tumeshindwa kesi.”

Hata hivyo, taarifa kutoka ndani ya Bunge zinasema baadhi ya wajumbe wa Kamati Teule wamejipanga kueleza kile kinachodaiwa kuwa hakikuelezwa katika ripoti ya awali.

“Labda liishie kwenye kikao cha kamati ya chama. Lakini likifika ukumbini, hawa watu watatafuta mlango wa kutokea na wataukosa.

“Hapo ndipo tutakapoeleza kila kitu…,” ameeleza mjumbe mmoja wa kamati teule ambaye bado ni mbunge.

Tarehe 23 Juni 2006, serikali chini ya Rais Kikwete iliingia mkataba na kampuni ya Richmond ambayo baadaye ilithibitika kuwa haikuwa na sifa, uwezo kifedha wala hadhi ya kufanya kazi iliyoomba.

Nyaraka kadhaa ambazo MwanaHALISI inazo zinaonyesha kuwa walioingiza nchi katika sakata hili, ni pamoja na Lowassa, ambaye wakati huo alikuwa waziri mkuu.

Nyaraka zinathibitisha kwamba Lowassa siyo tu alishiriki, bali alikuwa anatoa maelekezo ya nini kifanyike kwa kila hatua.

Kwa mujibu wa nyaraka hizo, Dk. Ibrahim Msabaha ambaye alikuwa waziri wa nishati na madini wakati huo, alibakia kama karani tu wa kutekeleza maagizo ya Lowassa.

Akitii maagizo kutoka kwa Lowassa, Juni 21, 2006, Dk. Msabaha, alimwandikia barua Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Athur Mwakapugi akimwagiza atekeleze maagizo ya waziri mkuu yaliyotaka mkataba wa Richmond kusainiwa mara moja.

Barua ya Dk. Msabaha kwa Mwakapugi ilisema, “…iagize Tanesco iingie mkataba na kampuni ya Richmond kwa ajili ya umeme wa kukodisha haraka iwezekanavyo. Nakuletea nakala ya kibali kilichotolewa kutoka ofisi ya Mhe. Waziri mkuu kwa kumbukumbu za wizara.”

Mara baada ya Mwakapugi kupata maelekezo kutoka kwa Dk. Msabaha, naye alitoa maagizo siku hiyohiyo kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco, Balozi Fulgence Kazaura, akimwagiza kuhakikisha shirika linaingia mkataba na Richmond.

Maelezo hayo ambayo aliyaandika kwa mkono yalisomeka kwa kifupi “...andaa barua kwa Mwenyekiti wa Tanesco kumuagiza waingie mkataba na Richmond.”

Taarifa ambazo gazeti hili limepata wakati tunakwenda mitamboni zinasema, mmoja wa mawakili wa kujitegemea, Kennedy Fungamtama aliyenukuliwa na gazeti la Tanzania Daima akishauri serikali kuilipa Dowans, ni mmoja wa mawakili wa kampuni hiyo.

Fungamtama anatetea Dowans katika kesi ya madai Na. 131/2010 kati ya Dowans Tanzania Limited na Tanesco iliyopo katika mahakama ya rufaa.

0
Your rating: None Average: 4.2 (6 votes)
Soma zaidi kuhusu: