Kikwete njiapanda


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 20 January 2010

Printer-friendly version
CCM kumfia mikononi
Vigogo kibao kutimka
Rais Jakaya Kikwete

KUNDI la vigogo waandamizi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) limepanga kujiondoa ndani ya chama hicho iwapo masharti yake hayatakubaliwa, MwanaHALISI limeelezwa.

“Kama hatukusikilizwa, tutatoka. Tutaunda chama chetu au tutajiunga na moja ya vyama vilivyopo,” ameeleza mmoja wa viongozi wanaoshinikiza mabadiliko.

Mpasuko huo mpya na wa aina yake unalenga kushinikiza kuondolewa nafasi za uongozi, vigogo ambao wamewahi kutuhumiwa ufisadi ndani ya chama.

Kamati Kuu (CC) ya CCM inakutana mjini Dar es Salaam Jumamosi hii na Halmashauri Kuu (NEC) itakutana Jumatatu ijayo ambako hoja hizi zinatarajiwa kuwekwa wazi na “huenda kutolewa maamuzi.”

Mkakati wa kuhama CCM umepewa nguvu na taarifa za Kamati ya Ali Hassan Mwinyi zilizovuja hivi karibuni. Taarifa zinasema kamati imependekeza viongozi wanne waandamizi wavuliwe uongozi ili kurejeshea chama hadhi yake mbele ya umma.

Wanaotajwa kuondolewa uongozi ni mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, mfanyabiashara na mbunge wa Igunga, Rostam Aziz; mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge na mbunge wa Bukoba Vijijini, Nazir Karamagi.

Taarifa zinasema ripoti ya mwisho ya Kamati ya Mwinyi, iliyopelekwa kwa Rais Jakaya Kikwete, inawatuhumu Rostam, Lowassa na Karamagi kwa kujenga makundi ya kujisafisha ambayo yameonekana kudhoofisha chama na serikali.

Kwa upande wake, Chenge anatuhumiwa kwa “kuaibisha” chama kutokana na tuhuma nzito za ufisadi ambazo zinamkabili.

Wakati Lowasa, Rostam na Karamagi wanatumuhiwa ufisadi katika mkataba wa Richmond, Chenge anakabiliwa na tuhuma za ununuzi wa rada ya kijeshi.

“Hawa jamaa wamejenga mtandao wa kujisafisha. Ni mtandao huu ambao ni kiini cha matatizo yaliyopo ndani ya chama na serikali hivi sasa,” chanzo cha habari cha gazeti kimeeleza.

Kamati ya Mwinyi inasema kuondolewa nyadhifa za uongozi kwa vigogo hao wanne, kunaweza kurejesha utulivu na hadhi katika chama wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu, ameeleza mtoa taarifa.

MwanaHALISI limeelezwa kuwa wajumbe wa Kamati ya Mwinyi walikuwa makini kuhusu taarifa zinazotaja CCM kuhusishwa na fedha zilizoibwa Benki Kuu (BoT) kupitia kampuni ya Kagoda.

Katika mazingira ambapo chama kimeshindwa kujieleza kinagaubaga na kueleweka kuwa hakikutumia fedha za Kagoda – kampuni inayotajwa kumhusisha Rostam Aziz – Kamati imeona kuwa anayetuhumiwa aondolewe uongozi ili “kulinda chama.”

Taarifa zinasema wanaoshinikiza mapendekezo ya kamati yaheshimiwe vinginevyo watahama CCM, ni pamoja na wabunge ambao wamekuwa wakijitambulisha kwa kupinga ufisadi.

Hata hivyo, taarifa zimeeleza kuwa mpango wa kuanzisha chama kipya au kujiunga na kilichopo, utaweza kufanywa iwapo tu vikao vya juu vya CCM vilivyopangwa kuanza mwishoni mwa wiki hii, vitashindwa kuchukua hatua zilizopendekezwa dhidi ya watuhumiwa wa ufisadi nchini.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na CCM hivi karibuni, vikao vya Kamati ya Maadili, CC na NEC vitafanyika kati ya 23 na 26 Januari 2010.

Mjumbe wa mkakati wa “mafisadi wabaki” au “wapinga ufisadi watoke,” amesema tayari mkakati wa ama kuanzisha chama kipya au kujiunga na chama kimojawapo cha upinzani hapa nchini umeiva.

“Tunasubiri vikao ili kuamua nini cha kufanya. Kama CCM itaendelea kulea mafisadi, tutarudi kutoka Dodoma (bungeni) na chama kipya. Na iwapo tutashindwa kukisajili kutokana na muda kuwa mfupi, tutajiunga na moja ya vyama vya upinzani vilivyopo,” amesema mjumbe huyo wa NEC.

Septemba mwaka jana NEC iliunda Kamati ya watu watatu iliyoongozwa na rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi kuchunguza kile kilichoitwa “mpasuko” ndani ya Bunge na Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Wajumbe wengine wa Kamati hiyo, ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Pius Msekwa na Spika wa zamani wa Baraza la Kutunga Sheria la Afrika Mashariki, Abdulrahman Kinana.

Tayari Kamati ya Mwinyi imepeleka mapendekezo yake kwa mwenyekiti wa chama hicho, Rais Kikwete.

Gazeti hili linaweza kuthibitisha kwamba kamati ya Mwinyi imependekeza kuvuliwa nyadhifa kwa walau vigogo wanne wa chama hicho ili kurejesha umoja na mshikamano ndani ya chama, jambo ambalo kama litafanikiwa, basi mpango mzima wa kuanzisha au kuhama chama unaweza kuyeyuka.

Mtandao wa kuondoa mafisadi katika chama umeanza kujipanga kwa kutafuta wajumbe wa NEC wa kuwaunga mkono kutoka katika mikoa mbalimbali. Miongoni mwa wanaotafutwa kufikiwa ni makatibu wa CCM wa mikoa.

Hata hivyo, mpango wa kuvua nyadhifa za uongozi watuhumiwa wa ufisadi, unatarajiwa kupata upinzani mkali ndani ya NEC kutokana na kundi la watuhumiwa kuwa na nguvu kubwa ya ushawishi ndani ya kikao hicho na hivyo kuwapo uwezekano mkubwa wa mmeguko.

“Hofu yangu kubwa ni kwamba mara baada ya CC kujadili mapendekezo hayo, vigogo hao watapata taarifa na wataanza mipango ya kukabiliana na hoja hizo. Kwa hiyo vita hapa itakuwa kwenye NEC,” kilisema chanzo kimoja cha habari.

Wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanasema mpango wowote kati ya hiyo miwili – ule wa kufukuza mafisadi au ule wa kushughulikia watuhumiwa wa ufisadi, unaweza kukipasua chama.

Hii itategemea jinsi mwenyekiti Rais Kikwete atakavyocheza karata zake, amesema mjumbe wa NEC na kuongeza, “aamue kife au kipone.”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: