Kikwete, Rostam, Lowassa, Karamagi wadaiwa Dowans


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 02 February 2011

Printer-friendly version
Gumzo
Rais Jakaya Kikwete

HATIMAYE kampuni ya Dowans Holding SA imesajili mahakama kuu nchini tuzo yake ya Sh. 94 bilioni iliyodondoshewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC).

Tuzo hiyo ilitolewa 5 Novemba 2010 baada ya wanaojiita wamiliki wa Dowans “kushinda” shauri walilolifungua dhidi ya shirika la umeme la taifa (TANESCO).

Mkataba wa 23 Juni 2006 uliofikisha TANESCO ICC, unahusu uzalishaji umeme wa dharula. Ulihusisha TANESCO na kampuni ya Richmond Development Company (LLC). Dowans ilirithi mkataba huo isivyo halali.

Hadi sasa, hakuna mwenye uhakika wa kitakachoamuliwa na mahakama – kulipwa au kutolipwa.

Hata hivyo, wakati umma unasubiri uamuzi wa mahakama juu ya shauri hilo, ni muhimu jambo moja kufahamika mapema. Iwapo ombi la Dowans litakubaliwa, wanaopaswa kulipa fedha hizo si TANESCO.

Wanaotakiwa kulipa mabilioni haya ya shilingi ni wale walioshiriki kuingiza nchi katika mkenge. Hawa wanafahamika hata kwa majina, mahali wanapoishi, anuani zao za posta na namba zao za simu.

Kwanza, ni yule aliyeongoza kikao cha baraza la mawaziri, 20 Februari 2006 - siku nne baada ya kuanza mgao wa umeme, ambamo taarifa zinasema, serikali iliweka msimamo wa kununua mitambo yake yenyewe. Huyu anapaswa kulipa.

Ni rais Jakaya Kikwete. Huyu anapaswa kulipa zaidi ya kile kitakacholipwa na wenzake wengine, kwa kuwa alibariki au kunyamazia watendaji wa serikali, akiwamo aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa, waliobadilisha maamuzi ya baraza la mawaziri yaliyotaka TANESCO kununua mitambo yake.

Kinyume na maelekezo ya baraza la mawaziri, watendaji hao waliijulisha kampuni CDC Globeleq kuwa serikali imesitisha mpango wake wa kununua mitambo kutoka kampuni hiyo.

Hadi Bunge linamlazimisha Lowassa kujiuzulu, Kikwete hakusikika kukaripia Lowassa, wala katibu mkuu wa nishati na madini, Arthur Mwakapugi kwa hatua yao ya kuficha ukweli na kupindisha maamuzi ya serikali.

Hakumweleza Lowassa kuwa hatua yake ya kuzuia TANESCO kupata taarifa za Pratt & Whitney iliyodaiwa na Richmond kuwa mshirika wake, zilichangia kwa kiasi kikubwa nchi kuingia gizani.

Alishindwa kumuondoa aliyekuwa mwanasheria mkuu wa serikali, Johnson Mwanyika katika nafasi yake hadi mwisho.

Aliamua “kufunika” hadi mapendekezo ya Bunge yaliyotaka Mwanyika, Mwakapugi na mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini, Edward Hoseah kuachia ngazi.

Kama Rais Kikwete angefanyia kazi taarifa kuwa kampuni ambayo Lowassa alikuwa anahaha kutaka kuipa kazi imeshindwa hata kupeleka wataalamu wake nje ya nchi kuangalia mashine za umeme, angeweza kuzuia mkataba huu kufungwa.

Wala rais Kikwete hawezi kusema kuwa serikali yake haikuwa inafahamu juu ya jambo hili. Bali kwa kuwa rais aliogopa marafiki zake – Lowassa na Rostam – alishindwa kuzuia Richmond kupewa kazi.

Alishindwa kumfukuza kazi Dk. Ibrahim Msabaha kwa hatua yake ya kukubali kugeuzwa karani na Lowassa, badala ya kufanya kazi ya uwaziri aliyomkabidhi.

Mwingine anayepaswa kulipa ni kigogo wa serikali aliyelazimisha TANESCO kufunga mkataba na kampuni hewa; aliyeshinikiza zabuni kufunguliwa bila kushirikisha TANESCO na aliyeagiza kazi ya tathmini ya mradi kufanywa na bodi aliyoiunda, badala ya bodi ya zabuni ya TANESCO.

Ni yule aliyeshinikiza muda wa zabuni kuongezwa hadi 20 Machi 2006 ili kubeba kampuni yake; aliyelazimisha vigezo vya zabuni kupunguzwa kutoka 30 vya awali hadi tisa.

Aliyeamuru tathimini ya pili kufanyika; pamoja na Richmond kuonekana na mapungufu 13 kulinganisha na wazabuni wengine, aling’ang’aniza kupewa kazi.

Huyo ni Edward Lowassa, waziri mkuu aliyejiuzulu. Kama mahakama itaona Dowans inastahili kulipwa, basi iamrishe Lowassa alipe sehemu ya fedha hiyo.

Nyaraka zinathibitisha kwamba Lowassa siyo tu alishiriki kuhakikisha Richmond inapata mkataba, bali alikuwa anatoa maelekezo ya nini kifanyike kwa kila hatua.

Taarifa kutoka ndani ya TANESCO zinasema, menejementi ya shirika haikuwa na mpango wowote wa kukodisha mitambo ya kuzalisha umeme. Ililenga kununua mitambo yake yenyewe chini ya “mpango wa ununuzi wa moja kwa moja kutoka kwa watengenezaji.”

Barua ya TANESCO ya 20 Februari 2006 iliyotumwa kwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Arthur Mwakapugi, inathibitisha kwamba TANESCO haikutaka kuingia katika “mtego” wa makampuni ya kitapeli ya kufua umeme wa dharula.

Kikao cha baraza la mawaziri cha 10 Februari 2006, kinasisitiza hilo pia. Mkutano kati ya aliyekuwa waziri wa nishati na madini, Dk. Msabaha na watendaji wa wizara yake, 21 Februari 2006 unaeleza bayana “mpango wa serikali, si kukodisha mitambo, ni kununua.”

Aidha, uamuzi wa bodi ya TANESCO kutangaza mara moja zabuni ya ununuzi wa mitambo inayohitajika, ni uthibitisho mwingine kuwa “yote yaliyofanyika hayakuwa maamuzi ya TANESCO.” Yalikuwa maamuzi ya Lowassa na washirika wake.

Ni Lowassa aliyetajwa na Kamati Teule ya Bunge kushinikiza kubadilishwa kwa maamuzi ya baraza la mawaziri yaliyotaka TANESCO kuagiza mitambo yake.

Ni Lowassa aliyeagiza TANESCO kutangaza upya zabuni ya kutafuta kampuni ya kuzalisha umeme wa dharula. Alitenda yote haya bila kibali cha baraza la mawaziri na bila kufuata sheria za manunuzi ya umma (PPRA).

Wakati haya yanafanyika, tayari TANESCO ilishakubaliana na kampuni ya CDC Globeleq – kampuni tanzu ya Songas –kuingiza nchini mitambo inayotakiwa.

Hivyo basi, katika mazingira haya Lowassa hawezi kukwepa tuhuma kuwa maamuzi yake juu ya suala hili, yamechangia kwa kiasi kikubwa kuingiza nchi katika matatizo.

Pili, mwingine anayepaswa kulipa sehemu ya fedha inayodaiwa, ni Nazir Karamagi, waziri wa nishati na madini ambaye aliridhia mkataba kuhamishwa.

Karamagi alificha taarifa muhimu menejementi ya TANESCO kuhusu Richmond kuhamishia mkataba wake kwa Dowans.

Kifungu cha 15:12 cha mkataba kinasema kabla mkataba kuhamishwa, ni lazima “Richmond wapate ridhaa ya TANESCO, tena ya maandishi.” Karamagi alipuuza hilo.

Ilikuwa hivi: 28 Novemba 2006, Karamagi alimpigia simu Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO, Balozi Fulgence Kazaura kuuliza kama mkataba kati ya TANESCO na Richmond unaweza kuhamishwa.

Balozi Kazaura anathibitisha katika mahajiano yake na Kamati Teule ya Bunge, kwamba alimueleza Karamagi, “Hilo litawezekana pale tu pande mbili zitakaporidhia” – TANESCO na Richmond. 

Balozi Kazaura anasema, ni Karamagi aliyemtaarifu Richmond wanataka kuhamisha mkataba wake kwa “kutumia haki yake chini ya kifungu 15.12.”

Ni Karamagi aliyetaja kampuni ya Dowans Holding SA kuwa ndiyo inayohamishiwa mkataba.

Karamagi aliyekula kiapo cha kulinda rasilimali za taifa, alifanya yote haya wakati akijua kuwa Richmond tayari imehamishia mkataba wake kwa Dowans, tangu 25 Sptemba 2006.

Lakini hakueleza TANESCO jambo hili. Hakusema kuwa hatua ya Richmond ya kuhamisha mkataba bila kushirikisha TANESCO, tayari imevunja mkataba.

Badala yake, 21 Desemba 2006 aliilazimisha TANESCO ikubali takwa la Richmond la kuhamisha mkataba wake kwenda Dowans na kuilazimisha kuwa hayo yaliyotendeka siku hiyo, “ndiyo yahesabike kuwa makubaliano halali kati ya TANESCO na Richmond.”

Wala Karamagi hakujisumbua kufahamu sababu za TANESCO kuandikia barua kadhaa Richmond, ikiwamo ile ya 27 Oktoba 2006 kulalamikia kucheleweshwa kwa utekelezaji wa mkataba.

Hakujihangaisha kufahamu kwa nini TANESCO wameamua kuandikia benki ya Citibank wakiomba kusaidia uchunguzi wa kampuni inayohamishiwa mkataba.

Kwa makusudi kabisa, Karamagi aliamua kuacha kazi za serikali, badala yake akageuka kuwa wakala wa Richmond na dada yake Dowans.

Hakuna mahali popote katika kumbukumbu za Bunge panapoonyesha Karamagi kujutia haya.

Badala yake, kinachoonekana ndani ya ripoti ya Bunge, ni tuhuma zinazomhusu waziri wa serikali kusaliti serikali.

Hadi sasa, hakuna ajuaye iwapo Karamagi alilipwa kwa kufanya yote haya au alitenda kwa kujitolea su kwa ahadi ya malipo ya baadaye.

Bali kinachofahamika kwa wengi, ni kwamba Karamagi aliripoti yote aliyotenda kwa waziri wake mkuu, Lowassa. Hivyo, Karamagi ni mtu mwingine ambaye anastahili kulipa fedha hizo iwapo mahakama itaamua zilipwe.

Kama Karamagi angezingatia misingi ya kazi yake, haya yasingetokea; Dowans isingekuwapo; kesi isingefunguliwa na Lowassa asingelalamika kwa kupoteza uwaziri mkuu wake.

Ni kwa sababu, Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza Richmond isingeundwa; wala  taifa lisingeingia katika hamkani ya kudondoka kwa waziri mkuu na serikali kuvunjika.

Vilevile Karamagi angetimiza kazi yake kama alivyotakiwa, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kisingeunda kamati ya wazee  kutafuta suluhu na wala ushindi wa Kikwete katika uchaguzi uliopita, usingekuwa huu wa “tia maji, tia maji.”

Muhusika mwingine ambaye anastahili kulipa iwapo mahakama itaamua hivyo,ni Rostam Aziz.

Kwanza, Rostam ameficha taarifa juu ya mmiliki halisi wa Richmond na Dowans. Ni majuzi tu, alipoumbuka baada ya mwanasheria mkuu wa serikali, Jaji  Fredrick Werema kupasua jipu.

Jaji Werema amesema, “Rostam ndiye mwenye Power of Attorney” – mamlaka ya uwakilishi ya kampuni ya Dowans.

Hatua ya Rostam ya kuficha taarifa kwamba Richmond haikuwa na uwezo kifedha na kitaaluma, zimechangia kwa kiasi kikubwa Bunge kuunda Kamati Teule kuchunguza Richmond; Lowassa kupoteza uwaziri mkuu; serikali kuvunja mkataba na hatimaye kesi kufunguliwa.

Hatua ya Rostam imechangia pia kushamiri kwa misuguano ndani ya chama chake; minyukano ndani ya jamii na kupungua kwa kura za Kikwete.

Kabla ya Werema kumtaja Rostam, wimbo wa mwanasiasa huyo ulikuwa “siijui Richmond na siifahamu Dowans.”

Hata pale ilipoelezwa kuwa anwani ya posta ya kampuni yake ya Caspian, barua pepe na baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo, ndiyo wanatumika Richmond na Dowans, bado Rostam aliendelea kusisitiza kutozifahamu kampuni hizo.

Akiwa mbunge wa Bunge la Jamhuri ambapo ameapa kulinda katiba na kutetea sheria zake, Rostam alipaswa kueleza TANESCO kuwa Richmond ni kampuni hewa.

Alipaswa kumueleza swahiba wake, Rais Kikwete kuwa kampuni hii itapunguza kura zako, itavuruga chama chako na itaharibu taswira ya taifa.

Alipaswa kueleza kuwa Richmond tayari imehamishia mkataba wake kwa Dowans, bila kushirikisha TANESCO.

Haya angeyasema, Dowans wasingepeleka kesi mahakamani, migomo iliyoshamiri katika kila pembe ya vyuo vikuu nchini, isingekuwapo kwa kuwa serikali isingekuwa bize kushughulika na Dowans.

Naye Dk. Ibrahim Msabaha ambaye wakati Richmond inafunga mkataba na TANESCO alikuwa waziri wa nishati na madini, anastahili kulipa sehemu ya fedha hizo.

Kosa kuu la Dk. Msabaha ni kule kukubali kugeuzwa karani na Lowassa. Nyaraka zinaonyesha, Dk. Msabaha alitii kila agizo alilopewa na Lowassa.

Kwa mfano, akitii maagizo kutoka kwa Lowassa, 21Juni 2006, Dk. Msabaha, alimwandikia barua Mwakapugi akimwagiza atekeleze maagizo ya waziri mkuu yaliyotaka mkataba wa Richmond kusainiwa mara moja.

Dk. Msabaha asingekubali kugeuzwa karani, taifa lisingefikishwa hapa; Richmond isingekuwapo, kesi isingefunguliwa, wala fedha zinazodaiwa zisingekuwa mjadala.

0
Your rating: None Average: 2 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: