Kikwete sasa unapotea njia


Hilal K. Sued's picture

Na Hilal K. Sued - Imechapwa 22 September 2010

Printer-friendly version

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), sasa kimeingia katika hatua mpya ya uwepo wake. Hatua hii si nyingine, bali imezidi kujitambulisha katika alama yake maarufu ya biashara (famous trademark) – ufisadi katika ngazi za juu.

Hatua hii ni ya kutisha zaidi na inaashiria jinsi gani nchi inavyozidi kupoteza mwelekeo kutokana na watawala kushindwa kutazama zaidi ya urefu wa pua zao.

Baada ya kigugumizi kingi, usanii na geresha kutoka kwa viongozi wa serikali na chama katika kushughulikia watuhumiwa wa ufisadi, sasa wameamua moja kwa moja, na kwa njia za bayana, tena hadharani kuutetea ufisadi na mafisadi.

Wiki iliyopita, mgombea urais wa chama hicho, Jakaya Kikwete amekuwa kiongozi wa kwanza kufanya hivyo katika kampeni za uchaguzi zinazoendelea.

Akiwa katika jimbo la uchaguzi la Rombo alimnadi na kumminia sifa kedekede, Basil Mramba aliyepitishwa na chama chake kuwania ubunge katika jimbo la Rombo.

Mramba ni mmoja wa watuhumiwa wakuu wa ufisadi nchini ambaye tayari amefikishwa mahakamani.

Anatuhumiwa kusababisha hasara ya mabilioni ya shilingi za umma kutokana na maamuzi ya hovyo ambayo kwa tafsiri yoyote ile ni maamuzi yalioashiria ufisadi mkubwa.

Kikwete alimsimamisha Mramba kwenye jukwaa na kumnadi mbele ya halaiki ya watu huku akiwaambia kuwa huyu ndiye anayewafaa kuwawakilisha na kwamba kesi inayomkabili siyo kesi kubwa.

Aidha, katika ziara hiyo hiyo ya kampeni, Kikwete alikwenda jimbo la Monduli ambako nako alimnadi Edward Lowassa, anayewania ubunge katika jimbo hilo.

Ni Lowassa aliyeandika historia ya uongozi nchini kwa kuwa waziri mkuu wa kwanza kujiuzulu kwa muda mfupi kutokana na tuhuma ya mkataba tata wa Richmond.

Lakini Kikwete akizungumza katika mkutano wa hadhara jimboni Monduli, alisema tuhuma dhidi ya Lowassa zilikuwa za kusingiziwa.

Kama Kikwete angekuwa makini asikwenda Monduli kumnadi Lowassa. Asingefika Rombo na wala asingekanyaga Igunga ambako mmoja wa watuhumiwa wakuu wa ufisadi anagombea ubunge.

Wala asingekanyaga Bariadi kumnadi Andrew Chenge, mwanasheria mkuu wa zamani wa serikali aliyekabiliwa na tuhuma za rushwa katika ununuzi wa rada.

Kiongozi makini angebaki mbali na watuhumiwa hawa. Kwanza, angehakikisha kwamba wahusika hawapitishwi na chama chake.

Pili, angegoma kufika katika majimbo yao kuwaombea kura na kujiombea yeye pia. Lakini Kikwete sivyo alivyo. Amekwenda Rombo, Monduli na atakwenda Igunga na Bariadi.

Kote huko atawasafisha kila mtuhumiwa kwa kusema “tuhuma dhidi yao ni za kupika.”

Hatua ya kupitisha Chenge, Lowassa, Rostam na Mramba na Kikwete binafsi kuamua kuwapigia kampeni kwa nguvu na kwa ujasiri mkubwa tena hadharani, kunatoa picha moja tu:

Kwamba, Kikwete na chama chake wanadharau wananchi wanaokerwa na vitendo vya ufisadi, achilia mbali juhudi za wanaharakati wa ndani na nje ya nchi wanaopambana na ufisadi. Ni sawa na kuwambia “tafuteni shughuli nyingine, hii sitaki muifanye.”

Je, kulikuwa na ulazima gani Kikwete kwenda katika majimbo ya wagombea hao na kuwanadi? Vipi anaweza kujiondoa katika uchafu huu?

Wapo watakaosema kwamba Kikwete anagombea urais na hivyo alistahili kwenda katika majimbo hayo ili kuomba kura. Ni kweli. Lakini hapa ndipo ambapo umakini wa kingozi na chama chake ulipopaswa kuangaliwa.

Kikwete anafahamu fika, kwamba kutokana na uwezo wao wa kisiasa na kiuchumi, Mramba na Lowassa hawana tatizo la kushinda uchaguzi katika majimbo yao. Hivyo basi, hakukuwa na ulazima wa yeye kwenda kuwapigia kampeni.

Angeweza kutunza zaidi hadhi yake mbele ya wananchi kwa kuyakwepa majimbo hayo.

Wapo wanaosema ipo sababu nyingine kubwa iliyompeleka Kikwete kuwafanyia kampeni. Ni kujaribu kuwasafisha kutokana na tuhuma zinazowakabili.

Kwa kuzingatia hilo, Kikwete alipaswa kuwa mwangalifu na kile anachokisema katika majukwaa ya kampeni, hasa kuhusu masuala ya mahakama na sheria.

Hii inatokana na ukweli kwamba mashitaka yote ya jinai hupelekwa mahakamani na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu (DPP) ikisaidiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru).

Kwa maana hiyo, ni sahihi kusema kwamba Kikwete ndiye aliyemshitaki Mramba mahakamani kwa tuhuma za ufisadi, na leo hii anautangazia umma kwamba ni mtu safi. Si bora angeacha kumpeleka mahakamani tangu mwanzo?

Hatua hii inaipa nguvu ile hoja inayotolewa mara kwa mara kwamba serikali yake inafanya geresha tu mbele ya wananchi kuwapeleka watuhumiwa wa ufisadi mahakamani – kwani wanaonekana ni maswahiba wake.

Aidha, si mara ya kwanza rais Kikwete kuonekana akiwatetea watuhumiwa wa ufisadi hadharani. Juni mwaka 2007, rais Kikwete aliweka rekodi ya kuwa rais wa kwanza katika barani Afrika, kama siyo dunia kutangazia ulimwengu kuwa si vyema kwa marais walio madarakani kuwaandama wale waliowatangulia.

Alisema kwa kufanya hivyo, kunaweza kuwatia hofu watawala na hivyo kuamua kung’ang’ania madarakani.

Alitoa kauli hiyo kujibu swali aliloulizwa na waandishi wa habari juu ya tuhuma za ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka zilizokuwa zikimkabili mtangulizi wake, Benjamin Mkapa.

Vilevile, Agosti mwaka juzi mara baada ya kufumuka kwa wizi wa mabilioni ya shilingi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Taifa (BoT), Kikwete alisimama bungeni na kupora madaraka ya mwendesha mashitaka, hakimu na Bunge.

Alimtaka ndani ya Bunge kusamehe watuhumiwa wote wa wizi. Aliwapa hadi 31Oktoba 2008 kurejesha fedha hizo. Hadi sasa, hakuna mwenye uhakika wa kiasi gani cha fedha kimerejeshwa. Nani aliyerejesha? Ziko wapi fedha zilizorejeshwa?

Alichukua fursa hiyo kuzipangia bajeti fedha zitakazorudishwa. Aliagiza fedha zitakazorejeshwa zitumike kununulia mbolea na kuigawa kwa wakulima.

Lakini nani anafahamu kiasi cha ambacho kilichonunuliwa kwa fedha zilizorejeshwa. Bila shaka, hakuna.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: