Kikwete na sauti ya Kolimba kutoka nyikani


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 26 March 2008

Printer-friendly version

MWISHONI mwa wiki hii Watanzania wanatarajia kusikia maamuzi makubwa yatakayofanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho kukaa Butiama. Kikao hiki cha NEC kinatarajiwa kuweka historia katika taifa hili kutokana na mambo mawili makubwa; moja CCM inatarajiwa kusema lolote kuhusiana na mazungumzo ya mwafaka kati yake na Chama cha Wananchi (CUF) katika juhudi za kupata suluhu ya mpasuko wa kisiasa visiwani Zanzibar.

La pili, ni habari za kujadiliwa kwa kusudio la Mwenyekiti wa chama hicho ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, la kutaka kutenganisha siasa na biashara. Akiwa Zanzibar Februari mwaka huu wakati wa maadhimisho ya miaka 31 ya kuzaliwa kwa CCM Rais Kikwete alisema anataka kuanzisha mchakato wa kutenganisha biashara na siasa kwa sababu ya kuwako kwa mgongano wa kimaslahi.

Wakati suala la mwafaka limekwisha kuonyesha mwelekeo wa maamuzi kutokana na CUF kusema wazi kwamba wamekubaliana na CCM katika mazungumzo yao juu ya kuanzishwa kwa serikali ya mseto huko Zanzibar, kutenganisha siasa na biashara ni kazi ngumu kuliko zote ambazo Rais Kikwete amejitosa tangu aingie madarakani.

Ugumu wa kutenganisha siasa na biashara unajielekeza katika mambo mengi ya kimsingi. Kubwa kuliko yote ni mgongano na mkanganyiko wa kiitikadi ndani ya CCM. Tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini baada ya taifa hili kuachana na ujamaa na kuanza kukumbatia mfumo wa uchumi huria, CCM si tu imejikuta haina itikadi mahususi bali pia imekataa kukubali kwamba imechanganyikiwa kiitikadi.

Itakumbukwa kwamba aliyewahi kuwa katibu mkuu wa CCM na waziri katika serikali ya awamu ya pili ya Ali Hassan Mwinyi, Marehemu Horace Kolimba, alipata kukosoa chama chake kwa kauli kali kwamba kimekosa dira. Kauli ya Kolimba ilisababisha mtafaruku mkali kiasi cha kufanya NEC imuite kujieleza na baada ya kujieleza Kolimba alifikwa na mauti. Pamoja na kifo cha Kolimba, kilichoabaki ni ukweli ambao leo hii tunaushuhudia.

Kwamba tangu kuvurugwa kwa azimio la Arusha mwaka 1992 kule Zanzibar na kuacha siasa za taifa hili zikiendeshwa bila maadili na kanuni katika mambo mengi, hasa suala la fedha katika uchaguzi na kuendesha vyama vya siasa, CCM imejikuta ikukumbatia kila aina ya wanachama na hata kuwashawishi wengine kugombea nafasi mbalimbali za kisiasa kwa sababu tu ya nguvu ya fedha.

Ni katika kipindi cha miaka kati ya 90 na sasa CCM imejitokeza waziwazi kuwa chama cha wafanyabiashara wakubwa wakishawishiwa na viongozi wakuu wa chama na pengine hata wa kiserikali.

Ni katika mtiririko huo CCM imejikuta ikiwakumbatia wafanyabiashara wakubwa na hata pengine kuwatafuta kwa udi na uvumba ili ama wawanie nafasi za kisiasa ndani ya chama hicho au wawe wafadhili wa chama hicho. Ni katika hali ya kujiachia na kuachana na misingi ya kiitikadi na miiko ndiko kunakomsumbua Rais Kikwete leo kutafuta njia ya kutenganisha siasa na biashara.

Kwa hiyo anachotaka kufanya Rais Kikwete ni kujaribu kurejesha maadili na miiko ndani ya CCM kwa kutumia lugha ya kutenganisha siasa na biashara. Swali kubwa linasumbua vichwa vya watu; kwamba ni kwa nini utaratibu huo ubuniwe sasa na si kabla ya hapo? Ni kwa nini sasa wakati kilio cha ufisadi kimetanda kila kona serikalini na kwenye taasisi zinazojitegemea?

Kimtazamo inaweza kufikiriwa kwamba kuvunjika kwa kanuni na miiko ndani ya chama hiki kikongwe kumechangiwa zaidi na kuvamiwa na wafanyabiashara na hivyo dawa ya kurejeshwa kwa maadili au miiko hiyo ni kutenganisha siasa na biashara. Mtazamo huu hata kama utakuwa unachukuwa uzito gani wa hali halisi ni potofu kwa kiwango kikubwa.

Ni potofu kwa sababu za kihistoria. Zipo kumbukumbu zinazoshuhudia wafanyabiashara kama Rupia, Sykes na wengineo ambao juhudi zao binafsi za kusadia TANU ndizo ziliongeza vuguvugu na hatimaye mapambano ya kudai uhuru. Kwa maana hiyo wafanyabiashara hawa walikuwa ni baraka kwa TANU. Suala linalohitaji mjadala wa kina hapa ni kwa nini wafanyabiashara wa leo wanaonekana kikwazo katika siasa? Je, tatizo ni wafanyabiashara tu au ni njama za watumishi wa umma na hata baadhi ya viongozi wa kisiasa kula njama na wafanyabiashara katika kuhujumu nchi na hivyo kukipaka chama tawala matope?

Tathmini yoyote ikifanywa sasa hivi juu ya mikataba mibovu ambayo taifa imetumbukizwa kama hii ya Richmond; IPTL; Songas; NBC; TTCL; ATC; mikataba ya uchimbaji madini kutaja kwa uchache tu, iliandaliwa na watumishi wa umma. Hawakuweka mbele maslahi ya taifa. Hawa ndio wamefanya maisha ya Watanzania kuwa magumu zaidi kuliko inavyoweza kuelezwa. Wachoraji wa mipango ya EPA wote ni watumishi wa umma. Wamekubali kula njama na wafanyabiashara.

Kwa hiyo tunapotafakari kilicho moyoni mwa Rais Kikwete ni hisia za wazi kwamba wafanyabiasha wameharibu siasa za nchi hii na hasa hasa siasa za CCM. Chaguzi zimekuwa ni za kuhonga fedha, sheria ya takrima ni matokeo ya matumizi ya fedha zisizo na ukomo katika uchaguzi. Sasa dawa inadhaniwa kuwamba ni kuwabana wafanyabiashara.

Ebu tujaribu kutafakari kwa upana zaidi, CCM ina wafanyabiashara ambao ni wenyeviti wa chama katika mikoa na hata wilaya; ina wafanyabiashara ndani ya NEC na hata kwenye kamati kuu. Hawa ni watu wenye ushawishi mkubwa katika taifa hili kwenye kutunga sera na hata kuzitekeleza. Je, hawa katika mchakato wa kutenganisha siasa na biashara wanalengwa kuondolewa? Na wale waliko kwenye baraza la mawazi? Hawa Rais Kikwete analenga kuwafanya nini?

Kwa upeo wangu, nidhani hata baada ya CCM kufanikiwa kumtisha Kolimba na hata baada ya safari ya Kolimba hapa duniani kufikia mwisho, walipaswa kujiuliza mara mbili kama kweli aliyokuwa amezungumzia kuhusu chama kokosa dira ilikuwa ni kweli au fitina ya kisiasa.

Kama kweli kwa miaka yote hiyo CCM ingekuwa imejipa fursa ya kukaa na kutafakari kwa kina maneno ya Kolimba, leo hii haya anayosema Kikwete yasingekuwako.

Ndiyo maana tangu awali nilisema kwamba ingawa anachokusudia kufanya Rais Kikwete sasa ni kutaka kurejesha maadili na miiko ndani ya CCM, anasahau kwamba CCM ni chama tawala kinachozaa serikali anayoongoza; ndani ya serikali yake wamejaa watumishi wasiojua wala kufuata maadili yoyote ya kiutumishi; wapo ambao inadaiwa kwa tabia ni kama wanalipwa ujira na baadhi ya wafanyabiashara; wapo ambao hawana tena soni kwani kila aina ya uchafu wana ujasiri wa kuufanya.

Katika hali kama hii kuzungumzia wafanyabiashara na siasa bila kwanza kuwawajibisha mafisadi wakubwa waliomo kwenye utumishi wa umma, ni kutibu jipu kwa kupaka dawa bila kulikamua kwanza.

Wafanyabiashara wamefika hapo walipo kwa sababu ya kusaidiwa na watumishi wa umma; kwa nini Kikwete hataki kuelewa jambo jepesi kwamba watumishi wa umma wanaishi maisha yasiyofanana na vipato vyao halali; na hata wakitakiwa kueleza waliokopata ukwasi walionao asilani hawatakaa waweze kwa sababu ni kwa njia chafu. Je, hawa wamo kwenye vyama vya siasa?

Kwa maana hii ninafikiri pamoja na ukweli kwamba Rais Kikwete anataka kujenga maadili ya kisiasa nchini; jambo ambalo ni jema na la heri, anasahau kwamba waliolifikisha taifa hili hapa lilipo leo ni watumishi wa umma. Bila kwanza kusafisha ndani ya serikali kamwe kulia na wanasiasa pekee hakutapunguza ufisadi nchini.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: