Kikwete tuondoe katika 'Jamhuri ya mashangingi'


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 17 June 2008

Printer-friendly version

WABUNGE wapo Dodoma wakijadili bajeti kuu ya serikali ya mwaka wa fedha wa 2008/09. Tayari wengi wamekwishaweka bayana hisia zao kuhusu bajeti hii, wakionyesha kutoridhishwa na mikakati iliyomo.

Kadhalika, wapo wanaounga mkono kwa asilimia miamoja; hawaoni upungufu wowote kwenye bajeti hii ambako serikali inatarajia kutumia Sh. 7.2 trilioni. Kwa hao, kila kitu ni dhahabu; bajeti nzuri na mipango mizuri.

Niseme tu kila mtu ana haki ya maoni yake kuhusu jambo lolote linalogusa maisha yake; kwa maana hiyo, si jambo la kustaajabisha kuona kwamba wapo watu wanaoiona bajeti ya mwaka wa fedha ujao, pamoja na mapungufu yake yote, kuwa ni mipango iliyoratibiwa vizuri kwa asilimia miamoja.

Pamoja na ukweli huu, kila wakati serikali inapowasilisha bajeti yake nimekuwa najiuliza swali, "Je, itatokea siku serikali itambue kwamba mtindo wa maisha ya watumishi wake ndiyo chimbuko la maangamizi ya taifa hili?

Najiuliza swali hili hasa ninapotazama matumizi ya magari ya serikali. Huwa najisemea, "Tanzania ni Jamhuri ya mashangingi."

Hakuna ubishi kwamba kuna ugonjwa wa matumizi ya magari ya kifahari kwa kila mtumishi wa serikali mwenye hadhi ya kupewa usafiri. Hakuna ubishi kuwa sasa ni rasmi kwamba magari ya serikali ni "mashangingi."

Magari haya ni msururu wa Toyota Land Cruiser kuanzia VX, GX, Prado, bila kusahau Nissan Patrol na Range Rover. Haya ni magari ya kifahari kwa maana halisi ya neno fahari; iwe kwa mataifa masikini kama Tanzania au hata yale yaliyoendelea kama yale yanayotusaidia katika bajeti kila mwaka.

Hakuna kiongozi wa serikali ya Tanzania hata mmoja anayekerwa na matumizi ya magari haya. Kila mmoja kuanzia ofisa mwandamizi wa wilaya, mkoani hadi wizarani wanatamani na kutumia magari haya. Yule asiyekuwa nalo anafanya juhudi kubwa kulipata. Kwa hali hii tumejikuta tumekwisha kutengeneza "amhuri ya mashangingi."

Inawezekana kwamba wanaotumia magari haya wanaona fahari kubwa. Lakini wasichokumbuka ni kwamba gharama ya kuliweka shangingi moja barabarani ni fedha ya kutosha kujenga madarasa kadhaa na kuweka samani za kutosha. Hakuna gari linalonunuliwa chini ya Sh. 100 milioni.

Jaribu kufikiria, mkurugenzi mmoja wa serikali kwa wiki anatumia si chini ya lita 200 za mafuta, iwe ni dizeli au petroli. Hii maana yake ni kwamba kwa gharama ya mafuta tu, ofisa huyu anachota kodi za wananchi kiasi cha Sh 400,000 kwa wiki. Gharama hizi hazijumuishi matengenezo ya kawaida ya gari.

Pengine ni katika kutafakari hali kama hii, Rais Paul Kagame wa Rwanda alitambua kwamba kodi za wananchi zilikuwa zikiishia kugharimia uendeshaji wa magari ya serikali ya namna hiyo, hivyo akafikia hatua ya kusema, "mashangingi serikalini sasa basi!"

Rwanda ilifikia hatua hiyo na kuyauza kwa mnada magari yote ya aina hiyo yaliyokuwa yanamilikiwa na serikali kwa sababu ilitambua kwamba yalikuwa ni mzigo usiobebeka kwa walipakodi wa nchi hiyo.

Iliwekwa bayana kwamba kama yupo mtumishi wa umma mwenye kutaka kutembelea shangingi, basi alikuwa huru kununua kwa fedha zake, lakini serikali kwa vyovyote isingegharimia magari hayo ya anasa.

Ni katika kutafakari uamuzi huu wa kijasiri wa Rwanda, najiuliza, yuko wapi kiongozi wa aina ya Kagame kusaidia kuiondoa Tanzania kwenye safu ya Jamhuri za mashangingi? Yuko wapi mbunge mwenye ujasiri wa kuandaa hoja binafsi ya kuishurutisha serikali kuachana na anasa za mashangingi?

Najiuliza, yuko wapi waziri mwenye uchungu na nchi hii, anayejua shida za wananchi na apendekeze kuachana na mashangingi? Wako wapi viongozi wanaofanana na Kagame katika hili? Wapo? Kama wapo wasimame tuwahesabu!

Ni fedheha kwamba pamoja na umasikini uliogubika taifa hili watu waliokalia ofisi za umma wanaishi maisha ya anasa kubwa. Wanaishi maisha ya kufuru tupu. Niliwahi kuandika katika safu hii, kwamba kinachosumbua taifa hili si kukosekana kwa rasilimali vitu, bali rasilimali watu, hasa watu-viongozi.

Viongozi wamehujumu taifa,; wamelikaba koo taifa kiasi kwamba hakuna tena mjadala wa kutafakari njia ipi inafaa kwa maendeleo. Wanaliua taifa. Hakuna anayesumbua kichwa chake kwa ajili ya maendeleo ya kweli ya taifa hili. Watu wamejenga ubinafsi kwa kiwango cha kutisha.

Tangu mwaka 1990, serikali ilipopotea njia na kuamua kuwakopesha wabunge wote magari ya kifahari –mashangingi – bila kujijua ilijenga na kuimarisha utamaduni wa kushabikia maisha ya anasa. Kwa bahati mbaya sana anasa hizi ni kwa gharama ya walipa kodi. Ni anasa hii inayotafuna taifa hili.

Ndiyo maana wakati wabunge wakiijadili bajeti ya 2008/09 wanapaswa kujiuliza maswali magumu, kati yake ni hili la uhalali wa serikali kuendelea kumiliki mashangingi yote haya.

Madhara ya mashangingi ni mkubwa kuliko inavyoweza kuelezwa. Matumizi makubwa ya fedha za walipa kodi, maisha ya anasa na kusahau shida za wananchi, ni matokeo ya serikali kushindwa kutambua kwamba ipo madarakani kwa ajili ya wananchi.

Uwezo wa serikali wa kutambua matatizo ya wananchi wake, jinsi inavyotekeleza majumu yake – yakishabihiana na uwezo wa taifa; ni mambo ya kimsingi yanayoipa uhalali wa kuendelea kutawala.

Serikali sugu, isiyojali wala kushtushwa na matumizi yaliyopindukia ya watumishi wake, haiwezi kudai kuwa na uhalali wa kutawala kwa sababu tu iliingia madarakani kwa njia ya kura. Hapana!

Serikali hiyo inakosa uhalali kwa sababu haitazami shida za wananchi. Hii ni serikali iliyosaliti ridhaa iliyopewa kwa njia ya kura.

Hali hii ya kutojali ndiyo inafanya Tanzania kupitwa kimaendeleo hata na nchi ilizozisaidia kujikomboa na zile inazoendeleza kusaidia ushauri kuhusu jinsi kujitawala.

Hakuna ubishi kwamba Uganda ilikombolewa na Tanzania kama ilivyo kwa Rwanda na Burundi, lakini hatua wanazopiga zinaonyesha kwamba watawala wao wako makini zaidi kuliko wa Tanzania.

Wabunge wanaweza kuibadili serikali ya Tanzania kama wenyewe wataamua kuachana na anasa za mashangingi na kuishurutisha kuyauza kwa mnada ili ulevi huu ambao umekuwa utamaduni usitajwe katika safu za watawala waadilifu.

Ndiyo maana nathubutu kumwambia Rais Jakaya Kikwete asione aibu kujifunza kwa Kagame juu ya madhara ya mashangingi kwa uchumi wa taifa masikini kama Tanzania.

0
No votes yet