Kikwete na umeme


editor's picture

Na editor - Imechapwa 27 July 2011

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

RAIS Jakaya Kikwete anasema chimbuko kuu la uhaba wa umeme nchini ni ukame. Mabwawa ya maji yanayotumika kuzalisha umeme yanakauka kutokana na ukosefu wa mvua hivyo kupunguza kiwango cha uzalishaji umeme kwa njia hiyo.

Sawa, lakini kwanini huwa tunamwaga maji pale msimu wa mvua unapoongoka na maji mengi kuingia kwenye mabwawa?

Rais hakuulizwa swali hili na mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) aliyeko Afrika Kusini. Lakini alikuwa na wajibu wa kuligusia. Kwanini serikali haivuni maji ili kuyahifadhi na kuyatumia yanapopungua?

Hatuwezi kuteta na muumba anayetujaalia au kutunyima mvua. Sasa anapotujaalia mvua nyingi, lazima tukumbuke inawezekana sana tukazikosa msimu ujao.

Huo ni upungufu mkubwa kwa wataalamu wa mazingira, maji na nishati. Inaonyesha hawapangi na kutekeleza mipango yao kwa ushirikiano.

Njia nyingine kubwa inayotumika kuzalisha umeme nchini, ukiacha ile ya mafuta mazito (IDO), ni ya mitambo ambayo huendeshwa kwa kutumia gesi.

Rais katika mahojiano na BBC, hakugusia kamwe kwamba serikali inalea mkataba wa kifisadi ilioingia pamoja na wanaoitwa wawekezaji katika gesi asilia.

Hakueleza mkataba huo umetandwa na wingu la ufisadi na ndio chanzo cha kuzorota kwa uzalishaji na usafirishaji wa gesi hadi kuifikisha jijini Dar es Salaam.

Tunasema serikali inunue mitambo hata 100 leo, itakuwa ni bure. Hakuna gesi ya kuiendesha. Hakuna kwa sababu miundombinu iliyopo Songosongo mkoani Lindi, ni mibovu na ukarabati wake unahitaji mabilioni ya shilingi za umma.

Mtambo wa Symbion Power ni mfano hai. Una uwezo wa kufua megawati 112 za umeme. Lakini, tangu ulipoanza kuwashwa Mei mwaka huu, unatoa umeme chini ya megawati 60.

Ufinyu huo wa kuzalisha na kusafirisha gesi unaendelea japokuwa serikali hulipa kila mwezi kiasi cha Sh. 60 bilioni kwa Songas na washirika wake Pan African Energy Tanzania Limited wenye mkataba.

Rais atambue kuwa ukosefu wa umeme ni kubwa kuliko serikali anayoongoza wanavyofikiri. Na ukame haiwezekani ikawa ndio kisingizio.

Umeme ndio injini ya ukuaji wa uchumi popote pale katika zama hizi. Hakuna maendeleo bila umeme kwa sababu hakuna harakati za kiuchumi.

Tayari, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wamesema watakosa Sh. 840 milioni kila mwezi tatizo la umeme likiendelea. Jumuiya ya Waajiri Tanzania (ATE) wao watapoteza asilimia 30 ya ajira walizonazo.

Serikali ijue inacheza na nyoka, ambaye desturi yake ni kudhuru tu. Ukosefu wa umeme unadhuru na itadhuru uchumi; serikali itashindwa kuhudumia watu; familia hazitazalisha. Hatima? Ni anguko la kihistoria.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)