Kikwete unda upya Baraza la Mawaziri


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 22 April 2008

Printer-friendly version

KATIKA hili, Andrew Chenge, aliyejiuzulu uwaziri juzi, alisema kweli. Miezi miwili iliyopita aliwaeleza waliokuwa wanakerwa na kuteuliwa kwake tena kuwa waziri wamuulize huyo aliyemteua.

Ni kauli ya kweli na jeuri. Ni kweli kwa sababu Chenge hakujipa uwaziri. Ni kweli kwa sababu alijua kuwa kama lengo lingekuwa ni kuunda serikali ya watu safi na makini yeye asingekuwamo.

Ni kweli kwa sababu aliyemteua hakuwa ameishiwa watu wa kuteua kushika nyadhifa za uwaziri. Ni kweli kwa sababu serikali ilikuwa inaundwa upya baada ya kuvunjika kutokana na kashfa ya ya kampuni feki ya Richmond iliyopewa tenda ya kuzalisha umeme wa dharura bila kustahili.

Kauli ya Chenge ilikuwa ya kweli kwa sababu alijua aliyemteua alijua 'madudu' yake, ambayo alilenga kuyalinda kwa kuwa na Chenge karibu.

Zaidi ya hayo, Chenge alishapigiwa kelele za kutosha kuwaamsha hata waliokuwa wamelala. Kila ilipotajwa mikataba mibovu ya serikali kwa miaka 10 iliyopita, Chenge alihusishwa.

Zilipoguswa rushwa za kimfumo zinazowagusa wakubwa serikalini, Chenge alihusika. Alijua, na rais wake alijua, kwamba haikuwa bahati mbaya yeye kutajwa katika orodha ya mafisadi Septemba mwaka jana.

Yeye na rais wake walijua kwamba upepo wa kisiasa ulikuwa mbaya dhidi ya Chenge; na kwamba kwa uongozi unaozingatia maslahi ya wananchi, uteuzi wake ulikuwa kejeli kwa wananchi hao.

Ukweli huu ndio ulimpa Chenge ujasiri wa kuwadhihaki waliokuwa wanamhoji. Ukweli huo ndiyo ulikuwa chanzo cha jeuri yake. Ni kweli. Kama Rais Jakaya Kikwete asingemtaka, asingemteua.

Aliyemteua anajua alichokuwa anataka kukilinda kwa kumrejesha Chenge kwenye Baraza la Mawaziri. Na kama kuna mtu alipaswa kuulizwa ni huyu, si Chenge. Kwa hiyo, Chenge alikuwa sahihi na alisema kweli.

Inasikitisha kwamba Rais Kikwete hakuhojiwa moja kwa moja, bali alifikishiwa ujumbe huo kwenye habari zilizoandikwa zikimnukuu Chenge; na wengine tulimhoji kupitia makala magazetini.

Kama angekuwa kiongozi msikivu, naye alipaswa kuchukua hatua pale pale na kumvua uwaziri, maana wananchi tulishatilia shaka uteuzi wake huo. Badala yake, rais alijivalisha jeuri ya Chenge, akaogelea katika matope yale yale.

Kile kile alichodhamiria kukipuuza, kwamba haendeshwi na vyombo vya habari, sasa kimefumuka kwa njia nyingine na kuwaumbua wote wawili – yeye na Chenge wake.

Kwa sababu hiyo, kujiuzulu kwa Chenge si sifa ambayo mashabiki wa serikali wanapaswa kuitumia kuisafisha serikali na chama chao. Haiwasafishi. Fursa ya kujisafisha walikuwa nayo huko nyuma, hawakuitumia.

Kwanza hakupaswa kuwamo kwenye Baraza la Mawaziri mwaka 2006 kwa sababu Rais Kikwete alimjua vema kabla hajaingia madarakani. Wapo watu ambao walipotangazwa tu kuwa mawaziri, wenye kutazama upande mwingine wa shilingi walitilia shaka umakini wa rais.

Miongoni mwao Chenge alikuwamo. Ikaja fursa ya pili ya kujikosoa na kujisafisha. Mambo yalipokwama mwaka jana rais akabadili mawaziri na kuwahamisha wizara. Akashindwa kumwondoa Chenge na mizigo mingine!

Badala yake akamhamisha kutoka wizara ya Afrika Mashariki na kumfanya kuwa Waziri wa Miuondombinu. Hii ni moja ya wizara nyeti kabisa hapa nchini. Hakika, Kikwete hakustahili kumkabidhi Chenge wizara nyeti kama hii.

Lakini fursa ya wazi ni pale waziri mkuu wake (Edward Lowassa) alipomsaidia kuvunja baraza. Likaundwa na upya na kina Chenge wamo!

Hiyo ilikuwa ishara tosha ya kujua uhusiano wa Chenge na Kikwete, na uzito wa Chenge katika serikali ya awamu ya nne. Ndiyo maana hatukushangaa alipotamba kwamba rais anajua kwanini alimteua!

Sasa wengine wanasema yawezekana uhusiano wao ulikuwa na uhusiano na hivyo vijisenti vyake – kama vile walivyokuwa wanamsema Nazir Karamagi; kwamba Kikwete hana pesa lakini anapenda kuzungukwa na wenye nazo!

Bahati mbaya, yaliyomkuta Karamagi yanakaribiana na yaliyomkuta Chenge. Karamagi alisaini mkataba wa Buzwagi akiwa safarini kikazi nje ya nchi pamoja na rais.

Sula la 'vijisenti' vya Chenge limemwagwa hadharani akiwa China kwenye ziara pamoja na rais. Na kama vile ambavyo Chenge alikwepa kwenda Uingereza asije kuhojiwa na waandishi wa habari kuhusu sakata hili, rais naye ameahirisha ziara ya Uingereza (18/04/2008) akamtuma Makamu wa Rais.

Hii inaonyesha kuwa ingawa rais alikuwa na jeuri ya kumteua Chenge, kumlinda na kunyamazia shutuma dhidi yake – kana kwamba anawakomoa Watanzania – bado alijua dhambi yake, na hakutaka kusutwa zaidi baada ya mambo kuanza kumwagika yenyewe.

Na sasa wanadhani kwa kuwa amejiuzulu wao watapona. Wanakosea. Kwanza, tutawaona watu makini iwapo hatua zitachukuliwa dhidi ya Chenge. Maana kama ni kujiuzulu tu, si mwisho wa sakata hili.

Kujiuzulu ni hatua moja. Maana yake amekubali tuhuma ili achunguzwe kwa uhuru. Kama serikali inajidai inatawala kwa sheria, basi tungependa kuona mkondo wa sheria ukitumika, hata kama ni dhidi ya bilionea.

Hii tabia ya watu kujiuzulu tu bila kushughulikiwa au kurejesha wanachodaiwa kuiba, hailisaidi taifa, wala haikisafishi Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake. Tutafika mahali itakuwa desturi; mtu anatuhumiwa, anajiuzulu lakini haguswi na vyombo vya dola.

Lakini sote tunajua vyombo vyetu vya dola vinawaumiza wadogo na wanyonge, hata kwa kuwasingizia. Hata hili lingesuasua tu kama si kuibuliwa na vyombo vya Uingereza na baadaye kuvaliwa njuga na vyombo vya nyumbani.

Rais na watu wake walijua kwamba katika serikali yake ya mamba, wamo kenge wengi, na Chenge alikuwa mmojawapo. Walijaribu kufunika kombe lakini zamu hii 'mwanaharamu amekataa kupita.'

Sawa amejiuzulu, lakini serikali haijawa safi. Ni kazi ya rais kuisafisha. Vunja yote, unda upya. Wateuliwe wachapa kazi, watumishi waadilifu. Hilo ndilo Watanzania wanalolitarajia. Kama atashindwa historia itamhukumu pamoja nao.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: