Kikwete utachomoka Dowans?


Paschally Mayega's picture

Na Paschally Mayega - Imechapwa 19 January 2011

Printer-friendly version

NIMESOMA maandiko ya baadhi ya waandishi waliohoji, nani aliyetufikisha hapa katika sakata hili la Dowans?

Baadhi yao wanasema aliyetufikisha hapa ni Spika wa Bunge, Samwel Sitta na Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza mkataba tata kati ya serikali na kampuni ya kitapeli ya Richmond Development Company (LLC), Dk. Harissn Mwakyembe.

Lakini wapo wanaosema aliyetufikisha hapa ni wewe rais wangu mpendwa, Jakaya Kikwete.

Ndiyo maana umeshindwa kuzungumza lolote juu ya uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa migogoro ya Biashara (ICC) unaotutaka tulipe Dowans mabilioni ya shilingi.

Hawa wanasema, “Kwa namna moja au nyingine Rais unahusika na kashfa hiyo na kwamba Mwakyembe, aliyeisulubu Richmond na baadaye Dowans alikaribia kukutaja wakati akiwasilisha ripoti ya kamati yake mbele ya Bunge.”

Hakukutaja kwa sababu alilenga kukunusuru wewe na serikali yako. Msingi mkuu wa kufanya hivyo, Dk. Mwakyembe na wenzake hasa Sitta waliona hatari ya hoja yao kukataliwa, iwapo jina lako lingekuwapo katika orodha ya watuhumiwa.

Waliamua kufa na Edward Lowassa pekee, mmoja wa maswahiba zako na ambaye wakati huo alikuwa waziri mkuu wako.

Kwa maneno yake mwenyewe Dk. Mwakyembe alisema kamati yake haikuyaweka hadharani mambo kadhaa mazito iliyoyabaini wakati wa uchunguzi wake kwa Richmond, hasa jinsi ilivyopatiwa zabuni ya kufua umeme kinyemela na kinyume na taratibu.

Swali gumu ambalo kila mwananchi anapaswa kujiuliza ni hili: Hivi kulingana na mwenendo wa kashfa hii na ukweli uliojitokeza sasa, rais wangu unawezaje kujiokoa?

Rais wangu, Watanzania waliambiwa kuwa Dk. Mwakyembe na kamati yake walitumia zaidi ya Sh. 400 milioni, fedha za walipa kodi maskini wa nchi hii kusafiri ndani na nje ya nchi walikoona wangeweza kuupata ukweli.

Nao wakaupata. Lakini mwingine wakaamua kuuficha.

Nadhani sasa muda umefika wa rais kusema kila kitu. Kutaja kila mhusika na jinsi alivyoshiriki katika kuangamiza nchi na janga hili. Iwapo nawe umo, basi ni vema ukajitaja.

Haitakuwa busara ukasubiri wengine kukutaja. Tayari wapo vimbelembele wanaotaka jambo hili lirudi tena bungeni. Angalia wasije wakakutajia huko.

Hili ni muhimu kwa sababu, vita dhidi ya ufisadi imeigharimu nchi. Kwa muda wa miaka mitatu na ushei minyukano ya kila aina ilipamba moto, huku mkuu wa nchi ukiwekwa katikati na jina lako likitumika kusafisha baadhi ya watuhumiwa na wengine kuwachafua.

Kisa ni kutaka kumridhisha kila mmoja – wale wanadaiwa kutuhumiwa na ufisadi kwa upande mmoja na makamanda wa ufisadi kwa upande wa pili.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja wanasema malipo hayo hayakwepeki.

Lakini mawaziri wako Sitta na Dk. Mwayembe wamejitokeza hadharani kupinga madai hayo na kusema huo ni wizi mwingine ndani ya serikali.

Hata hivyo, linalotushangaza wengi ni ukimya wako rais wangu. Je, wewe msimamo wako uko wapi? Au unahofia kujitosa kwa kuwa Dk. Slaa alishakutaja kuwa ni miongoni mwao?

Suala hili lina utata maana mkuu wa nchi umekaa kimya kwa sababu hutaki kuonekana mbaya.

Rais wangu kama ukweli uliofichwa ungewekwa hadharani na serikali yako ikaporomoka kama ambavyo wengine wanadai kuwa ingetokea, haya mateso yanayolikumba taifa yangetoka wapi? 

Labda wangekuja wengine kuendesha serikali ambapo wangekuwa makini katika kuhakikisha kesi hii tunashinda mahakamani.

Hata haya mauaji ya Arusha pengine yasingetokea. Hata mchezo mchafu uliochezwa na wana mtandao wako mwaka 2005 usingechezwa katika uchaguzi uliyopita.

Ndugu zetu waliuawa na polisi hawakuwa na kosa, bali walikuwa wanapigania haki zao, ikiwamo kuzuia malipo haya ya Dowans.

Wanaodai haki wanauawa na wataendelea kuuawa mpaka walioficha ukweli watakapoamua kuusema ili wauaji wapate kuporomoka.

Ni Watanzania wangapi wanatakiwa wauawe na kujeruhiwa hata waiguse mioyo yenu ili uwekwe wazi ukweli uliofichwa?

Wana deni kubwa watu hawa kwa watu wa nchi hii. Watanzania hawatabaki mabwege milele! Lakini kitu ambacho nataka waelewe kuanzia sasa ni kuwa iko siku isiyo na jina Watanzania wataandamana nchi nzima kudai ukweli uliofichwa ambao ungewaondolea mzigo wa mateso waliobebeshwa! Siku hiyo haiko mbali sana.

Katika mazingira haya, Rais wangu watu utatoka vipi ndani ya Dowans? Usipotoka watu wako wakasema kati ya wanaolipwa na baba yumo, watakuwa wamekosea wapi?

Kimya kimekuwa kingi. Simama useme unachokijua kuhusu malipo kwa Dowans, ili watu wako wakuelewe, vinginevyo itakuwa vigumu kukutoa hasa katika kipindi hiki cha lala salama ambapo hata wale wasio na sifa ndani ya chama chako wanatamani kurithi nafasi yako katika uchaguzi ujao wa mwaka 2015.

Mwandishi wa makala hii, Paschally Mayega amejitambulisha kuwa msomaji wa MwanaHALISI. Anaishi Dar es Salaam. Anapatika kwa simu Na.0713334239
0
Your rating: None Average: 4.7 (3 votes)
Soma zaidi kuhusu: