Kikwete, viko wapi vyama vya msimu?


Hilal K. Sued's picture

Na Hilal K. Sued - Imechapwa 15 September 2010

Printer-friendly version

AKIHUTUBIA mkutano wa kampeni mkoani Tanga wiki iliyopita, mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete alisema vyama vya upinzani ni vya “msimu.”

Siamini kama Kikwete alilenga vyama kama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) au Chama cha Wananchi (CUF), ingawa bila shaka alikuwa anataka wasikilizaji wake waamini hivyo.

Aidha, Kikwete hawezi akasema, bila ya kutafuna maneno kwamba chama chake, hakipati tija yoyote kwa kuwepo wingi wa vyama vya upinzani.

Duniani kote, hasa katika nchi hizi za Afrika, wingi wa vyama hunufaisha chama kilichopo madarakani.

Kwa mfano, katika uchaguzi wa urais nchini Kenya mwaka 1992, Daniel arap Moi alishinda kwa asilimia 35 ya kura, huku wapinzani wake wakuu, Kenneth Matiba wa FORD na Mwai Kibaki wa DP, na vyama vingine vidogo, walipata asilimia 65 ya kura zilizosalia.

Baada ya uchaguzi, Kenya ilibadili mfumo huo na kuweka sharti la mshindi kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura.

Pamoja na kwamba mshindi wa uchaguzi anapatikana kwa wingi wa kura, lakini kuna kila dalili kuwa iwapo Kikwete atabahatika kushinda, ataweza kupata chini ya asilimia 50.

Tukiacha hilo la wapinzani kugawana kura, kuna hili jingine la kuvifanya baadhi ya vyama kama mradi wa chama tawala.

Wengi wa viongozi wa vyama hivyo huwa na uswahiba au “hununuliwa” na viongozi wa CCM ili kutoa kauli zenye lengo la kuvidhoofisha vyama makini vya mageuzi. Mifano ipo mingi na vinafahamika hata kwa majina.

Kwa jumla, kauli ya Kikwete, kwamba vyama vya upinzani ni vya msimu haina mashiko. Kikwete na CCM yake, kwa mfano, hawawezi kusema kuwa CHADEMA ni chama cha msimu.

Hawezi kusema, CUF ni chama cha msimu. Hawezi! Hii ni kwa sababu, mara baada ya kuapishwa kuwa rais wa Jamhuri, 21 Desemba 2005, Kikwete amekuwa katika wakati mgumu kujibu hoja za upinzani.

Ndani na nje ya Bunge, serikali ya CCM na Kikwete mwenyewe, wamekuwa wakihaha kujinasua kutoka katika lundo la kashifa za ufisadi zinazoikabili serikali yake.

Hakuna sehemu ambako CCM imejikuta katika hali ngumu kama suala la ufisadi; suala ambalo CHADEMA ilikuwa imelivalia njuga na kukitoa chama hicho kamasi kwa kipindi chote cha miaka mitano ya utawala wa Kikwete.

Je, katika mazingira haya, Kikwete anaweza kusema CHADEMA au CUF ni chama cha msimu?

Kama CUF ni chama cha msimu, nini kilichosababisha yeye na serikali yake kusalimu amri kule Zanzibar na kuicha CUF leo ikipepea kwa kujihakikishia nafasi ya kuingia serikali, iwe jua au mvua?

Wala hakuna mashaka, kwamba ni CHADEMA na mgombea wake wa urais, wakati huo akiwa mbunge wa Karatu, Dk. Willibrod Slaa iliyoibua na kuweka hadharani rasilimali za umma zinavyokwapuliwa na kikundi kidogo cha watu.

Katika hatua moja, Spika wa Bunge la Jamhuri, Samwel Sitta aliwahi kunukuliwa akimtaka Dk. Slaa kutoa ‘vielelezo’ alivyokuwa navyo. Alipowasilisha alidai kuwa ni feki na hivyo angemchukulia hatua za kisheria.

Isitoshe, upinzani na hasa CHADEMA wameonyesha, na kwa ushahidi kwamba baadhi ya fedha zilizokwapuliwa katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), zilitumika katika kampeni zilizomwingiza yeye madarakani.

Hatimaye serikali ikakubali kusalimu amri na kuruhusu ukaguzi wa hesabu kufanyika katika akaunti ya EPA. Yaliyofumuka kuanzia hapo yanajulikana kwa wengi, kama siyo kwa kila mmoja, akiwamo Kikwete.

Haya ufisadi katika Richmond ulipigiwa kelele na upinzani ukiongozwa na CHADEMA. Ni baada ya kushinikiza Bunge kuunda Kamati Teule kuchunguza tuhuma hizo.

Yaliyotokea yanafahamika. Kwamba Edward Lowassa alilazimika kujiuzulu, tena kwa aibu.

Hata pale ambapo Kikwete alipora majukumu ya mwendesha mashitaka mkuu wa serikali (DPP), mahakama na bunge, kwa kutoa msamaha wa jumla kwa watuhumiwa wa EPA, ni wapinzani waliomjia juu Kikwete.

Je, kweli Kikwete anaweza kusema CHADEMA ni chama cha msimu?

Ni upinzani uliokaba koo serikali katika ufisadi uliohusu uchimbaji dhahabu Buzwagi, ununuzi wa rada chovu na kwa bei ya kuruka, ukwapuaji mabilioni ya shilingi uliofanywa na makampuni ya Meremeta, Deep Green Finance Limited na ujenzi wa Minara Miwili BoT.

Katika chaguzi ndogo za ubunge zilizofanyika katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, vyama ambavyo Kikwete ameita vya msimu, ndivyo ambavyo vilikitoa kamasi chama chake.

Kwa mfano, matokeo ya uchaguzi katika jimbo la Tarime, Biharamulo na Busanda, yameonyesha kuwa CHADEMA siyo chama cha kuchezewa.

Kimsingi vyama vya upinzani haviwezi kubezwa kwa kauli za rejareja za viongozi wa CCM. Kuna mengi ambayo vyama hivi vimeyafanya na ambayo yameleta tija kwa wananchi.

Bali tukijenga hoja kuhusu CCM, hicho ndicho chama kinachojisahau zaidi. Huwa kinachukua kila kitu na kukabidhi serikali na chenyewe kwenda likizo hadi uchaguzi mwingine.

Wakati huo, vyama vya upinzani huwa vinaibuka na kuzama vikitafuta jinsi ya kukabiliana na “zimwi” mwishoni mwa miaka mitano. Tuseme kweli, nani wa msimu katika hali hii: CCM au vyama vya upinzani?

CHADEMA au CUF vingekuwa vyama vya msimu, CCM ingekuwa imelala ikisubiri ushindi. Sivyo ilivyo.

Angalia. CCM imejifunza kutumia helikopta kufika ambako ni vigumu kufika kwa magari au ambako ingetumia muda zaidi. Imepunguza siku za mapumziko za mgombea wake. Imekataa kukutana na wagombea wa vyama vingine katika mdahalo wa wazi.

Wananchi wapigakura hawawezi kuamini kile anachosema Kikwete. Wanaona anasema uongo na mwisho wa waongo huandaliwa na wananchi waliochoka kudanganywa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: