Kikwete wa 2005, siyo wa 2010


Hassan Juma's picture

Na Hassan Juma - Imechapwa 27 October 2010

Printer-friendly version
Rais Jakaya Kikwete akikampeni 2010

Mwaka 2005 Rais Jakaya Kikwete alichaguliwa kwa kishindo na wananchi wa kada mbalimbali. Alikubalika kutoka Pwani hadi Bara, Kusini hadi Kaskazini. Sababu zilikuwa nyingi.

Lakini kubwa kuliko yote ni mbinu safi na chafu zilizowezesha uhamasishaji wa vyombo vya habari na ushabiki uliopindukia. Hapakuwa na muda wa kutosha kutafiti rekodi yake ya utendaji na hulka zake nyingine ambazo wakati huo, zilikuwa hazifahamiki kwa wengi.

Sisi tuliokuwa karibu naye, tunakubaliana jambo moja, kwamba Jakaya alikuwa hapendi kujiingiza katika mijadala migumu inayohusu hali ya nchi.

Kila inapojitokeza kuanzishwa mjadala huo, Jakaya alikuwa mjanja wa kubadilisha mada hiyo na kama alionekana kushindwa kuzuia mjadala huo, alikuwa mwepesi wa kuahidi kuwa atashughulikia jambo hilo maana anajua chanzo chake.

Miaka mitano baadaye, Jakaya anafahamika vizuri kwa walio karibu naye na hata walio mbali. Uwezo wake na udhaifu wake sasa viko wazi zaidi. Kwa hiyo, Jakaya wa mwaka 2005, kwa wananchi waliowengi, si huyu wa mwaka 2010.

Chini ya utawala wa Jakaya, taifa letu limeshuhudia mengi ya kuwafanya waliompigia kura mwaka 2005 wafikiri mara mbili kumpa kura mwaka huu.

Mtangulizi wake, Benjamin Mkapa aliacha taifa lenye uchumi imara, dola yenye nidhamu, na chama chenye mshikamano.

Lakini miaka mitano baada ya Mkapa kuondoka madarakani, uchumi wa taifa uko mashakani na matumaini ya wananchi juu ya taifa lao yamekuwa madogo mno.

Ni kwa sababu hata yeye mwenyewe na ilani ya chama chake hawaahidi mabadiliko yoyote yatayorejesha matumaini. Hata hicho ambacho Kikwete anahubiri, “Amani na mshikamano” havitokani na wao kutendewa haki au kuwa na maendeleo mazuri, bali hutokana na kuishi kwa matumaini kuwa siku moja hali itakuwa njema.

Uongozi ndiyo njia pekee ya kuwahakikishia wananchi kuwa hali ya baadaye itakuwa njema kuliko ilivyo sasa. Matumaini hayo sasa hayapo, na wengi ndani ya CCM wanakubaliana kuwa chini ya Jakaya hilo haliwezekani.

Hao ndio waasisi wa kauli mbiu ya “Chagua mtu siyo chama.” Kada mmoja maarufu wa CCM amesikika akisema kuwa “CCM safi lakini Jakaya bomu.”

Kwa bahati mbaya, sauti za namna hii hazitakiwi ndani ya CCM, maana zikisikika, akina Jakaya na kundi lake wanakimbilia kusema kuwa “hao ni wale walioshindwa mwaka 2005.”

Kichama, Jakaya alirithi chama chenye mshikamano na nidhamu, lakini akaasisi siasa za makundi yaliyomwingiza madarakani.

Ni makundi hayo yalioendelea kukihujumu chama na dalili zinaonyesha kuwa yamekuwa yakiongezeka kila kukicha, badala ya kupungua; kumkabidhi nchi mtu aliyeshindwa kuuunganisha chama chake ni hatari tusiyoweza kuimudu huko mbeleni.

Matokeo ya makundi haya, ndiyo yaliyomfanya Jakaya aiamini familia yake kuliko viongozi wenzake katika chama.

Jakaya alipokea taifa lenye umoja, lakini lenye majeraha ya ubaguzi aliouanzisha wakati yeye anaingia madarakani.

Baada ya miaka mitano, tuna taifa lililogawanyika kikanda, kiitikadi, kimatabaka, kidini na hata kimtizamo. Mwenyewe anadai tofauti za mtizamo ni kitu cha kawaida na hapajatokea mtu wa kumhoji juu ya usemi huu aliouzoea sana kuutumia kila mara.

Nijuavyo mimi, tofauti za mtizamo ndiyo msingi wa tofauti nyingine zote. Hii ni kwa sababu shughuli ya mwanadamu huanzia ubongoni mwake.Kwa hiyo, mtizamo ndiyo msingi wa maamuzi tufanyayo mara nyingi hata kama taaluma mbalimbali zinasisitiza umuhimu wa kufungia mitizamo yetu mahali fulani ili kuruhusu mawazo mapya ya kutuwezesha kufanya maamuzi yasiyo na harufu ya ubinafsi.

Mathalani, katika kampeni zinazomalizika, kumekuwepo na fikra za kuwa Kikwete anakataliwa na wapigakura kwa sababu yeye ni Muislamu. Hizi ni fikra potofu.

Watu hawa wanajuwa kuwa mwaka 2005 Jakaya alikuwa muislamu, lakini bado akachaguliwa kuongoza taifa. Hivi sasa, anapoomba uongozi kwa mara ya pili, bado ni muislamu yuleyule na wapiga kura ni walewale wanaomkataa sasa.

Mwaka huo huo aligombea na kupambana vikali na mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe ambaye ni mkiristo. Lakini Mbowe alikataliwa na wakiristo ambao waliomchagua Jakaya.

Mtizamo wa Jakaya na wenzake ni kuwa Dk. Slaa anakubalika kwa sababu ya ukiristo wake badala ya ukweli kwamba kuona kuwa utendaji na msimamo wa Dk. Slaa ndio unaomfanya akubalike.

Sababu nyingine ya kukubalika kwa Dk. Slaa ni hali mbaya inayowakabili Watanzania chini ya utawala wa Jakaya. Hata ndani ya CCM tunakubaliana kuwa hali ya kukosa matumaini inaweza kuongoza wapigakura kumchagua mtu asiyetegemewa.

Kushamiri kwa siasa za udini hakukuanza na uchaguzi huu, bali hata ndani ya chaguzi za ndani ya CCM harufu ya udini imekuwamo, lakini hukemewa na viongozi wenye msimamo unaoeleweka na ambao wanaojua wanachokisimamia katika chama.

Lakini hatua ya sasa ya kukemea udini kwa kuwatumia wakuu wa mikoa na wilaya, kumezalisha fikra za kuwa Jakaya anapokabiliwa na upinzani, ni mwepesi wa kukimbilia visingizio vinavyoongeza mipasuko katika nchi kuliko kuipunguza.

Hivi sasa majeshi yote yanadaiwa kuwa yamewekwa katika hali ya tahadhari utafikiri nchi inakwenda vitani. Kwa CCM na Jakaya, dalili za kutokubalika kwao ni uhaini usioweza kuvumiliwa na kulazimisha majeshi yachukue nafasi yake kutishia umma.

Hofu hii, kwa namna ya ajabu, inamuonyesha Jakaya asivyo makini katika matumizi ya vyombo vya dola. Tumeshuhudia wiki hii, vyombo vya dola vikimkamata mgombea ubunge wa Temeke kwa “kosa” la kumtusi Jakaya, lakini kabla havijamaliza kumhoji, yeye Jakaya mwenyewe akawatusi Watanzania wote kuwa ni “kusanyiko la majuha.”

Inaonekana kiongozi huyu anapungukiwa na uwezo wa kuwaleta wananchi pamoja kwa sababu mara zote ana kundi na upande anaoushabikia hata kama anafanya hivyo kwa kutumia simu, huku akijifanya kukaa kimya bila kuonyesha mwelekeo katika masuala ya msingi.

Kimsingi, hali ya nidhamu serikalini inatisha sana maana sasa viongozi wa kuu wa dola na hata katika sekta nyeti, wamegeuka wafanya biashara wakuu, huku majukumu ya kidola yakichanganywa na biashara.

Enzi za kuona viongozi waandamizi wa dola wakitumia muda mwingi kufikiri namna ya kuongoza dola na vyombo vyake, hazipo tena. Wamesajiri makampuni kwa majina ya bandia na kuendelea kujikusanyia mamilioni ya shilingi huku wakijipatia kubwa kupitia mikataba mbalimbali ya serikali.

Jakaya anayajua haya, lakini hawezi kuyabadili na akafanikiwa kubaki salama.

Kutokana na sababu nilizozitaja hapo juu, ni wazi kuwa kura za Jakaya zitapungua sana na hata kushindwa katika uchaguzi unaofanyika kesho Jumapili.

Ni kwa sababu, Jakaya si mgombea salama hata kidogo katika makundi yote na matabaka yote ndani ya taifa. Kwa tabaka la mafisadi wanaomiliki uchumi wa nchi na raslimali zake, Jakaya ni bima yao na rafiki mwema.

Ufisadi wa kiwango tulicho nacho, kuulinda na kuuhakikishia usalama, inahitaji kiongozi mahiri na shupavu katika kufanya maamuzi. Jakaya si mmoja wa viongozi hao.

Kwa tabaka la walalahoi, Jakaya aliwatosa muda mrefu sana pale alipoamua kwenda na mafisadi. Amekiri mwenyewe hajui nini chanzo cha umaskini nchini.

Ahadi zake kwao hazitekelezeki na nchi wahisani wanajua hivyo. Kuwahakikishia usalama walalahoi wa taifa hili, kunahitajika kiongozi makini, asiyewaogopa walalahoi na kuwa tayari kujibu kero zao.

Jakaya amekwepa sana kuhojiana na walalahoi na badala yake anachagua aulizwe nini, wapi na nani?

Kugongeana mikono wakati wa kampeini, kuhani misiba, au kubeba watoto wadogo hadharani, si dalili kuwa wewe ni kiongozi wa watu.

Walalahoi wanahitaji sera na hatua madhubuti za kuwapatia haki yao ya msingi katika taifa lililosheheni utajiri unaonufaisha wachache.

Hali kadhalika wasomi, wana harakati, wana habari, wajasiria mali, watendaji serikalini, vyama vya ushirika, wafanyakazi, wanafunzi wa vyuo vikuu, wakulima vijijini, wanawake na vijana hawana uhakika wa kulindwa na kusikilizwa chini ya Jakaya kwa miaka mitano ijayo.

Walio wengi katika makundo haya, hawatampa kura labda wakilazimishwa na “kamati za ufundi” katika majimbo ili kuokoa jahazi linaloonekana kuzama kwa kasi ya ajabu.

Nikubaliane na ujumbe wa “sms” moja iliyozunguka nchini siku za karibuni ikisema, “Mwaka 2005, tulihukumiwa kifungo cha miaka 10. Baada ya miaka 5, umetolewa msamaha kwa wafungwa. Tutumie fursa hii kuwa huru…”.

Mwandishi wa makala hii, Yusup Haji amejitambulisha kuwa ni msomaji wa MwanaHALISI na mwanachama mwaminifu wa CCM. Anaishi Dar es Salaam.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: