Kila uchao ni mbinu chafu mpya, tuzipuuze


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 13 October 2010

Printer-friendly version
Jamvi la Weledi

KWA muda wa wiki sasa nimekuwa natumiwa ujumbe mfupi wa maandishi kwenye simu zangu zikilenga kumkashifu mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa.

Ujumbe huu unatumwa kutoka kwenye simu namba +3588108226 na unasema hivi:

“Slaa ni mropokaji na mgomvi anatukana vyombo vya ulinzi na usalama. Anataka damu imwagike ili mradi aingie Ikulu. Tumkatalie kuigeuza nchi yetu Somalia.”

Kwa bahati mbaya sijui kama nilikuwa mlengwa wa sms hizo kwa sababu, ujumbe huo niliupata kwenye simu zangu tatu tofauti. Awali nilijaribu kujibu ujumbe huo, lakini baadaye nikataka kuzungumza na mwenye hiyo namba iliyokuwa ikisambaza ujumbe husika. Sikufanikiwa. Nilibaki najiuliza kwamba kwa nini leo Slaa anaonekana kuwa hivyo?

Watanzania wengi walikuwa hawamjui Dk. Slaa kwa maana ya kwenye anga za kisiasa hadi mwaka 1995 alipoamua kuondoka kwenye Chama Cha Mapinduzi (CC) baada ya kufanyiwa mizengwe katika kinyang’anyiro cha ubunge katika jimbo la Karatu licha ya kuongoza kweny kura za maoni.

Ni kutokana na jeuri ya madaraka ya CCM. Dk. Slaa alikuwa amemshinda mbunge aliyekuwa amemaliza muda wake, Patrick Qorro, lakini kwa sababu ya ukaribu wa Qorro na wakubwa wa chama wakati huo, Dk. Slaa akaenguliwa na nafasi yake akapewa Qorro.

Alipoingia upinzani, Dk. Slaa alimshinda kwa mbali chaguo la wakubwa Qorro katika uchaguzi mkuu mwaka 1995, akatetea tena kiti hicho mwaka 2000 na mwaka 2005.

Tangu aingie bungeni ni vigumu mno kusema kuwa Dk. Slaa si mbunge ambaye amekwenda juu ya uwakilishi wa jimbo la Karatu. Ameishi kama kiongozi na kuwakilisha mawazo ya Watanzania wengi ambao wabunge wao waliowapigia kura waliwatosa na kuendesha biashara nyingine kule bungeni.

Nirejee kwenye mada yangu sms dhidi ya Dk. Slaa. Swali ambalo nimejiuliza ni hili, ni kwa nini Dk. Slaa kwa miaka 15 amesimamia mambo ya kimsingi, kama vita dhidi ya ufisadi.

Akiwa mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, Dk. Slaa, ameandika historia ya aina yake. Ameadabisha watendaji wanaokiuka taratibu za matumizi ya fedha za umma katika halmashauri za miji, wilaya na manispaa.

Amelia na matendo machafu ya watawala kwa kipindi chote hicho, lakini leo hii wahuni wachache wanataka kuaminisha watu kuwa ni “mropokaji na mgomvi … Anataka damu imwagike…?”

Haya nimeyatazama na kuyapima katika uwanja mpana wa kisiasa hasa katika fukuto la uchaguzi mkuu na kuona kwamba sms ni sehemu tu ya mkakati mzima wa mbinu za kuangamizana kwenye uchaguzi.

Ujumbe huu unaotumwa kumchafua Dk. Slaa ni zile za kusambazwa kwa watu wengi kama zinazosambazwa kwa ajili ya promosheni ya makampuni ya simu, huu ni mkakati unaolenga kumkamata mtu mmoja mmoja.

Ingawa mbinu za kusambaza ujumbe kwa njia ya simu ni halali katika zama hizi za maendeleo katika sekta ya mawasiliano, si rahisi njia hizo kutumika bila kupitia mamlaka zinazodhibiti mawasiliano nchini.

Kwa maana hiyo, kama Dk. Slaa na watu wakitaka kujua nani hasa anasambaza ujumbe huo, ni rahisi sana, cha kufanya ni kuwasilisha malalamiko Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Katika kipindi cha wiki mbili, zimeibuka mbinu zenye mkanganyiko sana zikilenga kuwavuruga wapiga kura.

Nia ya matamko haya, kama lile lililotolewa na vyombo vya ulinzi na usalama’ likisomwa hadharani na Mnadhimu Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Luteni Jenerali Abdurrahman Shimbo, lilikuwa kama onyo kwa vyama vya siasa, wanasiasa, vyombo vya habari na mashirika yasiyo ya kiserikali, ni kujengea watu hofu.

Lakini mkakati huo unaonekana kama sasa umekuwa ni wa kudumu kwa kuwatumia pia viongozi wa dini kama ambavyo kwa nyakati tofauti masheikh ama kwa kujua au kutokujua wamejikuta wakitumbukia katika mambo ya kisiasa na kwa mtindo ambao unaonyesha dhahiri kumtaka kumshughulikia Dk. Slaa.

Ninapotazama mawasiliano haya yote ninayaweka kwenye jukwaa moja la mikakati ya watu wanaoitwa spin doctors wakijaribu kugeuza upepo wa kisiasa kwenda watakako kwa kuwaingizia wananchi hisia zilizokengeuka juu ya wagombea urais.

Duniani kote inajulikana kwamba kazi ya ma-spin doctor wanaufanya umma uamini usiku ni mchana na machana ni usiku. Wanasukumwa na kitu kimoja tu. Kulinda watu wao ili waonekane wanafaa na hivyo kukubalika kwa umma.

Hawafanyi kazi ya kujenga hoja zenye nguvu, zenye ushawishi wa kweli ila wanasumbuliwa zaidi na historia za hao wanaowafanyia kazi.

Lakini kibaya zaidi ni ukweli kwamba ma-spin doctor wanafanya kazi ya kupenyeza mambo mabaya dhidi ya wapinzani wao kwa kuwa wanajua wapinzani wao wana nguvu kubwa, wana ushawishi mkubwa na kwa kweli wana nafasi kubwa ya kuaminiwa na pengine kupewa ridhaa
Ndiyo maana watu wenye akili zao walipoona masuala ya ndani kama mahusiano binafsi ya Dk. Slaa na Josephine Mahimbo, yalipowekwa hadharani kwa uhabiki mkubwa na msukumo mkubwa wa kisiasa, walijua kwamba kazi imeanza.

Lakini pia wakati Ukatoliki wa Dk. Slaa ambaye amekuwa mbunge kwa miaka 15 na kabla ya hapo diwani wa CCM kwa zaidi ya miaka mitano, ulipoanza kuwa ni jambo la kujadiliwa baada ya kuutaka urais, waungwana walijua kwamba jamaa wako kazini.

Cha kushangaza ni kwamba wakati mbinu hizi chafu zikiendeshwa kwa kasi ya moto wa nyika tangu, umma umeamua kupuuza yote yanaosemwa dhidi yake; umefanya hivyo kwa kuwa wanamsikiliza, wanamfuata kwenye mikutano yake, wanamuunga mkono, wanamchangia fedha na kumuombea ili afike safari yake salama.

Mtu anapotafakari mbinu hizi chafu za kutaka kuchafuana ili kupata madaraka anapaswa kujuliza, gharama ya madaraka ni kubwa kiasi hicho?

Je, kama mbinu chafu zinaruhusiwa kuwa sehemu ya uchaguzi wenye kanuni na maadili yake? Huyu anayetumia mbinu hizo akishinda, nini kitamfanya kusimama katika uadilifu?

Ndiyo maana umma unapaswa kujihoji na kujitazama sana kama 31 Oktoba 2010 utakapojongea sanduku la kura dhamira itakayowaongoza ni nini? Kupata viongozi wachapa kazi ambao wamethibitisha kwa matendo halisi au kusukumwa kwa parapaganda?

Wanapojongea sanduku la kura ni lazima walau kukumbuka kwamba fursa nyingine ya kuweza kufanya mabadiliko kuanzia kwenye udiwani – ambao huunda mabaraza ya halmashauri; ubunge ambao huunda Bunge na rais ambaye huunda baraza la mawaziri, ni miaka mitano ijayo. Ni fursa adimu kweli!

Nitoe rai kwa kila mmoja, kwamba tuwasililize wagombea. Mbinu chafu hazina nafasi katika mchakato mzima wa uchaguzi, zipuuzwe na kudharauliwa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: