Kila zama zina mashujaa wake


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 13 October 2010

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

MASHUJAA hawazaliwi wakiwa mashujaa. Hakuna shujaa ambaye anakuja katika jamii ya watu akiwa ni shujaa tayari.

Mashujaa hutengenezwa na historia. Matukio na mang’amuzi mbalimbali ya maisha ya watu yanaweza kuwabadilisha baadhi yao na kuwafanya wawe mashujaa; watu walioushinda woga na kuamua kufanya mambo ambayo yanazidi maslahi yao wao wenyewe, kwa ujasiri na kwa kujitoa hata kuwa tayari kufa kwa ajili yake.

Naomba ieleweke sizungumzii viongozi! Nazungumzia mashujaa. Siyo kila mtu anayejiita au kuitwa kiongozi ni shujaa, na siyo kila shujaa ni kiongozi lakini inapotokea jamii imempata kiongozi ambaye ni shujaa, basi jamii hiyo iko katika nafasi nzuri zaidi ya kujilinda na kujisogeza mbele.

Katika uchaguzi huu unaokuja wapo viongozi na wapo mashujaa. Wapo wanaotaka kuwa viongozi na wapo ambao ushujaa unaletwa mabegani mwao na historia.

Kwa upande wa urais, kuna tofauti kubwa sana kati ya wagombea. Wapo ambao wanaamini ni viongozi wazuri na wengine wamejionesha kuwa ni viongozi wazuri.

Lakini kati yao naamini ni mmoja tu anasimama kama shujaa yaani mtu jasiri aliyeamua kuweka heshima yake, hadhi yake, maisha yake na nafasi yake ili asimamie kitu ambacho ni kikubwa zaidi kuliko yeye mwenyewe.

Jakaya Kikwete si shujaa na Prof Ibrahim Lipumba siyo shujaa ila wote ni viongozi ambao kwa namna moja au nyingine wameweza kuongoza vyama vyao, na kwa upande wa Kikwete serikali yake bila kuonesha ushujaa wa aina yoyote ile.

Lakini tunapochukua jedwali la ushujaa tunajikuta tunabakiwa na mtu mmoja ambaye ametuthibitishia kwa maneno na vitendo vyake kuwa ameweka Tanzania juu ya maslahi yake binafsi.

Dk. Willibrod Slaa angeweza kuwa shujaa kwenye chama chochote. Lakini katika fungate hili la historia ya mwanzo wa karne ya ishirini na moja amepiga magoti kubebeshwa jukumu la kihistoria ambalo Kikwete alilikwepa wakati wake ulipofika.

Nikiwa mmoja wa mashabiki wakubwa kabisa wa Kikwete kabla ya uchaguzi wa mwaka 2005, niliamini kabisa kuwa Tanzania ingeweza kumtumia kuweza kuivusha kuelekea mafanikio.

Yote hayo yalihitaji ushujaa wa hali ya juu. Lakini changamoto zilipofika mezani kwake zote zimebakia zikishughulikiwa kwa hadhari isiyo ya lazima. Kilele cha hayo ni pale uongozi wake ulipofyata mkia mbele ya mafisadi na kukiri eti “wakikamatwa wote nchi italipuka”.

Hapo ndipo nilipojua kuwa hatuna shujaa ikulu wa kutufaa. Nilipokuwa tayari kusamehe hilo nilijikuta nakatishwa tamaa jinsi uongozi wake ulivyoshughulikia mgongano ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Sijui ni kitu gani lakini ni dhahiri kuwa Kikwete na timu yake, walipoteza kabisa ujasiri wa kwanza kuisafisha CCM na chembe za ufisadi na pili, kuleta umoja wa malengo na mtazamo na upatanisho wa kweli ndani ya chama hicho.

Tunapokwenda kwenye uchaguzi mkuu ukiondoa umoja wa rangi na mshikamano wa jembe na nyundo, CCM hii siyo ile ya Nyerere; kilichopo sasa ni kivuli chake.

Ni kutokana uelewa huo ndipo tunaweza kuona ishara kwa mbali kwanini maelfu ya Watanzania wanafurika kumsikiliza Dk. Slaa, shujaa ambaye historia inamtengeneza mbele ya macho yetu.

Ninafahamu bila ya shaka kuwa uchaguzi haupimwi kwa idadi ya watu kwenye mikutano, na kukubalika kwa mgombea hakuji kwa kuvaa rangi za chama, bali ni maamuzi ya moyoni ya mpiga kura akilinganisha maslahi yake na yale ya nchi yake huku akiweka mbele urithi wa watoto wake.

Dk. Slaa anasimama kama shujaa kwa sababu kwanza inataka moyo kwa mbunge ambaye ni maarufu zaidi kuacha kugombea jimboni kwake ambako angeweza kushinda na kuamua kugombea urais dhidi ya mgombea ambaye ni maarufu ndani ya chama chake na nchini.

Kwa Dk. Slaa kuamua kuacha ujiko wa ubunge akiwa na uwezekano mkubwa wa kushindwa, kwanini mtu ambaye ni maarufu anaamua kuacha furaha na starehe ya kuwa mbunge na kusimama kugombea urais dhidi ya mtu maarufu, chama kikongwe na chenye uwezo wa kumgaragaza kama mcheza mieleka ya sumo?

Jawabu ni moja, kwamba alijiamini kuwa ajenda atakayosimamia yaweza kabisa kuwavuta Watanzania wamwamini na kumfuata.

Tofauti ya viongozi wa kawaida na mashujaa ni kuwa viongozi wakati mwingine wanatumia geresha, vitisho na mbinu chafu za ulaghai ili kuwavuta watu wawafuate.

Mashujaa huongoza kwa kuamuka kusimama peke yao kwanza na kuchukua msimamo ambao unawafanya watu wengine waamue kuwa upande huu au upande wa shujaa.

Kikwete alipewa mara nyingi nafasi za kuwa shujaa. Tangu alipotangaza kuwajua vigogo wa madawa ya kulevya, na kuwa ana majina yao na kuwataka “waache mara moja” hadi kujua wanaotumia ruzuku vibaya za mbolea na pembejeo, lakini hadi hivi sasa hakufanya kile ambacho Dk. Slaa amekifanya nacho ni kuwaita kwa majina yao na wakati mwingine kuwavua madaraka.

Kuanzia kubembelezana na waliofanya ufisadi kwenye shirika letu la ndege la ATCL na uvurugikaji wa mfumo wa elimu ya juu nchini chini ya bodi mbovu ya mikopo ya elimu ya juu, Kikwete ameonesha kushindwa kuonesha ushujaa.

Tangu zamani mashujaa ndiyo hushambuliwa. Watu hawashambulii woga. Kuanzia enzi za kina Mangi Mandara, Sina na Meli hadi kina Mkwawa na Mwanamalundi na machifu wa Kingoni kama kina Nduna Songea Mbano na Mputa na wenzao 66 walionyongwa pale Songea ni wao walioweka maslahi ya watu wao mbele na kwa kufanya hivyo walilipa gharama ya maisha yao.

Leo hii mashujaa wa Tanzania wanashambuliwa tena kwa kukataa utawala uliokuwa mzigo migongoni mwao.

Hivyo, leo hii tunashuhudia shujaa wa siasa za Tanzania katika zama hizi zetu Dk. Slaa akishambuliwa kutoka kila kona; kuanzia ilipojulikana ndiye atakuwa mgombea dhidi ya Kikwete.

Ndugu zangu ukweli uko wazi mbele zetu. Wameshtuka na wanatetemeka kama matete na mabua yanayopigwa na upepo wa joto la kiangazi wanapepesuka.

Kama unakubaliana nami kuwa mashujaa wanastahili kuungwa mkono, “Tumchague shujaa anayetufaa Dk. Slaa”.

Niandikie: mwanakijiji@jamiiforums.com
0
Your rating: None Average: 1 (1 vote)