Kilichofichwa na polisi hiki


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 19 January 2011

Printer-friendly version
Polisi Arusha

JUHUDI za jeshi la polisi za kujikosha baada ya mauaji ya Arusha, zinazidi kugonga mwamba, MwanaHALISI limeelezwa.

Kuanzia Jumamosi iliyopita, jeshi hilo limekuwa likirusha kipindi katika vituo vitatu vya televesheni – TBC, ITV na Channel Ten likionyesha mkanda wa video uliojaaa vipande vya matukio ya jijini Arusha.

Taarifa kutoka Arusha, jeshi la polisi, viongozi wakuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na mashuhuda wengine, zinasema kuna tofauti kubwa kati ya kile kinachosemwa na polisi na ukweli halisi wa kilichotokea jijini Arusha, 5 Januari 2011.

Wakati polisi ikisisitiza kuwa ililazimika kupiga risasi za moto kuzuia wafuasi wa CHADEMA kuteka kituo cha polisi, uchunguzi unaoyesha mauaji yalifanyika mbali kabisa na kilipo kituo cha polisi.

Kwa mfano, mkazi wa eneo la Sakina, jijini Arusha, Denis Machael Shirima, alipigwa risasi ubavu wa kushoto akiwa kwenye eneo la Kaloleni, karibu na baa maarufu ya Picknick.

Kutoka Kaloleni hadi Kituo cha Polisi Kati, kunakodaiwa na uongozi wa polisi kuwa wafuasi wa CHADEMA walitaka kukiteka, ni zaidi ya kilomita moja na nusu.

Kabla ya waandamaji kufika kituoni, wangelazimika kupita kwanza uwanja wa michezo wa Sheikh Amri Abeid, CCM mkoa, Mnara wa Mwenge, Rahaleo Gest House, makaburi ya wazee na shule ya Msingi Mount Meru.

Naye Ismail Omari, alipigwa risasi akiwa katika eneo la jengo la sinema la Metropole, zaidi ya kilomita moja na robo kutoka kituo kikuu cha polisi cha Arusha.

Kutoka eneo hilo kufika kituoni, waandamanaji wangelazimika kufika kwanza shule ya msingi Mount Meru, makaburi ya wazee na Arusha City Park.    

Aidha, baadhi ya vitendo vya ufyatuaji risasi vilifanyika mchana mara baada ya polisi kuanza kutawanya wafuasi wa CHADEMA na kuwakamata viongozi wao.

Raia wa Kenya, Paulo Njuguna Kayehe alipigwa risasi akiwa katika eneo la Jogoo House, karibu na kituo kikuu cha mabasi cha Arusha na benki ya CRDB.

Kutoka CRDB Benki kwenda kituo kikuu cha polisi kinachodaiwa kuwa kilitakiwa kutekwa na waandamanaji, ni lazima kwanza upite soko kuu, msikiti mkuu wa Bondeni, barabara ya Makongoro na Mnara wa Mwenge, umbali wa kilomita zaidi ya mbili.

“Polisi wanataka kujikosha tu. Ukweli unabaki palepale; kwamba mauaji haya yamefanywa kwa makusudi. Ni uwongo kusema polisi ‘walilazimika kutumia risasi za moto ili kujihami na wafuasi wa CHADEMA waliokuwa wanataka kuteka kituo,’ ” anaeleza kiongozi mmoja wa serikali mkoani Arusha.

Inaelezwa kuwa kizaazaa kilianzia eneo la Kaloleni, majira ya saa saba mchana ambapo wafuasi wa CHADEMA, walikuwa wakitembea kuelekea uwanja wa mkutano wa National Milling (NMC).

Waandamanaji walianzia Hoteli ya Mount Meru ambako walikuwa wamefikia viongozi, wabunge na wanachama wa chama hicho kwa ajili ya maandamano na mkutano.

Baada ya waandamanaji kufika eneo la Sanawari, ndipo magari ya polisi yakiwa na askari wa “kutuliza ghasia” yaliyokuwa nyuma ya maandamano hayo, yalipita kwa kasi kwenda mbele kuelekea eneo la Kaloleni. Yaliegeshwa karibu na Hospitali ya Dk. Mohamed.

Waandamanaji waliendelea na safari yao kama kawaida, ambapo kabla ya kufika eneo hilo, walikata kona kwenda kushoto, kuelekea njia inayotokea Mnara wa Mwenge.

Hiyo ilikuwa majira ya saa saba mchana; wakati huo mkutano wa hadhara ambao polisi walisema umeruhusiwa kufanyika ukiwa bado haujaanza.

“Mara baada ya kukata kona na kutembea kama mita 100 ndipo polisi walianza kurusha mabomu ya machozi na kufyatua risasi za moto, jambo ambalo liliwafanya waandamanaji kukimbia hovyo kunusuru maisha yao,” anaeleza mwandishi mmoja wa habari mkoani Arusha, Ramadhani Siwayombe.

Ni katika eneo hilo la Kaloleni ambako yalikuwa yamefikia – yapata kilomita mbili – huku polisi wenye silaha wakiwa wanasindikiza waandamanaji.

Ghafla katika eneo la stendi kuu ya mabasi katika njia inayotoka Benki ya CRDB kukaripotiwa mtu kupigwa risasi, ambapo ndipo alitajwa kuuawa Paulo Njuguna raia huyo kutoka Kenya.

Baada ya taharuki hiyo, taarifa zinasema baadhi ya wananchi wakawa wamejikusanya katika maeneo mbalimbali ikiwamo Kaloleni, nyuma ya uwanja wa Sheikh Amri Abeid, ambapo baadhi yao walianza kurushia mawe jengo la CCM mkoa.

Mara baada ya polisi kupata taarifa kuwa kuna baadhi ya watu wanarushia mawe jengo la CCM, ndipo walipofika eneo hilo na kuanza kurusha mabomu ya machozi na kufyatua risasi za moto.

Ni katika eneo hilo inaelezwa Denis Shirima alipigiwa risasi. “Alikuwa akitoka dukani kununua oil; akiwa na kidumu kidogo, wakati huo akirejea Sakina kwenye gereji yake,” ameeleza ndugu yake.

Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe akielezea kilichotokea Arusha alisema, “Chokochoko zote zilianzishwa na polisi. Kinachofanyika sasa ni kutaka kujikosha.”

Amesema, “Sisi tulianza kuondoka kwenye hoteli ya Mount Meru majira ya saa sita mchana kuelekea uwanja wa NMC ambako ndiko tulipanga kufanyia mkutano wetu wa hadhara. Lakini tulipofika eneo la Kaloleni, umbali wa kilomita kama mbili na nusu, polisi wakaanza kutushambuilia.”

“Mimi nilikamatiwa katika eneo hilo. Viongozi wengine wa chama, akiwamo mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, walikamatiwa katika eneo hilohilo. Vurugu zote unazosikia zilianzia katika eneo hilo,” anaeleza Mbowe kwa sauti ya kusononeka.

Anasema mara baada ya kutoka hapo, polisi walianza kupiga risasi ovyo, kurusha mabomu ya machozi na kuanza kushambulia watu ovyo mitaani.

Hata mkutano wa hadhara ambao viongozi wake walinukuliwa wakisema uliruhusiwa kufanyika, “…ulishambuliwa kwa mabomu na risasi za moto,” ameeleza.

Alipotakiwa kutoa ufafanuzi hasa wa kilichotokea, Mbowe alijibu, kuwa walipofika Kaloleni, gari moja ya polisi – ambao walikuwa nao tangu mwanzo – “lilitupita kwa kasi, katikati ya watu. Lilipofika mbele, askari wakashuka na kuanza kushambilia gari la kwa virungu gari la Mheshimiwa Grace Kiwelu (Mbunge, Viti Maalum).”

Anasema, “Mimi nilikamatwa wakati nilipokuwa nawazuia polisi kumshambulia Mheshimiwa Lucy Owenya (Mbunge, Viti Maalum).”

Alipoulizwa kwa nini Dk. Slaa hakuwa miongoni mwa watu ambao walikamatwa awali, Mbowe alisema Dk. Slaa na mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo waliwaomba kutangulia kwenye mkutano kutokana na matatizo yao ya kiafya.

“Maandamano yale yalikuwa ya zaidi ya kilomita tatu na kwa kasi tuliyokuwa nayo, tulimuomba Mzee Ndesamburo kutangulia uwanjani. Vivyo hivyo, tulimuomba Dk. Slaa, kutokana na matatizo ya mkono wake, naye atangulie uwanjani,” ameeleza Mbowe.

Naye Lema aliliambia MwanaHALISI juzi Jumatatu wakati linakwenda mitamboni kuwa madai kwamba waliouawa walikuwa wanataka kuteka kituo cha polisi, hayana ukweli wowote.

“Hayo ni madai ya uwongo kabisa. Kati ya watu 31 waliopigwa risasi na kujeruhiwa, waliosemewa mashitaka hawazidi watatu. Sasa kama kweli madai ya polisi yangekuwa yana ukweli, mbona hawa waliojeruhiwa hawakufikishwa mahakamani,” anahoji Lema.

Anasema, “Lakini pili, na ambalo ni kubwa zaidi, kama kweli kulikuwa na njama za kutaka kuteka kituo, kama polisi wanavyodai, mbona sisi sote tumefunguliwa shitaka moja la kufanya maandamano bila kibali?”

Ni Dk. Slaa, akiwa katika viwanja vya NMC, aliyeinuka na kutoa taarifa kwa wapenzi wa chama hicho kuwa mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, wabunge kadhaa na baadhi ya viongozi wamekamatwa na wapo kituoni na kwamba tayari kuna viongozi wameenda kushughulikia suala lao.

Akiwa bado anataka kutoa ufafanuzi ghafla kuliibuka tena tafrani katika uwanja huo kwa polisi kufika wakiwa na magari manne na kuanza kurusha mabomu ya machozi.

Ni katika mazingira hayo, Dk. Slaa alionya kuwa “…huo ni uchokozi” kwa kuwa mkutano huo ni halali kwa mujibu wa katiba na una baraka zote za kisheria.

Akiwa bado anaendelea kutoa maelezo, polisi nao waliendelea kurusha mabomu na risasi za moto, jambo lililomlazimu Dk. Slaa kushuka haraka na kujificha chini ya jukwaa. Maelfu ya watu walitawanyika kuogopa kipigo cha polisi, amesimulia kiongozi mmoja wa CHADEMA.

Mara baada ya hali kutulia; na kwa kuonyesha ujasiri wa kipekee, Dk. Slaa alipanda tena jukwaani na kuanza kuhamasisha wananchi kurejea katika viwanja ili kuendelea na mkutano huo.

Kufuatia wito huo, umati mkubwa wa wananchi ulirejea na kusikiliza taarifa aliyokuwa akiitoa Dk. Slaa juu ya viongozi wake kukamatwa na kisha kumpa kipaza sauti Ndesamburo ambaye alilaani kitendo hicho.

Dk. Slaa alirejea tena jukwaani na kusema kuwa taarifa walizopata ni kuwa dhamana imekubaliwa kwa viongozi na wabunge waliokamatwa lakini sharti lililotolewa ni mpaka ifike saa 12 jioni.

Baada ya kusema hivyo, akasema kuwa kutokana na hali hiyo haoni sababu ya wao kuendelea na mkutano wakati viongozi wao wako rumande.

Mara baada ya kusema hivyo mabomu tena yakaanza kurushwa uwanjani hapo na wananchi kila mmoja kuanza kutawanyika kwa njia yake.

Chanzo cha zogo la Arusha, kinyume na inavyoelezwa, kimetokana na uchaguzi wa Meya wa jiji la Arusha ambapo msimamizi wa uchaguzi, kaimu mkurugenzi wa jiji la Arusha, Estomii Chang’a kuitisha uchaguzi bila kushirikisha CHADEMA.

Awali madiwani wa CHADEMA walihudhuria kikao cha baraza hilo kilichofanyika 17 Desemba ambacho kiliitishwa na Chang’a; ambapo kikao hicho kilipangwa kufanya kazi mbili.

Kwanza, kuwaapisha madiwani ili kuthibitishwa kuwa ni madiwani halali wa jiji hilo; na pili kuchagua Meya na Naibu Meya.

Lakini kabla ya madiwani kuapishwa, ulizuka mtafaruku juu ya kuwapo kwa mbunge wa Viti Maalum (CCM), kupitia mkoa wa Tanga, Mary Chatanda.

Mzozo huo ulisababisha shughuli zote kusimama na kuanza kutafuta suluhisho ambalo maelekezo yake yalipatikana majira ya saa 10: 40 jioni na hivyo Chang’a kushauri madiwani waapishwe kwanza huku ikiwa bado madiwani wa CHADEMA hawajamaliza kujisajili.

Kazi ya kuapisha madiwani ilimalizika saa12.30, kwa mujibu wa Chang'a mwenyewe, na kwamba ilimlazimu kuahirisha kikao cha kuchagua Meya na Naibu Meya.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo na taarifa aliyoitoa katika magazeti ya serikali, Daily News na Habari Leo, ni kuwa usiku huo anadai aliandika barua ya kuwaalika madiwani wote kufika katika kikao siku ya pili kwa ajili ya kufanya uchaguzi. Anasema alituma karani kusambaza barua hizo kwa madiwani wote usiku huo.

Hapo tatizo lilipoanzia. Kanuni za shughuli za mikutano ya halmashauri kifungu Na.37 cha Serikali za Mitaa kinasema, “wajumbe wa mikutano ya baraza wataarifiwa kwa barua saa 24 kabla ya kufanyika kwa mkutano husika.

Madiwani wa CHADEMA, taarifa zinasema, hawakuwa wamepatiwa barua hizo, badala yake barua za kuwaita katika mkutano zilipelekwa usiku wa manane katika baa ya Pentagon inayomilikiwa na Estomii Mallah ambaye alikuwa anagombea nafasi ya umeya kupitia chama hicho.

Barua hizo zilikabidhiwa kwa mlinzi, na kwamba madiwani wa CHADEMA walipata taarifa siku ya pili na kuamua kufika katika mkutano haraka. Walipofika ndani ya ukumbi wa mkutano wakakuta tayari uchaguzi umemalizika.

0
Your rating: None Average: 4.8 (4 votes)
Soma zaidi kuhusu: