Kilichomwangusha Kikwete hiki


Nkwazi Mhango's picture

Na Nkwazi Mhango - Imechapwa 24 November 2010

Printer-friendly version
Rais Jakaya Kikwete

KUNA mambo mengi yaliyosababisha kuanguka vibaya kwa Rais Jakaya Kikwete na chama chake katika uchaguzi uliopita.

Kikwete ameanguka kutoka asilimia 80.2 mwaka 2005 hadi asilimia 61 katika uchaguzi wa mwaka huu.

Kwa ufupi, alishindwa kukidhi matarajio na mahitaji ya umma katika miaka mitano ya utawala wake; hasa kutimiza ahadi kuu ya “Maisha bora kwa kila Mtanzania.”

Kikwete ameshindwa kukuza uchumi; kusimamia urejeshwaji wa mali za serikali ikiwamo nyumba zilizoibwa wakati wa utawala wa rais aliyemtangulia, Benjamin Mkapa. Kikwete aliahidi kurejesha nyumba hizo mikononi mwa umma.

Aidha, Kikwete ameshindwa kuachana na baadhi ya marafiki zake, wakiwamo watuhumiwa wakuu wa ufisadi nchini. Alivunja rekodi kwa kutoa msamaha wa jumla kwa wezi wa fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya taifa (BoT).

Hadi anamaliza kipindi chake cha kwanza cha miaka mitano, karibu watuhumiwa wote wakuu wa ufisadi, akiwamo swahiba wake – Rostam Aziz ambaye anatajwa kuwa ndiye mmiliki wa kampuni ya Kagoda Agriculture Limited, iliyokwapua zaidi ya Sh. 40 bilioni, bado wanaendelea kupeta.

Jingine ambalo lilimfanya Kikwerte kushindwa vibaya, ni hatua ya chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM) – kuzuia mchakato wa kidemokrasia.
Katika kinyang’anyiro cha kutafuta mgombea urais, CCM hawakuruhusu Kikwete kupata mshindani. Alisimama pekee huku nguvu ya ziada ikitumika kuwatisha na kuwanyamazisha walioonyesha nia ya kugombea.

Mfano hai, ni hatua ya Sheikh Yahya Hussein kutisha wanaotaka kumpinga Kikwete. Ikulu ilibariki unajimu wake, badala ya kumkaripia. Jambo hili lilipunguza utamu wa uchaguzi na lilichangia kupunguza kura zake.

Licha ya kutonadi sera zake katika mikutano yake ya kampeni, hakushirikisha chama chake. Kampeni ziliendeshwa na familia na baadhi ya marafiki zake.
Hatua hii ilipunguza kwa kiwango kikubwa kura zake kwa kuwa wengi waliona kuwa mgombea huyo wa urais, anataka kugeuza Ikulu kuwa mradi binafsi wa familia.

Hadi kampeni zinamalizika, Kikwete hakuwahi kutaja mali zake. Kwa baadhi ya watu, hili lilimuondolea umakini na kuaminiwa, hasa wakati huu ambapo ufisadi serikalini umeshika kasi.

Akiwa katika mbio zake za kuusaka urais, Kikwete alipigia debe baadhi ya watuhumiwa wakuu wa ufisadi nchini. Wengine aliwamwagia hata sifa kwa kuwaita, “Jembe la kale” ambalo lingali na makali.

Miongoni mwa waliopigiwa debe na kusifiwa na ambao bila shaka walipunguza kura zake, ni Edward Lowassa, Basil Mramba, Andrew Chenge na Rostam.
Sababu nyingine ni ukweli kuwa licha ya kuwakatisha tamaa wapiga kura, serikali na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), walishindwa kuandaa na kusimamia uchaguzi wenye sifa na viwango vinavyotakiwa.

Angalia idadi ya waliojitokeza kupigakura. Ni pungufu kwa asilimia 30 ya waliojiandikisha.

Jingine ni hatua ya rais kunyamazia shutuma nyingi za wazi na kweli zilizoelekezwa kwa serikali yake.

Vilevile, hatua ya Kikwete kushindwa kueleza vyanzo vyake vya fedha ilipunguza sehemu ya ushindi wake.

Pamoja na kwamba Kikwete na chama chake walizindua kampeni ya kuchangia chama chao, lakini kila mwenye akili timamu aliona kwamba fedha zilizotumika, haziwezi kupatikana kwa njia ya michango ya “karata tatu.”

Kitu kingine kilichomwangusha ni kutokemea wazushi waliotumia baadhi ya vyombo vya habari na waandishi wa habari mmojammoja.

Kwa mfano, hatua ya gazeti la serikali, HabariLeo, kushupalia maisha binafsi ya mshindani wake mkuu katika kinyang’anyiro cha urais, Dk. Willibrod Slaa, kilipunguza kura za Kikwete.

Sababu nyingine ni matumizi mabaya ya vyombo vya dola na shutuma dhidi ya idara ya usalama wa taifa, kwamba imepanga kuchakachua kura. Haya pia yalipunguza kura zake.

Pamoja na kwamba watuhumiwa walijitahidi kukanusha, lakini maelezo waliyotoa hayakuaminika.

Pia rais aliridhia watu waliokamatwa wakitoa rushwa kupitishwa na chama chake kugombea nafasi za ubunge na udiwani katika maeneo mengi nchini.
Kesi zilizolistua taifa ni pamoja na ile iliyomhusu Magreth Sitta na Betty Machangu. Vigogo hawa waliendelea kuwa wagombea na kuruhusiwa kukipigia kampeni chama chao. Haya yalipunguza kura za rais.

Sababu nyingine ni matumizi ya fedha za umma kwenye kampeni zake. Rejea shutuma zilizotolewa dhidi ya mke wa rais, Mama Salma Kikwete ambaye alituhumiwa kutumia ndege na magari ya umma.

Hii ni nje ya tuhuma kwamba asasi yake ya WAMA ilitumika katika kumpigia kampeni mumewe na chama chake. Yote haya yaliupunguza kura za Kikwete.
Hadi sasa, mke wa rais, watoto wake – Ridhiwani Kikwete na Miraji, wanaonekana ni sura ya utawala bila kuchaguliwa na yeyote wala kutajwa popote katika katiba.

Hili liliwachukiza wapigakura wengi kiasi kutoona sababu ya kumrejesha Kikwete madarakani.

Haya ni nje ya tuhuma za rais kutumia fedha nyingi kwa safari za nje, badala ya kutatua matatizo ya nchi.

Ongezeko la deni la taifa; mfumko wa bei; kudhoofika kwa sarafu ya Tanzania kulinganisha na dola ya Marekani na kuongezeka kwa pengo kati ya walionacho na wasionacho, vyote hivyo vimechangia kutaka kumuondoa ikulu.

Kushindwa kwa rais kukabiliana na wahafidhina waliotaka Samwel Sitta anyang'anywe kadi ya CCM, ni sababu nyingine ya Kikwete kuambulia asimilia 61 ya kura. Kuna waliomwona ama ni dhaifu au anabeba mafisadi.

Sababu nyingine kubwa ni Kikwete kuendelea kuzuia kuandikwa kwa katiba mpya ambayo ingekuwa muarobaini wa kukabiliana hasa na ufisadi.

Kimsingi mambo mengi yaliyosababisha Kikwete kugeuka “chukizo la wananchi” na si chaguo na kipenzi chao, japo ataendelea kuwa rais.

Ni vema yeye na chama chake wangeziangalia ili achukue hatua ya kukabiliana nazo kabla ya uchaguzi wa mwaka 2015.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: