Kilimo kikubwa, utumwa mpya


Joseph Mihangwa's picture

Na Joseph Mihangwa - Imechapwa 31 March 2009

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

KATIKA hali isiyotarajiwa, na pengine bila ya utafiti na uchambuzi makini, Tanzania sasa imetangaza kuingia katika kile kinachoitwa “Mapinduzi ya Kijani” ya nchi zilizoendelea.

Mapinduzi ya Kijani maana yake ni Kilimo cha Mashamba makubwa na endelevu, chenye kutumia zana za kisasa kama vile matrekta, mashine za kuvuna (combined harvester) na viwanda vya kusindika mazao ya kilimo.

Kile ambacho kinapendekezwa na wataalamu wa kilimo ni kwamba, mkulima wa Tanzania mwenye kutumia jembe la mkono na plau hatakiwi; anapaswa kutupwa mara moja kwenye jumba la makumbusho asionekane tena, na “Mapinduzi ya Kilimo” yatawale na kuongeza uzalishaji.

Ndiyo kusema kwamba, programu za kumwendeleza mkulima mmojammoja, ili naye aweze kuwa mkulima endelevu, zilizoasisiwa enzi za uhuru, sasa basi!

Lakini swali muhimu ni hili: Ni wapi duniani mapinduzi ya kilimo yameleta neema (badala ya shari) ili yaweze kuigwa? 

Siku zote mapinduzi ya kijani yameambatana na matumizi ya mbegu zilizorekebishwa – genetically modified seeds” (GM), maarufu kama “Miracle Seeds”, mbegu zenye maajabu kwa uzalishaji zaidi. 

Mbegu hizi zilibuniwa na wana-mikakati wa Marekani kama sehemu ya mkakati wa kudhibiti kuenea kwa ukomunisti, kwa kufungua soko kamili la teknolojia ya kilimo kwa nchi masikini.

Mmoja wa wanamkakati hao, John King, aliwahi kuandika, “Mapambano kati ya Mashariki (ukomunisti) na Magharibi (ubepari) barani Asia, kwa sehemu kubwa, ni mashindano katika uzalishaji, na mpunga ni ishara ya mashindano hayo.”

Kuanzia miaka ya 1960, juhudi za nguvu ziliendelezwa kueneza mapunduzi ya kijani na “Kurekebisha Kilimo” kwa ujumla kwa nchi masikini bila kujali matokeo yake.

Hii haikuwa ajabu kwamba, baada ya kuratibu uzalishaji katika kilimo kwa njia ya zana kubwa na mashamba makubwa huko Marekani Kaskazini, katika miaka ya 1960, makampuni ya kilimo ya kimataifa (Agri-business Multinationals), yakaanza kutafuta masoko mahali pangine.

Kwa mfano, kati ya mwaka 1968 na 1975, Kampuni ya Zana za Kilimo ya International Harvester, iliongeza mauzo nje ya Amerika Kaskazini, kutoka chini ya asilimia 20 hadi asilimia 33 ya mauzo yote; John Deer kutoka asilimia 16 hadi 23 na Massey – Ferguson kutoka asilimia 40 hadi 70.

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) ndilo limepewa kazi ya kuratibu ukuaji wa shughuli za makampuni haya.  Baadhi ya makundi yake ya kikazi ni pamoja na majina makongwe kama Caterpillar, Tractors, John Deer, Fiat, FMC, Massey – Ferguson na Mitsui.

Kwa kuwa Kilimo kikubwa cha zana kubwa hutumia mafuta, vivyo hivyo makampuni makubwa ya mafuta yanaingia humo. Haya ni pamoja na British Petroleum (BP) na Shell. 

Ushirikiano kati ya FAO na makampuni ya kuhodhi unakwenda hadi kwenye (dawa) viua wadudu. Kundi la viua wadudu huhamasisha matumizi ya dawa hata pale palipo na njia mbadala ya dawa.

Mbegu za miujiza (GM), au kwa jina la kuzifagilia “High Responsive Variety (HRV), hazikubali kupandwa hivihivi na mkulima akavuna mazao mengi. Ingekuwa hivyo, makampuni haya yasingehusishwa.

Ili mbegu za HRV zitoe mazao mengi, zinahitaji umwagiliaji maji wa viwango vikubwa namaalum, matumizi ya mbolea, viua wadudu na viua magugu.

Ili uzalishaji uwe wa faida, sharti kiwe kilimo kikubwa kwa maana ya ukubwa wa mashamba na teknolojia – matrekta, haro, mashine za palizi, upukuaji na zana za kuvuna mashamba makubwa.

Kwa ufupi, mapinduzi ya kijani yanataka matumizi ya teknolojia na pembejeo za Kilimo, ambapo vyote hivyo vinahitaji mafuta, na kwa sababu hii mkulima mdogo hawezi kutarajia hata siku moja kuwa “mwana-Mapinduzi ya Kijani.”

Badala yake atakuwa manamba katika mashamba makubwa ya wenye uwezo. Huu ni utumwa mpya chini ya sera za Benki ya Dunia na nchi zenye viwanda. Mahali popote mapinduzi ya kijani yalipojaribiwa, yamesababisha bei ya chakula kupanda. 

Kupanda kwa bei ya mafuta kutaongeza bei ya nafaka. Kwa sababu pembejeo lazima ziagizwe kutoka nje, sekta ya kilimo ndiyo pekee inayolipia, na kwa maana hiyo kilimo cha mazao kama kahawa, pamba, chai, mkonge, korosho au tumbaku, lazima kipanuliwe kukidhi haja hiyo.

Ili kutimiza hili, sehemu ya ardhi ya kilimo cha chakula lazima itumike, na hivyo mkulima kulazimika kugawa muda wake kati ya kilimo cha mazao ya biashara ambayo serikali inayataka (na kwa yeye kupata fedha kulipia kodi), na kilimo cha chakula kwa ajili ya familia yake.

Kodi kubwa (na michango mbalimbali) na kuanguka kwa bei ya mazao ya biashara, itamlazimisha mkulima kuongeza eneo la kilimo cha mazao ya biashara. Lakini kwa kuwa ardhi ya kilimo kikubwa italimwa kwa mfululizo bila kupumzishwa, itapoteza rutuba haraka. 

Na ili kuiokoa ardhi, mkulima ataanza katumia mbolea za viwanda. Na kadri bei ya mbolea itakavyozidi kupaa, ataacha kuitumia. Hapo ataanza kugundua kwamba ardhi yake haiwezi kuota mimea tena na jangwa litaanza kunyemelea.

Mbali na madhara ya ki-ekolojia katika kufuata sera za kilimo za FAO na Benki ya Dunia, kuna hili ambalo wengi hatulioni: Kwa karne nyingi za majaribio, wakulima wadogo wameweza kuzalisha mbegu madhubuti za asilia, zenye kuvumilia matatizo ya ki-ekolojia. 

Mbegu hizi zitatoweka haraka pale mapinduzi ya kijani yanaposhinikizwa. Lakini FAO na Benki ya Dunia wanajua jinsi zinavyoibwa na kuhifadhiwa huko Ulaya. 

Haitashangaza kuona siku moja tukiuziwa mbegu hizohizo zikiwa zimebadilishwa kidogo tu na kufungwa kwenye pakti, zikiuzwa kwa fedha za kigeni.

Kwa kukimbilia mapinduzi ya kijani, serikali inajivua wajibu wa kumwendeleza mkulima mdogo na kufungua milango kwa masetla; hivyo kumfanya abaki kibarua kwenye ardhi ambayo bado anaihesabu kuwa ni urithi kutoka kwa mababu zake.  Huo ni utumwa mpya.

0
No votes yet