KIM JONG-IL: Kiongozi mgonjwa anayetumia "waigizaji" kumwakilisha


Zakaria Malangalila's picture

Na Zakaria Malangalila - Imechapwa 04 November 2009

Printer-friendly version

AFYA ya kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-Il imekuwa ikiandikwa sana na vyombo vya habari, hasa vile vya Ulaya na Marekani.

Kuna habari kuwa kiongozi huyo amekuwa mahututi kwa muda mrefu. Pia inasemekana huenda alishafariki siku nyingi.

Hawa wanasema kufariki kwake hakujatangazwa rasmi kwa hofu ya kuzuka mgogoro mkubwa wa kisiasa – ikizingatiwa kuwa mwanawe wa mwisho aliyemtaja kuwa atamrithi angali mdogo wa kushika hatamu.

Utata wa afya ya Kim Jong-Il umezua habari kwamba huenda kuna mtu (na pengine watu) anayefanana naye sana anatumiwa katika shughuli mbalimbali za kitaifa anazopaswa kuhudhuria Kim Jong-Il, ikiwamo kupokea wageni mashuhuri kutoka nje.

Kwa mfano, kuna habari kwamba alipotembelea Pyongyang, mji mkuu wa Korea Kaskazini Agosti mwaka huu, Rais mstaafu wa Marekani, Bill Clinton, hakukutana naye, bila kutambua, bali alikutana na kufanya mazungumzo na mtu aliyefanana tu na Kim Jong-Il.

Wachunguzi wa mambo nchini Korea Kusini wanaamini siyo picha zote zinazotolewa rasmi na serikali ya Korea Kaskazini humuonyesha kiongozi wake ni zake halisi.

Badala yake, wanasema, mtu anayefanana na Kim Jong-Il ndiye hutumika katika baadhi ya safari na ziara maeneo ya mashambani, viwandani, katika tafrija za kimila, kambi za jeshi na nyinginezo.

Imekuwa vigumu kupata uthibitisho wa taarifa hizi. Lakini wakimbizi kadhaa wa Korea Kaskazini waliovuka mpaka na kuingia Korea Kusini wanasema kuna “waigizaji” zaidi ya mmoja wanaotumiwa “kumwakilisha” Kim katika shughuli mbalimbali za kitaifa.

Ha Tae-young, mmiliki wa kituo cha radio Korea Kusini kiitwacho Radio for North Korea ambacho hurusha matangazo yake kwa saa mbili kila siku yakielekezwa Korea Kaskazini, anamnukuu mkimbizi aliyetoka nchi hiyo ya Kikomunisti akisema:

“Namfahamu msichana ambaye baba yake ni mwigizaji wa Kim Jong-Il. Hivi karibuni kiongozi huyo alipunguka sana uzito… amekonda sana. Hali hii inamfanya mwigizaji huyo naye ale kwa mpangilio ili kupunguza uzito.”

Aidha kuna baadhi ya watu wa Korea Kusini wameufanya “uigizaji” wa namna hiyo kuwa mtaji hasa katika mahojiano na televisheni na masuala ya michezo ya kuigiza.

Watu kadhaa wanaojitahidi kufanana na mwigizaji huyo wamekuwa wakionekana katika vipindi vya vichekesho katika televisheni, sehemu za usiku za starehe na hata katika filamu za kawaida.

Hata hivyo, baada ya Rais wa zamani wa Korea Kusini, Kim Dae-jung, kutembelea Korea Kaskazini na kukutana na Kim Jong-Il katika mkutano wa kihistoria (kwani nchi hizo mbili zina uhasama mkubwa), serikali ya Seoul, ilishauri mambo ya kumwigiza Kim yaachwe kwani yangeweza kuharibu juhudi za kuleta maelewano kati ya nchi hizo mbili.

Lakini tofauti na “waigizaji” wa Kim wa Korea Kusini, wenzao wa Korea Kaskazini hufanya hivyo kwa kuagizwa na serikali yao na hivyo hufanya kwa umakini mkubwa.

Toshimitsu Shigemura, mwandishi wa vitabu raia wa Japan, alikiambia kituo  cha televisheni kuwa Kim amekuwa mgonjwa kwa zaidi ya miaka kumi sasa, na huenda hata ameshafariki.

Anasema laiti ni Kim halisi, aliyeonekana dhaifu ndani ya ukumbi wa Baraza Kuu la Umma (Bunge) siku chache baada ya Korea Kaskazini kurusha kombora lake la masafa marefu Aprili 5 mwaka huu, basi huyo alikuwa si Kim, bali mwigizaji tu, ambaye ndiye huyo huyo aliyekutana na Bill Clinton Agosti.

Shegemura, ambaye pia ni mwandishi wa gazeti mashuhuri la Japan liitwalo Mainichi Shimbun, aliongeza: “Walikuwa ni watu tofauti kabisa, kwani Agosti alionekana na afya njema.”

Shigemura anahisi “muigizaji” huyo aliongea na Bill Clinton katika mazungumzo yao ya dakika 17, yaliyomwezesha mstaafu huyo wa Marekani kuishawishi serikali ya Kim kuwaachia Wamarekani wawili waandishi wa habari waliokuwa wanashikiliwa kwa muda wa siku 140 na nchi hiyo baada ya kuingia nchini kinyume cha sheria.

Aidha Shigemura anaamini kwamba “muigizaji” mwingine, kwa niaba ya Kim alikutana na Waziri Mkuu wa China, Wen Jiabao na mkuu wa Hyundai Asan, kampuni ya magari ya Korea Kusini.

Naye Choi Jin-wook, mhadhiri wa taasisi inayojishughulisha na masuala ya kuunguanisha Korea mbili – Korea Institute of National Unification – anasema viongozi hawa wanaotawala kidikteta mara nyingi huhitaji sana kutumia watu wanaofanana nao kwa maslahi ya kiusalama.

Anasema aliyekuwa kiongozi wa Iraq, Saddam Hussein naye pia alikuwa akitumia hila hii, sawa alivyofanya aliyekuwa kiongozi wa Uganda miaka ya 1970, Idi Amin Dada, na hata Adolf Hitler wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Hata hivyo anaongeza kuwa huenda wahariri wa picha wa Korea Kaskazini wanatumia picha za zamani za Kim alipokuwa katika afya nzuri kwa kuzifanyia utaalamu ili zionekane zimepigwa leo.

zakmalang@yahoo.com
0
No votes yet