Kimolo: Sijafikiria kwenda CHADEMA


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 23 June 2012

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii
Gabriel Kimolo

ALIYEKUWA Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Gabriel Kimolo amekanusha uvumi ulionea kuwa ana mpango wa kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Kimolo alijiuzulu ukuu wa wilaya 4 Mei 2012, akitaja sababu tatu za kuchukua uamuzi huo, ikiwamo ya serikali kukumbatia ufisadi.

Sababu ya pili ni serikali kushindwa kutatua matatizo ya pembejeo, ununuzi wa kahawa mbivu; na Rais Jakaya Kikwete kuchelewesha uteuzi wa wakuu wa wilaya kwa mwaka mmoja na miezi sita, hivyo kumfanya ashindwe kupanga mipango yake ya kazi na kibinafsi.

Kujiuzulu kwake kumeharakisha uteuzi wa wakuu wa wilaya. Siku tano baadaye Waziri Mkuu Mizengo Pinda alitangaza wakuu wapya wa wilaya walioteuliwa na Rais Kikwete, akiwamo Dk. Michael Kadeghe anayejaza nafasi ya Kimolo katika wilaya ya Mbozi.

Siku mbili baada ya kujiuzulu ukuu wa wilaya gazeti moja lilitaja baadhi ya sababu za uamuzi huo, ikiwamo lilichoita “hisia za wananchi”, kuwa Kimolo alikuwa na mpango wa kwenda CHADEMA.

Kimolo (50) amelieleza MwanaHALISI kuwa madai ya kuhamia CHADEMA au chama chochote cha upinzani ni uvumi tu, yeye hajafikiria suala hilo.

“Huo ni uvumi tu. Mimi sijafikiria kuhamia chama chochote na wala sijafanya mazungumzo yoyote kuhusu suala hilo,” amesema.

Lakini, amesema kwa umri wake wa sasa bado ni kijana, hivyo lolote laweza kutokea katika maisha yake ya baadaye.

Mwanasiasa huyo amefafanua kuwa bado yuko CCM, lakini ameshindwa kuweka bayana kama ataomba tena kugombea ubunge katika Jimbo la Babati Vijijini.

Aliwahi kuomba nafasi hiyo mara mbili, na kuibuka wa pili kila mara katika kura za maoni.

Akisisitiza suala hulo, amesema, “Siwezi kusema ndio au hapana. Mimi ni mwanasiasa tangu nilipokuwa na umri wa miaka 30. Hii itategemea na hali itakuwaje wakati huo…Kwa kweli inategemea na mipango ya Mungu.”

Kitendo cha kujiuzulu nafasi hiyo kiliibua malumbano, yakimhusisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro aliyepuuza sababu za Kimolo kujiuzulu, na kuutangazia umma kuwa “alikimbia baada ya kupata taarifa za kutokuwamo kwenye uteuzi mpya.”

Kimolo amekanusha madai hayo akisema hakuwa na taarifa zozote kuhusu suala hilo. Hata baada ya Waziri Mkuu kusisitiza madai hayo, yeye amesema hakuwa na taarifa za uteuzi kabla ya majina ya wakuu wa wilaya kutangazwa.

“Mimi sitaki malumbano na hawa wakubwa. Mimi nilishasema sikuwa na taarifa hizo, basi,” amesema.

Amesema mambo mengi yaliyomuudhi hayakutokana na viongozi wakuu kitaifa, yaani Rais Kikwete na Waziri Mkuu, bali jinsi uongozi wa Wizara ya Kilimo na Ushirika, chini ya Profesa Jumanne Maghembe ulivyoshindwa kushughulikia matatizo ya kilimo wilayani mwake.

Miongoni mwa mambo yaliyomkera na kujiuzulu ni baadhi ya kampuni za kununua kahawa kuvunja na kukaidi amri ya wilaya ya kukataza ununuzi wa kahawa mbivu kwa kejeli kuwa, “wao hawaongei na mbwa bali wanaongea na mwenye mbwa”.

Wanaotoa kejeli hizo, amesema pia wanakingiwa kifua na uongozi wa wizara.

Tatizo jingine ni eneo la vocha za pembejeo, ambalo amesema ‘limegubikwa na mizengwe mingi ya utawala na utendaji wizarani.”

Katika eneo hilo, Kimolo anasema kulitokea wizi wa vocha katika ngazi zote, taifa, wilaya na vijiji, ucheleweshaji wa vocha na mawakala kutolipwa fedha zao.

Kwa mujibu wa Kimolo, sababu za kujiuzulu kwake bado ni sahihi na uamuzi huo ameuchukua mwenyewe bila kushawishiwa na mtu yeyote.

“Mke wangu nilimweleza kwanza, akanielewa. Kwa hiyo hana tatizo. Watoto wangu bado wadogo ndo wanajiuliza imekuwaje, lakini nao taratibu wataelewa,” amesisitiza.

Kimolo alikuwa anazungumza kwa simu kutoka nyumbani kwake Babati, Manyara alipokwenda kuwaeleza ndugu na jamaa zake ili waelewe sababu za “uamuzi mgumu” aliochukua.

Mwanasiasa huyo ambaye ni mtaalamu wa masuala ya idadi ya watu, pia amekanusha kuhusishwa na kundi linalomuunga mkono Waziri Mkuu aliyejiuzulu Edward Lowassa katika harakati zake za kuwania urais mwaka 2015.

Taarifa zilizolifikia gazeti hili, zimeeleza kuwa Lowassa alikwenda Mbozi na kufanya kikao na Kimolo, na huenda hilo ndilo limemponza.

Pamoja na kukiri kukutana na Lowassa, Kimolo amesema hakuna mazungumzo waliyofanya pamoja wala mikakati waliyopanga, bali mbunge huyo wa Monduli alimuuliza, “unaendeleaje” na yeye akajibu, “ninaendelea vizuri.

“Lowassa alikaa hapa muda mfupi sana. Hata saa moja haikufika. Unajua huyu mtu ananifahamu sana, mimi nimegombea ubunge mara mbili Babati Vijijini na kuibuka namba mbili kwenye kura za maoni,” amesema.

Kimolo ameshika nafasi ya ukuu wa wilaya kwa miaka 13 katika wilaya za Makete, Iringa; Namtumbo, Ruvuma; na Mbozi mkoani Mbeya.

Wananchi wamepokeaje uamuzi wake? “Hao sitaki kuwasemea maana inaweza kuonekana najikweza, wewe kwa muda wako nenda Mekete, Namtumbo na Mbozi waulize wananchi wa kawaida, watakueleza. …mimi nilifanya uongozi makini hadi chini kwa wananchi.”

Amesema hakutumia uongozi wake kujinufaisha na sasa baada ya “kubwaga manyanga” amekuwa kama anaaza upya maisha yake.

Kabla ya kuteuliwa na Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa kuwa mkuu wa wilaya mwaka 1998, Kimolo alikuwa mtumishi wa umma kwa miaka minane katika ofisi mbalimbali, ikiwamo ikulu.

Msomi huyo wa Shahada ya Pili katika masuala ya idadi ya watu (demografia), amewahi kuwa mkufunzi katika kilichokuwa chuo cha Kilimo Nyegezi, chini ya wizara ya kilimo na chakula. Shahada ya kwanza ya demografia aliipata katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mwaka 1995 baada ya masomo ya Shahada ya Pili, alihamishiwa katika ofisi ya rais na 1998 akahamia ofisi ya waziri mkuu kitengo cha maafa alipofanya kazi kwa miezi saba, kabla ya kuteuliwa kuwa DC Makete.

0
No votes yet