Kinana: Mitaji ya CCM Jumapili


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 27 October 2010

Printer-friendly version

“TUNAINGIA katika uchaguzi mkuu tukiwa na wabunge 19 na madiwani 562 ambao wameshinda kutokana na kupita bila kupigwa.”

Hivyo ndivyo Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana anavyoanza mahojiano yake rasmi na MwanaHALISI wiki hii, ofisini kwake, Dar es Salaam.


 Anasema pia kuwa bajeti ya serikali katika elimu imeongezeka kutoka Sh. 1 trilioni hadi Sh. 2.4 trilioni huku idadi ya wanafunzi chuo kikuu ikikua kutoka   38,000 kati ya mwaka 1961 na 2005 hadi 122,000 leo hii.


Kinana anasema huo ni mtaji mkubwa “unaotuhakishia ushindi. Aidha, chama chetu kimetekeleza kwa zaidi ya asilimia 90 ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2005.”

Kinana alikuwa akieleza kwa nini chama chake kinajitapa kushinda hata kabla ya uchaguzi kufanyika na matokeo kutangazwa.


Anasema kati ya vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi huu, “ni CCM pekee iliyosimamisha wagombea ubunge katika kila jimbo na wagombea udiwani katika kila kata.”

Nchi mzima ina majimbo ya uchaguzi 239 na kata 3,335.


Anasema mbali na vigezo hivyo, ni mgombea urais wa CCM pekee ambaye ameweza kutembelea majimbo yote ya uchaguzi na kuzungumzia hoja zinazohusu eneo alilotembelea.


“Wananchi wanataka hoja za palepale kuhusu barabara, elimu na afya. Wagombea wa vyama vingine, hawakufika kila mahali na hivyo wameshindwa kujua matatizo ya wananchi,” anajigamba Kinana.


Katika nafasi ya urais, Kinana anasema chama chake kinatarajia kushinda nafasi ya urais kwa zaidi ya asilimia 80 na kwa nafasi ya ubunge kwa zaidi ya asilimia 90.


Alipoulizwa iwapo mgombea wake hatafikia kiwango hicho cha ushindi atajisikiaje, Kinana alisema, “Asiposhinda hivyo basi, wapigakura watakuwa wameamua.”

Hata hivyo, alisema haamini kuwa wananchi hawatamchagua Kikwete kwa muhula mwingine wa mwisho wa urais. 

Kuhusu nafasi ya upinzani kushinda nafasi hiyo, Kinana alisema vyama vya upinzani haviwezi kushinda nafasi ya urais kwa sababu mbili kubwa.


Kwanza, anasema vyama hivyo bado ni vichanga, havina mtandao na wala havikujiandaa kikamilifu kwa ajili ya uchaguzi.


Lakini pili, anasema viongozi wa upinzani “wametumia muda mwingi kulalamika na kuzua mambo ambayo hayapo, badala ya kunadi sera.”

Bali Kinana ameshindwa kueleza kile alichoita, “uongo wa upinzani” na nafasi ya “mtandao” mbele ya maamuzi ya umma.


Alipoulizwa kama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama cha Wananchi (CUF) wangekuwa wameungana, kungekuwa na hali kama unayoiona sasa, Kinana amesema, “Hapana.”

“Kama CHADEMA na CUF wangeungana wangekuwa na nguvu zaidi,” anaeleza. Anasema kutokana na uchanga wa vyama hivyo, muungano ungeweza kuvisadia kuwa na nguvu ya pamoja ya kupambana na CCM.


Kuhusu madai kwamba chama chake kimeanzisha makundi ya vijana yanayofahamika kama Green Guard ambapo mkoani Kilimanjaro wanaita “Interahamwe” kwa kuwa vimekuwa vikichochea vurugu, Kinana anakana madai hayo.


Anasema, “Si kweli. Tuna vijana wa UV-CCM ambao jukumu lao ni kulea viongozi wa baadaye wa CCM, kuhamasisha mikutano ya kampeni na kusaidia wapenzi wetu na wanachama kwa jumla kwenda kupigakura.”

Alipong’ang’anizwa kwamba gazeti hili limepata ripoti ya UV-CCM ya mwezi uliopita, inayokiri chama hicho kuanzisha vikundi vya vurugu, Kinana amesema, “Hakuna mahali popote ambapo CCM imekubali jumuiya zake kuanzisha vikundi vya vurugu.”

Badala yake, anatuhumu viongozi wakuu wa CHADEMA kuwa ndiyo wanaochochea vurugu.


Kuhusu kauli za Kikwete kuwa wanaotumia udini na ukabila wanataka kuleta maafa, huku UV-CCM wakikiri kuwa udini na ukabila ndivyo vilivyoleta mgawanyiko ndani ya chama hicho wakati wa kura za maoni, Kinana anajibu:
“Kila uchaguzi unapofika, ukabila na udini vinajitokeza. Lakini sisi wakati wowote tunapiga vita mambo haya,” anaeleza.


Akizungumzia maneno ya kuwa kura “zikiibiwa hatutakubali;” na kwamba hata chama chake kimekuwa kikiyatumia maneno hayo kama mtaji, Kinana alikana kuwa chama chake kutumia kauli hiyo kama mtaji wake kisiasa.


“Hatujatumia maneno hayo kama mtaji. Ingawa upo ushahidi wa kutosha kwamba Freeman Mbowe, mwenyikiti wa CHADEMA, aliishatamka kuwa iwapo kura zitaibiwa kunaweza kutokea umwagaji damu.


Tunachosema sisi ni kuwatahadharisha Watanzania kuepukana na mbinu zozote zinazohatarisha nchi,” anaeleza.


Alipoulizwa kwamba kama anaamini kuwa vita inaweza kutokea iwapo CCM itashindwa, haraka Kinana alijibu, “Siamini kama CCM au chama chochote cha siasa, iwapo kitashindwa uchaguzi, kinaweza kuleta vita.”

Anasema kama kuna yeyote ambaye anaona hakuridhika na mchakato wa uchaguzi ulivyokwenda, anaweza kwenda mahakamani kupinga matokeo yatakayotolewa.


Kuhusu CCM kuwa “bize” katika kampeni hizi kuliko ilivyokuwa katika kampeni za mwaka 2005, Kinana anasema, kila kampeni chama chake kimekuwa kinatenda kama ilivyo katika kampeni za mwaka huu.  

Alipoulizwa anaonaje hatua ya mgombea wake kutoa ahadi ambazo kama hazitatekelezwa, basi chama kitakuwa kimekufa; lakini zikitekelezwa hata kwa nusu, wanaweza kuendelea kujikongoja, Kinana alijitapa kwamba kila kilichoahidiwa kitatekelezwa.


“Kila ahadi ambayo mheshimiwa Kikwete ameahidi itatekelezwa. Ni kwa sababu, kila ahadi ameifanyia utafiti. Amekuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 20 akiwa waziri na mbunge. Amekuwa rais kwa miaka mitano sasa; anajua shida za wananchi,” anaeleza.


Kinana anasema, “Ni kweli baadhi ya ahadi alizotoa kama ilivyokuwa mwaka 2005 hazimo kwenye ilani ya uchaguzi ya chama chetu. Lakini zote hizo kama ilivyokuwa mwaka huo, zitatekelezwa.”

Anasema hata ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma haukuwa katika ilani ya uchaguzi ya CCM. Badala yake, ni miongoni mwa ahadi za papo kwa papo ambazo Kikwete aliahidi.


Swali: Hivi kwa nini mgombea wako hataki kufuata sheria – hata katika mambo madogo kama muda wa kupiga kampeni? Baadhi ya wananchi wanasema ni kwa kuwa amezoea kutokuwa makini. Wewe unaona ni kwa sababu gani?

Jibu: Kwanza, nikiri kwamba Kikwete anapata matatizo mengi ya muda. Wakati sisi tunapanga ratiba zetu, wananchi katika maeneo mengine ambayo hayamo katika ratiba wanavamia msafara wake na kutaka awahutubie kwa kutegemea atatoa ahadi hii au ile. Hayo ndiyo matatizo ambayo tunakabiliana nayo.


Juu ya maoni ya wengi kuwa hata Kikwete akishinda, huu ndio mwisho wa chama chake kushika serikali, kiongozi huyo wa kampeni anasema hakubaliani na hoja hiyo.


Anasema anamini kuwa CCM itashinda uchaguzi huu na itaendelea kushinda katika chaguzi nyingine zinazofuata. Anasema Watanzania wana imani kubwa na CCM kutokana na kazi nzuri ambayo imefanyika.  

Swali: Kuna sababu zozote zilizofanya Kikwete atumie familia yake kupiga kampeni usiku na mchana?

Jibu: Kila zama na kitabu chake. Lazima ukubali kuwa mwaka 1995 na 2000, katika kampeni ya Benjamin Mkapa, Mama Anne Mkapa alishiriki.


Hivi sasa kuna mabadiliko makubwa sana. Mama Salma Kikwete amefanya kazi kubwa ya kuwahudumia wananchi kupitia taasisi yake ya WAMA (Wanawake na Maendeleo). Hivyo ameingia katika kampeni ili kuimarisha nafasi ya mumewe kushinda.


Kuhusu hoja kwamba miaka mitano iliyopita Kikwete aliitwa kijana. Je, bado ni kijana hata baada ya mapambano ya mwaka huu?

Kinana anajibu, “Hapana, Kikwete ana miaka 60 sasa; hivyo ni mtu mzima.


Lakini naamini kuwa ana nguvu ya kuwatumikia wananchi. Namfahamu kuwa ni mwadilifu; anaipenda nchi yake kwa nguvu zote na uzalendo.


Swali: Daktari wake anasema nini juu ya afya ya mgombea wako hasa baada ya kukurukakara za huku na kule bila mapumziko?

Jibu: Binafsi sijazungumza na daktari wa rais. Jambo moja ni dhahiri kwamba Kikwete ana afya nzuri na ametembea masafa marefu kwa muda wa miezi mitatu. Naamini kuwa atamaliza kampeni yake kwa mafanikio.


Swali: Umewahi kunukuliwa ukisema kuwa “Siyo lazima CCM ishinde.” Ni kweli ulisema hayo? Ulitumwa na chama chako au mgombea? Unaamini hayo uliyosema?

Jibu: Sijasema hivyo. Siwezi kusema hayo. Bali mimi nimesema kwamba Watanzania zaidi kuliko vyama. Nikasema ushindi uwe ni kupiga kura na kukubalika.


Kuhusu changamoto ambazo chama chake kilikutana nazo katika kipindi hiki cha kampeni, Kinana anataja utaratibu mpya wa kura za maoni kuwa moja ya changamoto hizo.


 “Utaratibu huu wa kura za maoni katika baadhi ya maeneo ulileta mirafakano mikubwa kati ya walioshindwa na walioshinda. Hivyo imetuchukua muda mrefu na kazi kubwa kushughulikia makundi yaliyoibuka,” anaeleza.


Hata hivyo, Kinana hakutaka kuingia kwa undani kujadili suala hilo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: