Kingunge aanza kupukutika, wengine vipi?


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 09 December 2009

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala
Kingunge Ngombale Mwiru

NIWAKUMBUSHE wasomaji kwamba kuna mwanasiasa mmoja maarufu nchini ambaye ametangulia mbele ya haki, Ditopile Ukiwaona Mzuzuri, huyu achilia mbali siasa alikuwa na mikogo yake. Mungu amrehemu huko aliko.

Dito kama alivyojulikana na wengi, alipata kutuambia wanahabari kwamba unaweza kabisa kushambuliwa na vyombo vya habari na ukahimili kishindo na kuvuka salama. Kwa kifupi alikuwa anaeleza kwamba hanyimwi usingizi na vyombo vya habari.

Akiwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) alipata kusema pamoja na magazeti kumwandama sana kama mtu asiyefaa, lakini wakuu wake, akimaanisha mwenyekiti wa chama wakati huo, Rais Benjamin Mkapa, alimuoana anafaa ndiyo maana hakumbadili.

Dito aliamini kwamba habari za magazeti ni sawa na kelele za mlango zisizomzuia mwenye nyumba kulala usingizi wake! Lakini, baada ya uchaguzi mdogo wa jimboni Temeke mwaka 1996, kidogo kidogo mwanasiasa huyu ninayethubutu kumchukulia dhamana kwamba hakuwa na kinyongo, alitambua kwamba joto la vyombo vya habari si zuri sana.

Mwanasiasa mwingine mkongwe nchini, John Malecela, naye ni miongoni mwa wanasiasa wanaojua joto la magazeti. Akizungumza bungeni kwenye ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam mara baada ya Frederick Sumaye kuteuliwa kuwa waziri mkuu mwaka 1995, Malecela ambaye alipata kushika wadhifa huo kati ya 1990-1994 alithibitisha kwamba magazeti yanaathiri.

“Ndugu yangu Sumaye Dar es Salaam kuna joto, ukiacha joto la hali ya hewa kuna joto la magazeti, sasa ukiona joto hapa Dar es Salaam limezidi wewe nenda mikoani kwa wananchi huko utapata mapenzi ya kweli…” hii ilikuwa ni kauli ya Malecela akimuasa Sumaye.

Haya nimeyakumbuka baada ya kujioenea matukuio mawili makubwa ambayo yanashikamana. Haya yanahusu kampuni ya familia ya mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale Mwiru.

Kampuni hiyo, Smart Holdings, ilianza kuvuliwa nguo baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kufanya ziara katika kituo kikuu cha mabasi cha Ubungo.

Iligundulika kwamba kampuni hiyo iliyokuwa ikiendesha kituo hicho kwa maana ya kukusanya ushuru kwa niaba ya Jiji la Dar es Salaam, si tu ilikuwa inakosesha serikali mapato, bali mkataba wake ulikuwa wa ‘kifisadi’.

Baada ya Pinda kuelezwa mkataba huo ulivyokuwa wa ovyo, aliagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali akague kazi iliyokuwa inafanywa na kampuni ya familia ya Kingunge. Tunajua ripoti ilikwisha kukabidhiwa kwa Pinda ingawa mwenyewe hajaitoa hadharani kwa kile alichosema inafanyiwa kazi na makatibu wakuu wa TAMISEMI na ofisi yake.

Hata hivyo, makatibu hao wakifanya kazi hiyo, tayari kampuni ya Smart Holdings imetemeshwa kazi ya kukusanya mapato kituo kikuu cha mabasi Ubungo tangu tarehe 1 Novemba mwaka huu.

Lakini nini kilitokea, hakuna anayeweza kubisha kwamba vyombo vya habari vilifuatilia utendaji wa kampuni hiyo siku kwa siku na kueonyesha wazi kwamba kilichokuwa kinatokea Ubungo ni ufisadi wa mchana kweupe.

Kingunge mwanasiasa jabali la parapaganda, alishindwa kujinasua kwenye kashfa hiyo mbali tu ya kusema kampuni husika si yake ila ni ya familia yake.

Ngombale kama anavyofahamika na wengi, aliacha midomo wazi wabunge pale alipoeleza kuwa anatuhumiwa kwa makosa ambayo si yak wake; kati ya wakurugeni watatu wa kampuni wawili wanatoka katika familia yake. Mmoja ni mkewe na mwingine mwanawe.

Hata hivyo, utetezi wa Kingunge haukunusuru kampuni hiyo kutoswa kwani vyombo vya habari vilibainisha jinsi kituo cha Ubungo kilikuwa kimegeuzwa shamba la bibi.

Wakati Smart Holdings ikitimuliwa Ubungo ikaibukia kwenye jengo la Machinga Complex, habari zikaenea kwamba ilishinda zabuni ya kuendesha jengo hilo ikiwa ni pamoja na kukusanya ushuru.

Kwa kuwa magazeti kama ilivyo jukumu lake muhimu la kuwa mlinzi wa jamii, yakaeleza kwamba ile kampuni iliyotimuliwa Ubungo, imeula Machinga Complex. Umma ukapata taarifa na kujiuliza hivi ni lazima watu wenye mawaa wapewe kazi za umma.

Watu wakazidi kujiuliza kama falsafa ya Kaizari haifanyi kazi, kwamba tuhuma tu zinatosha kumwengua mtu kwenye nafasi yake, mbona hapa kwetu inapuuzwa. 

Wamachinga mwishoni mwa wiki wakacharuka na kusema katu, hawaitaki Smart Holdings kwenye jengo lao, mara habari zikavuja kwamba hata zabuni ya kuipa kampuni hiyo ilivyoendeshwa ilikuwa na walakini.

Sasa inaelezwa Smart Holdings haitakiwi kuonekana Ilala kwenye jengo la Machinga Complex.

Mfululizo huu wa matukio dhidi ya kampuni ya familia ya mkongwe Kingunge yanatoa fursa nyingine ya kupima kwa kina nguvu na maana ya vyombo vya habari katika jamii.

Kwa mara nyingine tena yanawasilisha ujumbe kwa watawala na wote wanaodhani kwamba kazi ya waandishi wa habari ni udaku ambao hauwanyimi usingizi; kwamba wataandika lakini hakuna litakalotokea.

Ningependa kuwahakikishia wale wote wanaoamini kwamba kelele za magazeti ni sawa na za mlango zisizomzuia mwenye nyumba kulala, kwa mfano huu mdogo wa mfululizo wa matukio dhidi ya kampuni ya familia ya Mzee Kingunge; watambue kwamba hata kama watajitia usugu na kupuuza haya yanayoandikwa leo, hata kama watajiona kwamba wapo salama kwa sababu labda watawala wa leo wamekataa kuchukua hatua, hakika hawako salama.

Salama yao ya leo ni ya kitambo kidogo tu, mwenye kuwashikilia usalama wao akiondoka, hakuna wa kuzuia nguvu za kisheria kuvuma na kuwatia wote pingu.

Ninatazama haya ya familia ya Kingunge katika mwakisio wa yatakayokuja kumpata  Benjamin Mkapa siku za usoni. Inawezakana wale wanaomlinda Mkapa sasa dhidi ya machafu yale wanafanya hivyo kwa kitambo kidogo sana , lakini salama yake ingekuwa ni kujitokeza kukabiliana na ukweli halisi wa mawaa yake.

Kadri nadharia ya Dito ilivyoshindwa, na kadri Malecela alivyoshauri kukimbia joto la magazeti ukiwa Dar es Salaam kwenda kuliwazwa na wananchi, na kwa mtiririko wa mwanasiasa mkongwe Kingunge kushindwa kuinusuru kampuni ya familia yake, ni ushahidi mwingine kwamba kazi ya kufichua maovu haitapotea bure. Hizi ndizo salamu zangu kwa wote wanaliokengeuka na kuacha uadilifu wangali wamekalia ofisi wa umma.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: