Kingunge amenywea ghafla


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 01 September 2009

Printer-friendly version
Kingunge Ngombale Mwiru

KINGUNGE Ngombale-Mwiru, mwanasiasa mkongwe, wiki iliyopita alifanya kitu ambacho alipaswa kukifanya siku nyingi zilizopita.

Ngombale alikuwa mwepesi kuliko ilivyo kawaida, kukwepa kujibu kauli ya Muadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, aliposema wazi kwamba, kamwe kanisa haliwezi kukaa na serikali, wala chama tawala, kujadili jinsi ya kuandika barua za kiuchungaji.

Kardinali Pengo alikuwa ametoa kauli hiyo wakati wa ibada ya mazishi ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza, Anthony Mayalla, aliyezikwa Agosti 26, mwaka huu.

Ngombale alikuwa mwanasiasa wa kwanza nchini kurusha kombora dhidi ya waraka huu, unaotoa elimu ya uraia kwa wananchi. Ni Ngombale aliyejitokeza hadharani mara mbili kuweka wazi msimamo wake.

Mara ya kwanza alifanya hivyo ndani ya Bunge, ambako aliliasa kanisa hilo kuuondoa waraka wake. Mara ya pili ni baada ya maaskofu wa Kanisa hilo kueleza wazi waraka huo usingeliondolewa kwa kuwa tu kuna watu hawautaki ijapokuwa hawajausoma.

Kingunge alijitokeza tena hadharani katika mkutano na waandishi wa habari, ambao alisisitiza kwamba ameusoma waraka huo na kuonya kwamba si mzuri kwa taifa.

Kardinali Pengo aliweka wazi msimamo wa kanisa, kwa kuzingatia kwamba Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, ilikuwa imeagiza serikali ikutane na viongozi wa dini kujadili waraka huo, ilikuwa ni kama kumwita Ngombale ajitokeze hadharani kueleza mwelekeo wake mpya baada ya kanisa kusema halina mpango wa kuondoa wala kuufuta waraka wake.

Kwa mshangao wa wengi, Ngombale mshauri wa zamani wa Rais Jakaya Kikwete, alijifanya kama vile hajasikia lolote.

Eti mazishi ambayo yalikuwa yanatangazwa moja kwa moja; ambayo hata rais Kikwete si tu kwamba alihudhuria, bali pia alitoa hotuba; na ambayo vyombo vyote vya habari vilitoa taarifa zake kwa mapana ya ajabu, Mzee Ngombale alisema, “Sikijui alichosema Kardinali Pengo.”

Kwamba, hakusoma wala kutazama televisheni yoyote. Kwa hiyo alisema hana la kusema (no comment).

Sisi wenye kimbelembele tukajua naam, Mzee wetu walau ameanza kuona mwanga. Kwamba suala la waraka ni kubwa kuliko alivyoliingia.

Sasa? Mzee wetu Kingunge ameamua kuepusha bawa lake! Ya nini kupigana na ukuta? Ya nini kujifanya profesa wa siasa wakati zama zimekupunga mkono? Ya nini kujibizana na maaskofu wasiomsikia profesa wa siasa?

Hapo ndipo Ngombale alipojifikisha. Ndipo alipofikia kwa sababu katika hali ya kawaida si jambo la kuingia akilini, kwamba kiongozi wa aina ya Ngombale asingeweza kusikiliza hotuba ya rais, tena wakati kuna jambo tete la waraka ambao unasumbua vichwa vya wasioutaka.

Kubwa zaidi, kwa ukaribu wake na rais ni jambo lisilowezekana kwa kiongozi wa namna hiyo kutofuatilia hotuba zake.

Lakini pia kama televisheni zote nchini ziliimba habari za mazishi hayo na magazeti karibu yote yaliandika habari za msiba huo, hivi tuseme Mzee huyu hasikilizi redio wala televisheni au hasomi magazeti?

Si tunaambiwa huyu ndiye alikuwa mstari wa mbele ndani ya NEC kumsulubu Spika wa Bunge, Samuel Sitta? Kwamba Sitta amekuwa refa mchezaji, kwamba ameijeruhi mno serikali na chama? Sasa mbona ameanguka kwa ghafla hivyo?

Kwa hakika, nilidhani mwenendo mpya na wa ghafla wa Mzee Kingunge alipaswa kuwa nao siku nyingi. Kitendo cha kusema hana cha kusema kuhusu kauli ya hivi karibuni, ya Kardinali Pengo, alipaswa kuwa nayo siku nyingi.

Alipaswa kuwa nayo siku ameanza kuuchokonoa waraka bila nguvu yoyote ya hoja ndani ya Bunge na kwa waandishi wa habari. Lakini zaidi sana, alipaswa kuwa nayo siku amejitwalia uendesha mashitaka dhidi ya Sitta, wakati akijua alikuwa na nafasi ya kuzungumza na Sitta ndani ya Bunge.

Ni kwa kutambua mwenendo mpya wa Kingunge, najikuta nikisema kweli Mzee wetu amenywea ghafla. Natamani kama angenywea mapema kabla ya hapo kwa kweli tungekuwa tumeepuka mambo mengi sana, ambayo yameumiza taifa hili, ikiwa ni pamoja na kutaka kauminisha wananchi kwamba eti nchi hii bado inajenga dola ya kijamaa. Kwamba, eti sasa ni ujamaa wa kumilikisha mwananchi mmoja mmoja nguvu za uchumi, wakati nchi imeachwa rehani mikononi mwa wageni, taifa likiachwa limepoteza mwelekeo.

Mzee Kingunge kama angepumzika na harakati za siasa za majukwaani, pengine angeacha kielelezo kwamba hata kwenye siasa watu wanastaafu. Muhimu zaidi ni kuepusha nchi na matatizo ya kushindwa kutambua kila zama zina vitabu vyake.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: