Kinyang’anyiro cha umeya


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 15 December 2010

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii
DK. Didas Masaburi

DK. Didas Masaburi, mbunge wa Baraza la diwani wa kata ya Kuvukoni, jijini Dar es Salaam, ambaye anabeba tuhuma za kufilisi mradi wa mabasi ya wanafunzi mkoani Dar es Salaam, amejitosa katika kinyang’anyiro cha umeya jijini.

Anapambana na wagombea wengine wawili, diwani wa kata ya Mchafukoge ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Dodoma Mjini, Hashim Sagaff na diwani wa Hananasif, Tarimba Abbas.

Hii ina maana kwamba iwapo atapitishwa na madiwani wa chama chake, ndoto ya wazazi na wanafunzi mkoni Dar es Salaam, kupata ufumbuzi wa tatizo la usafiri itakufa.

Wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanasema, hatua yeyote wa kumpitisha Masaburi kushika nafasi hiyo, “itasafisha njia ya chama chake kutokomea katika uchaguzi ujao.”

Tayari kinyang’anyiro hicho cha umeya kimeibua upya makundi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM); huku baadhi ya wagombea wakituhumiwa kutumia rushwa, udini na ukabila katika kutafuta ushindi.

Msimamizi wa uchaguzi katika kinyang’anyiro hicho, Kilumbe Ng’enda, naye ameingia katika tuhuma za kubeba mmoja wa wagombea wa nafasi hiyo.

Ng’enda ambaye ni katibu wa CCM mkoani Dar es Salaam, anatuhumiwa kumfanyia kampeni Dk. Masaburi na kujitangaza hadharani kufanya kazi hiyo.

Katika kinyang’anyiro hicho, mbali na kubebwa na Ng’enda, Masaburi anadaiwa kubebwa na baadhi ya watuhumiwa wakuu wa ufisadi nchini kwa kile wachambuzi wanaita, “Mkakati wa kuelekea 2015.”

Mchakato wa uchaguzi wa kutafuna mgombea nafasi ya umeya ndani ya CCM umepangwa kufanyika nchini kote leo, 15 Desemba 2010.

Aidha, chaguzi utakaowakutanisha wagombea watakaopitishwa na CCM na wa vyama vingine, umepangwa kufanyika 17 Desemba 2010.

Hata hivyo, Ng’enda amekana madai ya “kubeba” Masaburi. Anasema hana mgombea katika uchaguzi huo na kwamba kazi yake ni kusimamia uchaguzi tu, basi!

Anasema hadi sasa, hakuna mtu yeyote aliyemfuata na kutoa ushahidi unaoonyesha kuwa anafanyia kampeni Masaburi.

“Inawezekana nina mgombea. Hata ikiwa hivyo, hilo haliwezi kuwa kosa. Mimi ni mwanasiasa na ninawafahamu wagombea wote wanaoshiriki na inawezekana yupo ninayeona anafaa kuliko wengine,” anaeleza Ng’enda.

Alipoelezwa kwamba kuna ushahidi wa yeye kujitosa moja kwa moja kumfanyia kampeni Masaburi, Ng’enda alisema, “…Ninajua tatizo ni nini…”

Alisema, “Mimi ni mwenyekiti wa Sekretarieti ya chama mkoa wa Dar es Salaam na Tarimba ni Katibu wa kamati ya uchumi. Sasa tangu apewe kitengo hicho mwaka 2007 hajawahi kuleta hata mradi mmoja, hivyo ana wasiwasi kwamba mimi nitawaeleza wajumbe.”

Anasema, “Lakini mimi siwezi kusema hilo… Namwambia Tarimba aondoe wasiwasi na mimi, sitamwonea yeye wala mgombea mwingine yeyote,” alisisitiza.

Akiongea kwa njia ya mafumbo, Ng’enda anasema, “Hivi unadhani wafanyakazi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) hawana watu wanaowaunga mkono wakati za uchaguzi? Jambo la msingi hapa ni kufahamu, je wanaingiza mapenzi yao kwenye taratibu za uchaguzi?”

Alipoelezwa iwapo anafahamu kama mgombea anayempigia kampeni anakabiliwa na tuhuma za kuangamiza mradi wa mabasi ya wanafunzi, Ng’enda alisema, “Hayo tuwachie wapigakura.”

Naye, Tarimba alipotakiwa maoni yake, hasa kuhusu madai ya Kilumbe, kwamba hajabudi mradi wowote katika kipindi chake cha uongozi alisema, “Nimebuni miradi mingi na ushahidi upo kama mtu anataka kuuona.”

Hata hivyo, Tarimba alisema, hana matatizo na Ng’enda, bali anaamini kuwa hawezi kuwa msimamizi mzuri wa uchaguzi kwa vile anajulikana na kila mmoja kumpigia debe Masaburi.

“Mimi ni mtu mzima na ni mwanasheria. Kuna kitu kinaitwa conflict of interest (mgongano wa maslahi). Kwamba ni vigumu kwa mtu kuwa jaji wa jambo ambalo linakuhusu moja kwa moja,” ameeleza Tarimba kwa sauti ya upole.

“Sasa katika hali hiyo huyu mtu atawezaje kuaminika? Ni lazima Kilumbe ajitoe kusimamia uchaguzi huu,” anasisitiza.

Kinyang’anyiro cha kuwania umeya jijini Dar es Salaam kinakolezwa na ukweli kuwa makundi yanayowania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ndani ya CCM yamejitosa ili kupanga safu za uongozi.

Aidha, mvutano huo unatokana na mpango wa maendeleo wa jiji la Dar es Salaam, unaotarajiwa kutumia zaidi ya dola za Kimarekani 462 milioni (karibu Sh. 700 bilioni) katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

“Hili ndilo linazidisha ushindani, hasa kwa jiji la Dar es Salaam ambako kila diwani mashuhuri, na mwenye ushawishi, anakimbilia kugombea,” ameeleza mmoja wa madiwani wa zamani.

Diwani mmoja wa CCM ambaye amezungumza kwa sharti la kutotajwa jina amesema, “Kilumbe amewahi kutamka hadharani na mbele ya mashahidi kwamba yeye meya wake ni Masaburi. Ana mapenzi na Masaburi. Haya ameyasema kwa mdomo wake mwenyewe na mbele ya wanachama wa CCM, Ngalai na Adam Makulila.”

Amesema, “Huyu bwana, nilikuwa nimemuwekea mtego kwa kujua kuwa anamtaka Masaburi. Akasema mie mgombea wangu ni Masaburi.

“Mahali tulipokuwa kulikuwa na picha ya rais Kikwete na akaniambia kuwa katika hili, hata kama Kikwete angekuwa anawania umeya wa Dar es Salaam mimi ningempa kura yangu Masaburi,” anaeleza diwani huyo.

Kila mgombea miongoni mwa wagombea hao watatu wana nafasi ya kushinda.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: