Kiongozi aina ya Makamba ni janga la kisiasa


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 12 January 2011

Printer-friendly version
Tafakuri
Yusuf Makamba

UKIMSIKILIZA mtu anayeitwa Yusuf Makamba, katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), huwezi kukwepa kufikia hitimisho kwamba madaraka ndani ya chama tawala yamerahisishwa sana.

Kurahisishwa huko kunaelezwa kwa wazi kabisa na kauli na hata wakati mwingine matendo ya mtendaji wake mkuu, Makamba.

Ni jambo la bahati mbaya kwamba siasa nchini kwa muda mrefu sana ziliachwa mikononi mwa watu walioshindwa kufanya mambo mengine ya maana katika jamii.

Yaani siasa iliachwa kwa wabaingaizaji, watu wasiokuwa na elimu, wapiga domo na kwa hakika watu walioacha siku nyingi kutumia vichwa vyao zaidi ya mambo ambayo aghalabu hutendeka bila hata kujua.

Kwa mfano kunyanyua mguu kupiga hatua hakuna kufikiri kwa maana halisi, ni kitendo cha kawaida mno. Kunyanya tonge la ugali kutoka kwenye bakuli na kulichovya au kutowea kwenye mboga na kulipeleka mdomoni hakika hakuna akili yoyote ya maana inayotumika hapo.

Hakika si matusi kusema kwamba wanasiasa wengi wa nchi hii, hasa ambao wamejikuta wamepanda ndani ya chama tawala hadi kukabidhiwa madaraka makubwa ni watu wa aina hii, yaani hutumia akili zao kwa kiwango kidogo sana.

Wameacha bongo zikaota kutu kwa kuwa hawazisumbui, hawazifikirishi. Hata utendaji kazi wao unaakisi udhaifu huo.

Kielelezo cha akili iliyojaa kutu, na kuendesha mambo kwa mizaha mikubwa hata kama katika mambo nyeti, si mwingine. Ni Makamba.

Jumatano iliyopita, taifa lilitiwa doa baya sana na Jeshi la Polisi. Mkoani Arusha polisi waliua raia wasiokuwa na hatia ambao walikuwa wanatumia haki yao ya kikataiba kushiriki mkutano wa hadhara na kuandamana.

Wengine wameishia kujeruhiwa pamoja na madhara mengine yaliyosababishwa na risasi za moto na mabomu ya machozi. Ulikuwa ni ukiukaji wa wazi wa haki za binadamu.

Tukio hili linafanana kwa karibu sana na tukio kama hilo lililotokea visiwani Zanzibar, 26 na 27 Januari 2001. Makumi ya waandamanaji waliuawa na polisi wenye silaha za moto. Kisa ni mambo ya uchaguzi kama haya haya ya Arusha.

Huku taifa likiwa kwenye simanzi, Makamba akijua dhahiri hisia za wananchi katika kipindi hiki, ameibuka na kutoa kauli iliyoonyesha jinsi ambavyo ubongo wake alikwisha kuuweka stoo siku nyingi.

Makamba anaishi kwa mazoea tu, hana sababu ya kufikiri kabla ya kuzungumza na wala hajali madhara ya kauli zake kwa kuwa hata hajui nguvu, unyeti na nafasi ya kiti cha katibu mkuu wa chama tawala.

Ni kwa maana hiyo, Makamba ameamua kulumbana na Maaskofu. Anaamini kauli ya maaskofu kulaani mauaji ya Arusha ni kuingilia siasa.

Maaskofu hao pia waliitaka serikali kuchukua hatua za haraka kutatua tatizo ambalo chimbuko lake ni misuguano ya vyama viwili vya siasa katika Jiji la Arusha - CCM na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Vyama hivyo vinasuguana juu ya uchaguzi wa Meya wa Jiji la Arusha, ambao kila mwenye akili timamua anaju kuwa CCM imecheza faulu.

Makamba anajua fika kwamba chama chake kule Arusha kilicheza faulo, na hakika anajua kwamba amani inapotoweka mahali popote, si kazi ya wanasiasa tu kutafuta njia za kuirejesha, hasa inapokuwa maisha ya watu yamepotea.

Kwa akili ya Makamba anadhani kwamba suala la amani ya nchi ni hati miliki ya chama chake, lakini kibaya zaidi kwa akili ya kiongozi huyo pia anadhani kwamba kwa kuwa waliopigwa mabomu na risasi ni wananchi waliokuwa wamejitokeza kushiriki mkutano wa hadhara na maandamano ya CHADEMA, basi CCM ina kila sababu ya kuchekelea!

Ndiyo! Makamba kwa fikra zake nyepesi anaamini CCM imenufaika kwa kupigwa mabomu viongozi, wanachama na wapenzi wa CHADEMA.

Anashindwa kujua wananchi sasa wanafahamu kwamba CCM na serikali yake wameshindwa kuongoza kwa kutumia njia za kistaarabu za kushawishi; ndiyo maana sasa mbinu za manguvu zinatumika kana kwamba chama hicho ni chama cha kijeshi ambacho kumeunda serikali ya kijeshi na si iliyotokana na ridhaa ya wananchi.  

Wengi walitarajia kuwa Makamba angekuwa amejichimbia mkoani Arusha akizungumza na wafuasi wake, akionana na viongozi wa mkoa huo, wakiwamo wabunge, madiwani na wengine wote ambao walihusika kwenye mchezo mchafu wa kuchakachua umeya, ili kujenga heshima ambayo chama chake ilikuwa huko nyuma.

Lakini wapi! Makamba yuko Dar es Salaam akiendesha malumbano na Maaskofu. Tena kauli yake inaelekea kukinzana na ya mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete. Kila wakati Makamba amekuwa ni tatizo ndani ya CCM, hana lolote la maana analoweza kujigamba nalo kwamba uongozi wake umetekeleza.

Kiongozi huyu ametajwa mara kadhaa kuhusika kupalilia makundi ndani ya chama chake; amehusika katika kashfa mbaya ya kubariki mbinu chafu za kukomoa wanachama wenzake aghalabu kwa maslahi yake binafsi.

Mbaya zaidi, Makamba ni katibu mkuu karani. Hana sifa ya kuwa na jambo lolote la maana analoweza kusimama hadharani aseme, “nilibuni hili na mafanikio yake kwenye chama ni haya.”

Makamba ni katibu mkuu wa CCM kwa sababu tu ana bahati ya mtende. Hana elimu yoyote inayoweza kuhalalisha kukalia kiti hicho hasa katika zama za sasa ambazo changamoto zinazokabili taifa na hasa chama tawala zinahitaji vichwa vilivyotulia, upeo mkubwa na uwezo wa kupambanua mambo kwa nia mbili.

Moja ni kujenga utulivu na umoja wa kitaifa bila kujali itikadi za vyama, mbili ni kusaidia CCM kuwa chama cha kisasa zaidi kinachotambua nafasi yake kama chama tawala ndani ya taifa lenye rasilimali nyingi, lakini watu wake ni masikini wa kutupwa.

 Unapomtazama Makamba na kauli zake kama hizi za juzi dhidi ya maaskofu, hakika unafikia hitimisho kwamba hajitambui na hajui changamoto za taifa letu kwa wakati huu ni zipi.

Ndiyo maana kwake mauji ya raia wasio na hatia si jambo la kumfikirisha. Si uchimvi au kumuonea Makamba; ni jambo la bahati mbaya kwa CCM kuwa na katibu mkuu wa aina yake hasa katika zama hizi.

0
Your rating: None Average: 1 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: