Kipawa mbioni kuburuza serikali mahakamani


Editha Majura's picture

Na Editha Majura - Imechapwa 06 October 2009

Printer-friendly version
Uwanja wa ndege wa Julius Nyerere na maeneo yanayouzunguka

MPANGO wa kuishitaki serikali katika mgogoro wake na wakazi wa Kipawa, mjini Dar es Salaam kuhusiana na uamuzi wa kuwahamisha juu ya kupisha upanuzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, tayari umeiva.

Mgogoro huo unahusisha serikali na wamiliki wa nyumba 153 waliozuiwa eneo hilo tangu mwaka 1997 ili kuendeleza makazi yao.

Taarifa zinasema tayari mipango ya kuiburuza serikali mahakamani imeiva; wakati wowote kuanzia sasa serikali itakabidhiwa hati ya kusudio la kushitakiwa.

Hatua hiyo imefuatia kutopatikana maelewano kati ya pande hizo mbili licha ya jitihada zilizofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, William Lukuvi na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Evance Balama.

Viongozi hao wamekuwa wakitetea msimamo wa serikali kwamba italipa wakazi hao fidia kulingana na sheria ya zamani ya ardhi ya mwaka 1967 badala ya sheria mpya ya mwaka 1999.

Wakazi wa Kipawa pamoja na Kipunguni na Kigilagila wamesimamia hoja kuwa hadi sasa serikali imeshindwa kuwapatia wakazi hao muhtasari wa mkutano ulioazimia kuwa fidia italipwa kwa kufuata sheria ya mwaka 1999.

Serikali imekuwa ikidai kuwa azimio hilo lilitangazwa katika mkutano wa wahusika wote uliofanyika 10 Septemba mwaka huu na kushuhudiwa na waandishi wa habari na wawakilishi wa Wizara ya Miundombinu, Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, Polisi Mkoa wa Ilala, Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAAA), Kampuni ya uthamini ya Tanvaluers & Property Consultancy.

Ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pekee ambayo haikutuma mwakilishi wake katika mkutano huo uliokuwa chini ya uenyekiti wa Afisa Ardhi Mwandamizi wa Mkoa, Edger Japhet. Inaelezwa kuwa Japhet alisema uamuzi huo ulitokana na maelekezo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

“Sikiliza, unajua wakati serikali inashikilia kutumia sheria ya zamani ya mwaka 1967, imegoma kutupatia waraka wanaodai umetolewa kwa ushauri wa mwanasheria mkuu wa serikali,” alisema mmoja wa wanakamati wa wakazi hao.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Magnus Mulisa, ameiambia MwanaHALISI kwamba utaratibu wa kuishitaki serikali unakwenda vizuri.

“Ndani ya wiki hii tutawapelekea hati ya kusudio la kufungua kesi mahakamani, siku 90 baada ya hatua hiyo tutafungua kesi. Endapo watataka kufanya lolote, hatutasita kuomba zuio la kisheria,” amesema.

Kulikuwa na taarifa kwamba wakazi hao na serikali wameafikiana kuhusu njia ya kumaliza mvutano baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuingilia kati na kuagiza uongozi wa mkoa kulipa fidia kufuatana na sheria zote mbili.

Kwamba Waziri Mkuu ameagiza sheria ya mwaka 1967 izingatiwe kutokana na tathmini ya thamani ya mali iliyofanywa mwaka 1997 hadi 2000 inayoelekeza kuzidisha mara miaka mitatu na kuongezwa kiwango stahili kwa upungufu uliotokea wa asilimia sita.

Imeelezwa kuwa alichoahidi waziri mkuu Pinda ni kuzingatia misingi ya sheria mpya ya ardhi kuanzia mwaka 2000 hadi siku malipo yatakapofanyika.

Lakini Lukuvi na Balama wanakana kupokea maelekezo hayo na kwamba kinachofanyika ni kwa mamlaka husika katika wizara ya Fedha na Uchumi kuendelea na utaratibu wa kuandaa hundi za malipo ya fidia kwa kuzingatia sheria ya mwaka 1967.

Taarifa zilizopatikana juzi Jumatatu, zilieleza kuwa wamiliki wa nyumba 1,009 kati ya 1,053 wamejiorodhesha na kusaini orodha hiyo kama hatua mojawapo ya kuthibitisha kuendeleza utaratibu wa kuishitaki serikali badala ya kupokea hundi zinazoandaliwa.

Wananchi hao wamekuwa wakilalamika kuwa sheria ya ardhi ya mwaka 1967 imepitwa na wakati na itasababisha walipwe fidia ndogo.

Mpango wa kuhamishwa kwa wakazi hao umekwama kwa miaka 12 sasa kwa ukosefu wa fedha, tatizo ambalo serikali inasema imelitatua kama alivyonukuliwa akisema Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, John Chiligati bungeni.

Waziri Chiligati aliarifu kuwa serikali imetenga Sh. 30 bilioni lakini kuna taarifa kuwa iwapo malipo ya fidia yatazingatia sheria ya zamani, itagharimu Sh. 18 bilioni tu. Hiyo inajenga hisia kuwa wajanja wamepanga kujinufaisha.

Kuna shaka katika mpango wa serikali kushikilia kutaka kulipa fidia kwa kuzingatia tathmini ya 1997 kuzingatia sheria ya 1967 lakini malipo yazingatie sheria ya 1999 kama ilivyoshauriwa kitaalamu Julai mwaka huu, huenda ni mtego kwa vile laiti kama serikali ilijua hilo, isingeinga gharama kwa kulipa watathmini ili wafanye tathmini zaidi mwaka 1997 katika makundi mawili yanayozingatia sheria tofauti.

0
No votes yet