Kisasa ameandika asichokiamini


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 06 October 2010

Printer-friendly version

TOLEO lililopita la gazeti hili, lilibeba makala ukurasa huu iliyosema, ‘“Hatujakomaa’ kwa midahalo ya kisiasa.”  Makala ile iliandikwa na mmoja wa watu waliokulia na kulelewa katika mfumo wa chama kimoja; kufanya kazi katika chombo cha propaganda cha CCM, lakini waliokosa nyenzo muhimu za kuchambulia maisha na mazingira yao.

Mwandishi huyo ni Lucas Kisasa, meneja utawala wa magazeti yanayomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi ya Uhuru, Mzalendo na Burudani.

Mwaka 1995

Kwa kadri ninavyomfahamu Kisasa, si msahaulifu hata kidogo. Yeye ni miongoni mwa waandishi wenye kumbukumbu kubwa ila anasumbuliwa na kazi ya propaganda. Hivyo aliandika makala ambayo hata yeye haamini.

Mwaka 1995, kwa mara ya kwanza, ulifanyika mdahalo wa kihistoria ulioshirikisha wagombea urais kwenye Hoteli ya Kilimanjaro. Mdahalo uliandaliwa na jopo lililokuwa chini ya aliyekuwa Mhariri wa Business Times, Bernard Palela.

Washiriki walikuwa Benjamin Mkapa (CCM), John Cheyo wa United Democratic Party (UDP), Augustine Mrema (NCCR-Mageuzi), na Prof. Ibrahim Lipumba wa Chama cha Wananchi (CUF).

Kura za maoni zilizokuwa zinapigwa na wasomaji wa gazeti la Majira, zilionyesha Mrema alikuwa juu, wengi waliipa nafasi NCCR ya Mrema kuibuka na ushindi wa kishindo.

Lakini ni katika mdahalo ule, Mkapa alionyesha tofauti na ukomavu wa kifikra, huku Mrema aliyekuwa anapewa nafasi kubwa, akiwaangusha wafuasi wake kwa kujadili mambo rejareja badala ya kueleza atakachokifanya. Alionekana hana sera.

Kama mwaka 1995 CCM ilishiriki mdahalo, tena kwa mara ya kwanza, na ikafanya vizuri, inakuwaje Kisasa anaibuka, miaka 15 baadaye na kudai Watanzania hawajakomaa kwa midahalo ya kisiasa?

Labda anataka kukiri CCM hawajakomaa kwa midahalo ya kisiasa. Hata hilo linatiliwa shaka, kwani viongozi wake wanashiriki vipi makongamano ya kimataifa nje ya nchi?

Kama hivyo ndivyo, basi Kisasa anaungana na Watanzania wengine wanaosema CCM hawafai kuchaguliwa.

Uongo mbaya, mwaka 2005 Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) liliendesha mdahalo juu ya mwelekeo wa uchumi wa nchi. Walioshiriki walikuwa Waziri wa Mipango na Uchumi, Dk. Juma Ngasongwa (CCM), Mrema (TLP), Lipumba (CUF) na Cheyo (UDP). Wote wanasiasa.

Katika mdahalo ule ulioendeshwa na Mkenya, Joseph Warungu wa BBC, Dk. Ngasongwa alijitahidi kueleza kwa upeo mpana utekelezaji wa sera ya uchumi ya serikali. Cheyo na Prof. Lipumba walitia fora kufafanua masuala kadhaa ya kiuchumi, lakini ni Mrema aliyefunika kwa kuchekesha watu alipoibua hoja ya mgodi wa Bulyanhulu kumpa Mkapa zawadi ya “tofali la dhahabu.”

Mrema ndiye alitawala vichwa vya habari vya magazeti kuhusiana na tuzo ile. Serikali ilijitafuna na wiki moja baadaye ililazimika kujibu kwamba dhahabu ile ipo na ni mali ya taifa.

Kisasa hajui au hakumbuki? Kama anakumbuka inatoka wapi hoja kwamba ‘hatujakomaa’ kwa midahalo ya kisiasa? Anapata wapi ujasiri wa kudai kwamba ni jambo geni?

Hoja mfilisi

Mwandishi amerukia jambo jingine kuhusu ushiriki wa Salma Kikwete katika kampeni. Anasema lipo tatizo kubwa la uelewa wa watu juu ya dhana nzima ya midahalo ya kisiasa.

Kwa taarifa yake, hakuna hata mtu mmoja anayepinga Salma Kikwete kumpigia kampeni mumewe na wala hiyo haiwezi kuwa hoja. Kinacholalamikiwa hapa na ambacho Kisasa anajua bali anataka kufunika, ni mama huyo kutumia raslimali za umma kwa kampeni za mumewe. Wana CCM wenyewe wanalalamikia familia ya Kikwete kuteka kampeni; hilo kwangu si hoja.

Upo ushahidi kwamba anatumia magari ya serikali (ya wakuu wa mikoa na wilaya yakiwa yamebandikwa namba bandia); anatumia ndege ya serikali na hati za malipo zimeonyesha kuwepo kwa utata mkubwa.

Meneja kampeni Abdulrahman Kinana katika majibu yake, alidai Salma anatumia fedha za chama, lakini Mtendaji mkuu, Yussuf Makamba alidai anatumia asasi yake ya Wanawake na Maendeleo (WAMA). Heri majibu ya Kinana, majibu ya Makamba yanaibua hoja ya ukiukwaji sheria.

Kisasa anajua sheria za usajili wa asasi za kiraia kwamba  WAMA haipaswi kujihusisha na masuala ya kisiasa.

Sheria inayoizuia WAMA ni ileile iliyotumiwa na serikali ya CCM ilipochachamalia asasi ya HakiElimu ikidai inajiingiza katika masuala ya kisiasa, ikazuiwa kufanya kazi na baadaye viongozi wake kuitwa ofisi ya waziri mkuu, Dodoma na kusulubiwa kwa madai ya kuingiza siasa katika utendaji wake.

Kama Makamba anathibitisha hivyo kwamba Salma anatumia WAMA, huo ni ukiukwaji wa sheria na hicho ndicho kinalalamikiwa.

Umaskini

Kisasa amegusia suala jingine la umaskini wa kipato cha Watanzania akisema idadi kubwa ya Watanzania vijijini hawana uwezo wa kununua magazeti na hawana redio wala televisheni hivyo wasingenufaika na mdahalo.

Ni kweli? Lakini ajiulize ulipofanyika mdahalo mwaka 1995 Watanzania walikuwa na televisheni na redio nyingi kuliko mwaka 2010?

Hivi nusu karne baada ya uhuru, redio bado ni tatizo vijijini? Kwa hiyo, Rais Jakaya Kikwete anapozungumza na wananchi kwa njia ya televisheni na redio anapoteza muda? Nadhani Kikwete hakusoma makala ya Kisasa. Asingeipenda.

Huu ni upotoshaji mkubwa. Hivi leo kuna redio za FM na vituo vya televisheni vingi vinavyomilikiwa na halmashauri, mashirika ya dini na watu binafsi. Ndiyo maana nimesema Kisasa ameandika kitu asichokiamini.

Kama kada huyu wa CCM anaamini anachoandika, basi hayo anayotetea ndizo sababu hasa za kuiondoa CCM madarakani; kwamba imeshindwa kuwajengea wananchi wake uwezo wa kipato.

Je, CCM itaweza miaka mitano ijayo? Haiwezi, ndiyo maana mwandishi anakiri mwenyewe aliposema, “CCM inaweza kuwa na mapungufu yake. Lakini ni chama kipi ambacho hakina mapungufu?”

Kwa swali hilo, kada huyu wa CCM anataka wananchi wavumilie shida, wizi, rushwa, ufisadi na uchumia tumbo wa serikali ya CCM kwa vile hata vyama vingine vina mapungufu?

Ukweli ni kwamba kilichowakimbiza CCM na Kikwete kwenye mdahalo ni ukosefu wa uadilifu katika usimamiaji wa raslimali za umma, upungufu wa maarifa na kutojiamini.

Mwisho, magazeti hayachagui viongozi, yanachambua sifa za wagombea – udhaifu, uwezo, umakini, upeo wao na kuwaachia wapigakura. MwanaHALISI linafanya kazi hiyo kwa uadilifu mkubwa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: