Kisumo: Shumhuna hayuko pekee yake


Amosi Zakaria's picture

Na Amosi Zakaria - Imechapwa 29 July 2008

Printer-friendly version

Siddartha Gauthama, mwasisi wa madhehebu ya Buddha (miaka zaidi ya 500 Kabla ya Kristo) alitamka; "Usiishi katika nyakati zilizopita, wala usijihangaishe kuota yaliyopita, bali uelekeze akili yako katika mambo yaliyopo."

Tafakuri ya maneno haya ya Gautama imenijia ghafla baada ya kufuatilia kwa muda mzozo wa sasa wa kisiasa katika suala la nafasi ya Zanzibar katika Muungano.

Lipo kundi la Watanzania, wakiongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, linalosisitiza kuwa Zanzibar si nchi. Hoja hapa ni kwamba nchi ni moja tu - Tanzania.

Hivyo, Zanzibar ni sehemu ya Muungano, hivyo ni sehemu ya nchi. Kundi la pili linaongozwa na Naibu Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Ali Shamhuna, likidai kwamba iwe iwavyo, Zanzibar ni nchi. Ina katiba yake, Rais wake, Baraza la Wawakilishi (Bunge), ina wimbo wake na bendera yake.

Mvutano na mjadala huu si mpya, bali umekuwapo miaka mingi iliyopita, na umekuwa ukiendelezwa chini chini, hasa baada ya kushindikana kwa hoja ya Zanzibar kujiunga katika Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (IOC) ikifuatiwa na hoja ya kufufua serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano, mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Nguvu pekee iliyozima hoja hizi kitaifa ni ushawishi mkubwa wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Kwa wakati huo, Mwalimu Nyerere aliwashangaa wana CCM kuanzisha hoja za kuigawa na kuiua Tanzania huku wakijua kuwa si sera ya chama chao. Aliwaeleza kuwa kama sera hiyo ingekuwa inashabikiwa na wapinzani, lisingekuwa tatizo kwake, maana ni sera mbadala.

Fimbo yake kwa waliokuwa wanataka kuiendeleza hoja hiyo wakiwa ndani ya CCM ilikuwa moja: "Ondokeni kwenye chama, mjenge hoja mkiwa nje ya CCM, maana hii si sera yetu."

Wakanywea, wakaachaa nayo si kwa kukerwa nayo bali kwa kulinda maslahi yao ndani ya CCM. Lakini upinzani umekuwa ukiifufua hoja hii kwa maelezo mbalimbali, na kimsingi, karibu vyama vyote vya upinzani vinaungana katika sera kwamba Muungano unaofaa ni wa serikali tatu: Tanganyika, Zanzibar na Muungano.

Tume kadhaa za rais, ikiwamo iliyoongozwa na Jaji Robert Kisanga kuhusu muungano ilipendekeza juu ya umuhimu wa serikali tatu. Serikali ilipuuza ushauri huo, lakini haikujibu hoja.

Mvuto wa suala hili kwa Wazazibari uko wazi. Linapojadiliwa suala la hadhi ya Zanzibar ndani ya Muungano, Wazanzibari hawaendekezi tena itikadi za vyama.

Wanakubaliana kwamba Zanzibar ni nchi inayostahili kusimama peke yake, na Tanganyika ikitaka isimame peke yake, ndani ya Muungano.

Kinachoshangazwa ni kwamba watawala wameziba masikio. Hawasikii kauli za Wazanzibari wala za wataalamu wengine wa msauala ya kikatiba. wanachong'ang'ania wao (watawala) ni kauli za vitisho kwamba wanaopinga muundo wa sasa wa Muungano wanataka kuua Muungano.

Wamesema wengi, lakini katika siku za hivi karibuni amejitokeza mmoja wa waasisi wa CCM, Mzee Peter Kisumo, akatoa kauli kali dhidi ya kina Shamhuna na wenzake.

Alisema: "Kama Wazanzibari wanadai Zanzibar iwe nchi, wasiliseme kwa soni wala wasimbane Pinda. Shamhuna kama Shamhuna hatoshi kuitoa Zanzibar kwenye Muungano uliodumu kwa zaidi ya miaka 40."

Lakini hakuna popote ambapo Shamhuna alisema anataka Zanzibar ijitoe kwenye Muungano. Shamhuna na wenzake kama yeye, wanachosema ni kwamba Zanzibar ni nchi. Iliungana na nchi nyingine (Tanganyika) kuunda Jamhuri ya Muungano.

Muungano haukuua nchi, bali uliziunganisha kuunda jamhuri. Kinachogomba hapa ni muundo wa Muungano na tafsiri ya neno nchi.

Binafsi nawaona akina Shamhuna kama wana CCM walioongoka na sasa wanaona kwa mtazamo mpya. Chama chao kinapaswa kuwasikiliza na kuweka mazingira ya kuingiza hoja za Wazanzibari katika uboreshaji wa muundo wa Muungano.

Kisumo anapotosha Watanzania anaposema kwamba wanaojadili suala hili wana lengo la kuvunja Muungano.Katka umri alionao, Mzee Kisumo anapaswa kuwa amejifunza mengi katika historia, kwamba si lazima muundo wa Muungano wa leo ubaki kama ulivyokuwa wakati unaundwa mwaka 1964.

Kama mahitaji ya wakati ule yalihitaji tuwe na serikali mbili si lazima mahitaji ya sasa yabaki hivyo.

Akumbuke pia kwamba wakati Tanganyika ilipoteza hadhi ya kuwa serikali ndani ya Muungano, Zanzibar ilibaki na nafasi yake; na hata Mwalimu Nyerere alilizungumzia hilo akisema kwamba kwa mtazamo wao wakati huo, alikataa kuunda nchi moja ili kuepuka hisia za ubeberu (kwamba ameifuta na kuimeza Zanzibar).

Akasema ilikuwa zaidi kwake kuifuta Tanganyika kwa sababu, kutokana na ukubwa wa sehemu moja, ingekuwa vigumu kwa Zanzibar kuimeza Tanganyika.

Na mtu anayechunguza mjadala huu unavyoendelea sasa, lazima ajue kuwa Shamhuna hasemi hayo anayoyasema kama mtu binafsi. Anakisemea kikundi cha walio madarakani Zanzibar. Ni kikundi kinachotaka kuiona Zanzibar ikiwa na mamlaka zaidi katika masuala yanayoihusu. Ni kikundi kinachotamani kuona rais wa Zanzibar akiwa rasi kweli kweli.

Ni vema akina Kisumo na wahafidhina wengine ndani ya CCM wajue kuwa mjadala huu hauwezi kufa kwa kutishana na kukemeana. Unahitaji kujengewa hoja. Hoja itakayoshinda ndiyo ipewe nafasi.

Lakini kwa mtu yeyote anayetazama vema mahitaji ya Tanzania kisiasa na kijamii, mjadala huu umekuja wakati mwafaka. Kina Mzee Kisumo hawapaswi kuogopa mabadiliko; wala wasidhani kwamba hsitoria yao itafutwa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: