Kitabu kimoja hakikuzi maarifa


editor's picture

Na editor - Imechapwa 10 February 2010

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

SERIKALI sasa inatamani ujinga. Inataka kunyonga waandishi na wachapishaji wa vitabu nchini huku ikiporomosha zaidi kiwango cha ufahamu kwa watoto nchini.

Msimamo wake wa kutaka kutumika kwa kitabu kimoja tu kufundishia shuleni, unaashiria kufuta matumaini ya Watanzania ya kukua kiakili kwa kupata maarifa kutoka vyanzo mbalimbali.

Hivi mwalimu anayefundisha kwa kutumia kitabu kimoja tu kilichoruhusiwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, ananufaika nini kielimu na vipi anamnufaisha mwanafunzi?

Je, ni mwalimu yupi aliyesheheni maarifa, kati ya yule anayeandaa somo lake kwa kutumia kitabu kimoja na yule anayeandaa somo kwa kutumia vitabu viwili au vingi?

Ni dhahiri mwalimu aliyeandaa somo kwa kutumia vitabu vingi atakuwa amepata maarifa zaidi na kwa njia mbalimbali.

Hapa basi, upungufu uliopo kwenye kitabu kimoja unaondolewa na maarifa yanayopatikana kwenye kitabu kingine. Hapa tunakuwa na maarifa maridhawa.

Tatizo la kitabu kimoja halikomei kwa wanafunzi na walimu. Linahusu pia waandishi wa vitabu nchini na wachapishaji.

Wingi wa waandishi na wingi wa wachapishaji wa ndani vina maana ya wingi wa vyanzo vya maarifa.

Hapa kuna wingi pia wa mafao kwa wachapishaji binafsi ambao serikali haijaonyesha kusaidia ili kukabiliana na gharama za karatasi na nyenzo nyingine katika kuelimisha taifa.

Lakini woga mkuu uko kwenye kitabu kimoja kuongoza serikali katika ubia na makampuni makubwa, tena ya nje, ya uchapishaji vitabu.

Tunaona hatari ya wakubwa kutaka kuvuta mapato haramu kutoka kwa makampuni makubwa kama ushawishi ili wapitishe vitabu vyao.

Hili litaleta maangamizi ya waandishi na wachapishaji vitabu wazalendo. Hatupingi kuwepo vitabu vya wachapishaji wa nje, lakini elimu ni kukusanya maarifa na maarifa hayawezi kupatikana katika kichwa kimoja, kitabu kimoja.

Tunahimiza serikali kuwa na mjadala na waelimishaji, wataalam wa mitaala, waandishi na wachapishaji wa vitabu wazalendo juu ya kile inachotaka kutekeleza.

Tuna uhakika kuwa matokeo ya mjadala huo yatakuwa utambuzi kuwa vyanzo vingi vya maarifa ndiyo suluhisho na njia pekee ya kukuza tasnia ya uchapishaji nchini; ambao pia unakuza umahiri wa uandishi katika nyanja mbalimbali.

0
No votes yet