Kitanzi cha waendao na watokao Kigamboni


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 04 January 2012

Printer-friendly version
Uchambuzi

John POMBE Magufuli amewaambia wananchi wanaotumia vivuko vya serikali kwenye mkono wa Bahari ya Hindi, kutoka na kuingia Kigamboni jijini Dar es Salaam, wameze “dawa chungu.”

Ametangaza uamuzi wa serikali wa kuongeza nauli kutoka Sh. 100 hadi Sh. 200. Ametoa sababu: Ni nauli ya zamani. Gharama za uendeshaji zimepanda.

Bei ya mafuta imepanda. Wafanyakazi wameongezeka…mengi.

Anasema wasioweza au wasiotaka kulipa Sh. 200 watumie barabara. Wazunguke: Kigamboni, Kongowe, Mbagala na kuingia Dar es Salaam.

Wanaotaka kwenda Kigamboni, nao kama hawataki au hawawezi kulipa Sh. 200, wazunguke: Kutoka walipo jijini, Mbagala, Kongowe hadi Kigamboni.

Hilo ni pendekezo moja. Pendekezo la pili alilotoa, kwa mujibu wa mitandao ya taarifa, ni kwa asiyeweza kulipa, “kupiga mbizi” kutoka kingo moja hadi nyingine.

Hili laweza kuonekana kuwa kejeli au mzaha. Wengine wanaweza kusema ni dharau. Lakini alichofanya Magufuli na serikali yake kina maelezo zaidi ya hayo.

Kesho wenye mabasi watatumia sababu hizohizo kupandisha nauli. Kwani wameongeza watumishi. Bei ya mafuta imepanda. Gharama za uendeshaji kwa jumla zimeongezeka.

Nani atabisha? Wenye daladala wakigoma serikali itafanya nini? Itawapiga mabomu ya machozi? Itawafutia leseni? Itawalaumu na kuwaita “wahujumu?” Itafanya nini?

Hivi haiwezekani kwamba Magufuli amefungua njia ya wengine kuongeza bei kwa sababu hizohizo? Tusubiri kesho. Tutasikia.

Hilo ni moja. La pili ni kejeli ya kushindwa kulipa Sh. 200 lakini ukawa na uwezo wa kulipa Sh. 800 hadi 1,200 kwa njia moja – kwa kutoka au kuingia mjini. Halafu kuna la tatu, lile la kejeli ya kupiga mbizi.

Hapa kuna jedwali linaloonyesha gharama za usafiri wa binafsi na gharama za usafirishaji vifaa, mizigo, baisikeli, pikipiki na hata magari.

Mhariri anatoa fursa kwa wananchi kujadili suala la nyongeza ya nauli kwa wasafirio kwa vivuko Dar es Salaam. Ni wakati wako kutoa maoni kwa njia ya makala au baruapepe au simu (sms).

Angalizo: Vivuko vinapata kiasi gani kila siku? Ule “wizi mkubwa” uliowahi kutajwa kuhusiana na mapato ya vivuko, bado upo? Je, ni wakati mzuri kuongeza nauli?

Hivi karibuni serikali iliagiza matumizi ya asilimia 50 tu katika maeneo mbalimbali ambako tayari kulikuwa na bajeti kamili iliyopitishwa na bunge.

Je, nyongeza ya nauli yaweza kuwa njia ya kuziba pengo? Tujadili.

0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: