Kiti cha spika kimezidi wanaokikalia?


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 18 July 2012

Printer-friendly version

KITI cha spika kinaweza kuwa ni kikubwa “mno” kuliko uwezo wa waliopo kukikalia iwapo wahusika hawa hawatakuwa wanapima athari za maamuzi yao kuhusu miongozo ya wabunge.

Nimebaini hili pale Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai aliporidhia matakwa ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alipotoa muongozo wakati wa mjadala wa makadirio ya matumizi ya bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi bungeni.

Lukuvi ambaye sasa moja ya mikakati yake bungeni imejidhihirisha kuwa ni kukwamisha mtiririko wa hoja nzito za wabunge wa kambi rasmi ya upinzani ili kuzuia anachoona kinaumiza taswira ya serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupitia njia ya kuomba muongozo, aliingia kwa staili ya kutaka kutoa indhari juu ya kauli alizoita za uchochezi zilizotolewa na baadhi ya wabunge hao.

Alisimama baada ya kushuhudia lawama na shutuma kali dhidi ya watendaji wa serikali na vyombo vyake vya kusimamia ulinzi, usalama na sheria.

Wabunge wengi wakati huo walikuwa wameapa kuwa watawaachia wananchi kwenye majimbo yao kuchukua hatua wenyewe za kudhibiti uporaji au utwaaji wa ardhi wanazotumia baada ya kuridhika kuwa serikali na vyombo vyake vimeshindwa kuwajibika kusimamisha utwaaji huo wa ardhi.

Baadhi ya wabunge waliokuwa wakali kimatamshi kuhusu suala hili ni Halima Mdee (Kawe, CHADEMA) na Dk. Faustine Ndugulile (Kigamboni, CCM). Mdee na Ndugulile wote ni wabunge vijana na misimamo yao mikali ilisikika pia kwa Moses Machali (Kasulu mjini, NCCR-Mageuzi) na Esther Bulaya (Viti Maalum, CCM).

Matamshi ya wabunge hawa yalichagizwa na mchango makini wa Tundu Lissu (Singida Mashariki, CHADEMA) ambaye alikataa kutafuna maneno pale aliposema migogoro mingi ya ardhi nchini inasababishwa na utendaji mbovu wa serikali na vyombo vyake.

Lissu ambaye ni mwanasheria, alisema migogoro ya namna hiyo imekuwa ikizalisha machafuko katika nchi nyingi Afrika, na kwa mbali mazingira ya unyonge kwa wananchi wanaonyang’anywa ardhi yao, huzaa harakati za mapinduzi dhidi ya watawala.

Mdee alisema anasikitika kuona kwamba hata baada ya kukutana na viongozi wa wizara ya ardhi, kumekuwa na matatizo katika kufuatilia migogoro ya ardhi maeneo ya Tegeta, kiasi cha watu kupigana mpaka kujeruhiana kwa mapanga.

Ni yeye aliyetuhumu kuwa mmiliki wa kituo cha mafuta cha Namanga, Tegeta, amekuwa akitambia wananchi kuwa hawamwezi kwa lolote kwa kuwa ana pesa za kutosha, na yuko karibu sana na viongozi wa juu serikalini.

Dk. Ndugulile alilalamikia sana mradi wa mji mpya wa Kigamboni akisema kuwa serikali haijashirikisha wananchi, imewazuia kuendeleza maeneo yao tangu mwaka 2008, ili kusubiri mradi huo. Alisema mradi huo umehalifu sheria na kwa hivyo iwapo waziri hatarudi Kigamboni kuzungumza na wananchi, yeye atasimama nao kupinga mradi.

Lukuvi yawezekana alilenga kutisha wabunge wakakamavu wasiendelee kuishambulia serikali. Kauli ya mwisho ya naibu spika Ndugai ikawa kwamba wabunge wajiepushe na kauli zinazoweza kuonekana ni za uchochezi ndani ya bunge.

Katika dhana ya upanuzi wa demokrasia, hoja iliyotolewa na Lukuvi haina maana kwa sababu uchaguzi wa maneno katika kuikosoa serikali hausaidii kuficha uzembe wa serikali wa kutowajibika kimajukumu.

0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: