Kiwewe kitupu CCM


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 01 September 2010

Printer-friendly version
Mabere Marando

KOMBORA lililorushwa na muasisi wa mageuzi nchini, wakili wa mahakama kuu, Mabere Marando limetia kiwewe Rais Jakaya Kikwete na baadhi ya wasaidizi wake, MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa kutoka ndani ya chama hicho zinasema, tangu Marando atupe kombora kwa viongozi wastaafu na waliopo madarakani, kumekuwa na mkanganyiko ndani ya chama hicho.

Kundi moja la viongozi limekuwa likitaka Marando ajibiwe, huku kundi jingine likitaka kunyamaza, likihofia “kuyakuza na kuyaeneza nchi nzima.”

Marando, akihutubia mamia ya wananchi katika viwanja vya Jangwani, jijini Dar es Salaam, Jumamosi iliyopita, alisema wahusika wakuu wa ufisadi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), bado hawajakamatwa.

Aliwataja ambao hawajakamatwa kuwa ni rais mstaafu Benjamin Mkapa, Rais Jakaya Kikwete, aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa na mfanyabiashara Rostam Aziz.

Alisema serikali iliyopo madarakani haiwezi kumaliza ufisadi kwa kutoa kafara baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi na kuacha vigogo waliohusika kuendelea kupeta mitaani.

Kati ya Julai 2005 na Januari 2006, zaidi ya Sh. 133 bilioni zilikwapuliwa kutoka akaunti ya EPA ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Kwa mujibu wa nyaraka zilizopo, mabilioni ya shilingi yalikwapuliwa na kutawanywa katika mabenki mbalimbali nchini mjini Dar es Salaam.

Katika kipindi kisichozidi siku saba, tayari mabilioni ya shilingi yalikutwa yameshayeyuka kutoka mabenki yalikokuwa yamewekwa.

Akihutubia maelfu ya wananchi kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mkuu za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Marando alisema watuhumiwa wenyewe wa ufisadi hawajakamatwa.

Alisema ufisadi unaodaiwa kufanywa na mkurugenzi wa utumishi wa BoT, Amatus Liyumba au fedha za umma zinazodaiwa kuchotwa na mfanyabiashara Rajabu Maranda, ni sehemu ndogo sana ya fedha zilizoibwa.

Kwa sauti ya mpasuko na kwa wasikilizaji waliokaa kwa shauku ya kupokea ujumbe, Marando alisema, ufisadi hauwezi kumalizwa na CCM kwa kuwa nyingi ya fedha hizo zilitumiwa na chama hicho katika uchaguzi wa mwaka 2005.

Marando alikiri kuwa anatetea baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi katika akaunti ya EPA na kwamba hiyo ni haki yao kikatiba na kisheria. Alidai kuwa anasema anayoyasema kwa vile anafahamu kilichotendeka.

“Liyumba na Maranda wametolewa kama mbuzi wa kafara. Fedha zile zimeibwa na Mkapa, baada ya kuombwa na Jakaya Kikwete, Rostam Aziz na Edward Lowassa," alisema Marando huku umati wa wasikilizaji ukishangilia.

Akiitikia kauli za wananchi za “Sema! Sema!,” Marando alisema, “Nasema haya kwa sababu nafahamu hawawezi kunifanya chochote... wakithubutu nitawaumbua mahakamani."

Marando alikumbushia hotuba ya Dk. Slaa aliyoitoa Septemba mwaka 2007 kwenye viwanja vya Mwembeyanga, wilayani Temeke, Dar es Salaam ambapo alitoa orodha ya watuhumiwa 11 wa ufisadi ilianikwa ambayo yeye aliita “timu ya wachezaji 11.”

Katika hotuba yake, Dk. Slaa baada ya kutaja watuhumiwa, alisema wanahusika na wizi mkubwa kwa kuwa ama “wameruhusu au wameidhinisha au wamenyamazia ufujaji wa fedha za umma.”

Mbali na Mkapa, Kikwete, Lowassa na Rostam, wengine ambao Dk. Slaa alitaja ni aliyekuwa gavana wa BoT, Dk. Daudi Ballali, wakili wa mahakama kuu, Nimrod Mkono, mawaziri Basil Mramba, Andrew Chenge na Katibu Mkuu wizarani, Patrick Rutabazibwa.

Wakati Marando ameanza kuranda rejea za tuhuma hizo, ghafla kituo cha televisheni cha TBC 1 kilikatisha matangazo yake, jambo ambalo lilizusha tafrani kubwa kwa washabiki na wanachama wa chama hicho kutishia kuchoma moto gari la matangazo la shirika hilo.

Aliyeokoa TBC “kutoangamizwa” ni mkuu wa wilaya ya Ilala, Leonidas Gama ambaye taarifa zinasema aliwaeleza viongozi wa juu serikalini hatari iliyopo iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa kurejesha matangazo hayo.

Gama alichukua uamuzi huo baada ya mwenyekiti wa taifa wa Chadema, Freeman Mbowe kuomba msaada wa ulinzi kutokana na kuwapo kwa tishio la kutaka kushambulia wafanyakazi wa TBC na kuchoma moto vifaa vyao yakiwamo magari.

Mkuu wa wilaya alikuwa miongoni mwa wageni kutoka serikalini walioalikwa kuhudhuria mkutano wa Chadema.

Waliohudhuria mikutano ya vyama vya CCM na Chadema, wamesema umati uliohudhuria mikutano hiyo ulikuwa unalingana. Tofauti iliyokuwepo ni kwamba wakati CCM ilisomba wananchi kwa mabasi na malori, Chadema haikuonekana inafanya hivyo.

Siku moja baada ya Marando kutuhumu viongozi wa CCM kuchota fedha za umma kupitia Akaunti ya EPA, Meneja kampeni wa chama hicho, Abdulrahman Kinana aliitisha mkutano na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam kujibu madai ya Marando.

Katika maelezo yake, Kinana alisema Marando amekwenda kinyume na maadili ya kazi yake ya uwakili, jambo ambalo limetafsriwa na wachambuzi wengi wa mambo ya kisiasa kuwa “ameishiwa utetezi.”

Kinana amesema, “CCM imesikitishwa na kauli (za Marando), hasa ikizingatiwa kuwa aliyetoa tuhuma hizo ni mwanasheria.” Akashauri viongozi wakuu wa Chadema kuacha kutoa kile alichoita, “uzushi na kebehi…”

Baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi wamedai katika hati zao za kiapo kwamba baadhi ya fedha walizochukua, walizikabidhi kwa Salome Mbatia, ambaye wakati huo alikuwa mwekahazina wa chama hicho. Ni marehemu.

Kwa mfano, mmoja wa watuhumiwa wa EPA, Jeetu Patel, katika kesi iliyopo mahakamani, ameeleza katika kiapo chake kwamba karibu asilimia 60 ya fedha alizopewa alizikabidhi kwa baadhi ya viongozi wakuu akiwamo Mbatia.

Anasema fedha nyingine zilitumika kuingiza magari aina ya Hindra ambayo yalitumiwa na CCM katika kampeni zake za mwaka 2005.

Taarifa za kuaminika zinasema watuhumiwa wengi wana nyaraka ambazo pale zitakapowasilishwa mahakamani, zitabadili mkondo wa tuhuma.

Mbali na Marando kutuhumu viongozi hao wanne kuwa walichota katika EPA, mkurugenzi wa sheria wa Chadema, Tundu Lissu alianika hadharani moja ya mikataba ya kinyonyaji nchini aliodai una saini ya Luteni Kanali Jakaya Mrisho Kikwete.

Lissu alisema Kikwete ndiye alisaini mkataba wa kinyonyaji wa kuchimba madini wa Bulyanhulu, tarehe 5 Mei 1994 wakati huo akiwa waziri wa Nishati na Madini.

Alisema, “…mwaka 1996 niliporejea kutoka Marekani, nilikamatwa kwa kosa la uchochezi baada ya kusema kwamba serikali imefukia watu kule Bulyanhulu. Leo, miaka 14 baadaye, naambiwa Kikwete ameahidi kulipa fidia watu walioathirika na hatua ile.

“Kwanza, natoa wito kwa rais Kikwete, kabla ya kutekeleza uamuzi wake wa kulipa fidia wahanga wa mauaji yale, aombe radhi wananchi wa Kahama kutokana na hatua yake ya kusaini mkataba ulioangamiza maisha yao,” alisema.

Alisema, “Kisha aniombe radhi mimi binafsi kwa kunizushia kesi na kunilaza selo bila kosa.”

Mkataba ambao nakala yake Lissu alionyesha hadharani, ni ule uliofungwa kati ya serikali na Kampuni ya Kahama Mining Corpotion Limited. Leseni ilitolewa tarehe 5 Agosti 1994.

Utata katika mkataba huo, ni pale unaposemeka kuwa eneo la mradi ni Butabela, wilayani Geita, mkoani Mwanza, wakati leseni iliyotolewa inaruhusu shughuli za uchimbaji kufanyika katika eneo la Bulyanhulu, mkoani Shinyanga.

“Hawa Kahama Mining Corpotion wapo pale kinyume cha sheria. Kikwete anajua hili. Viongozi wote serikalini wanalijua hili. Lakini wanashindwa kuchukua hatua kuwaondoa wahusika kwa sababu, rushwa ilitawala mchakato wote wa uuzaji na ubinafsishaji wake,” alidai Lissu katika mahojiano ya baadaye na MwanaHALISI.

Kwa mujibu wa mkataba huo, awali eneo hilo lilikuwa linamilikiwa na serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) lililokuwa na asilimia 15 ya hisa na nyingine zikiwa za kampuni ya Sutton Rison kutoka Canada.

Mwaka 1999 inadaiwa kuwa serikali iliuza asilimia 15 ya hisa zake kwa kampuni ya Canada. Hata hivyo, haijulikani katika mchakato huo serikali ilipata kiasi gani.

Lissu amesema Rais Ali Hassan Mwinyi alikuwa amewahikikishia wananchi wa Bulyanhulu kuwa eno lao ni mali yao, na kwamba hawataondolewa.

Amesema hatua ya kuandika eneo la mkataba kuwa Butabela, mkoani Mwanza ililenga kuepuka kukaidi maagizo ya Rais Mwinyi, lakini ulikuwa ujanja tu kwani haikuchukua muda wakawakabidhi wawekezaji eneo walilolitaka la Bulyanhulu.

Taarifa ambazo viongozi wa Chadema wamekataa kuthibitisha zinasema chama hicho kinatarajia kushusha makombora mengine mawili ndani ya wiki mbili za kampeni. Zimesema lengo ni kushusha makombora 20 hadi kumalizika kwa kampeni za uchaguzi.

Kwenye uwanja wa Jangwani, Dk. Slaa aliahidi kufanya kidato cha sita kuwa elimu ya awali na inayotolewa bila malipo ya nyongeza kutoka kwa wazazi.

Aliahidi kuwa serikali yake itatoa elimu bora na katika mazingira bora ya madarasa, vifaa na walimu wanaolipwa mishahara inayokidhi mahitaji yao.
Alitaja umuhimu wa kilimo cha kisasa kinacholisha viwanda na kuongeza bidhaa na ajira; na kutumia nishati ya umeme kuendeshea garimoshi na siyo njia za kale za dizeli na kuni.

Dk. Slaa aliahidi kuwa na serikali ndogo kwa nia ya kupunguza matumizi ili fedha zitakazookolewa zitumike kwa maendeleo ya wananchi.
Kuingia kwa Marando katika msafara wa Chadema kumeleta chachu mpya. Anaifahamu Tanzania kwa vile aliishafanya mizunguko miwili nchi nzima wakati wa kuanzisha mageuzi.

0
No votes yet