KKKT lilipoteza ujasiri siku nyingi


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 15 July 2008

Printer-friendly version
Askofu wa KKKT

KANISA la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani, limejikuta katikati ya mgogoro wa kisiasa. Ni jambo la fedheha kuona baada ya kufanya kosa kubwa, sasa linalazimika kutumia nguvu nyingi kujisafisha.

Linapiga kelele kukana kukaribisha mfanyabiashara na mwanasiasa Rostam Aziz, ambaye wamekuwa wakimtumia katika mambo yao mengi huko nyuma.

Rostam, mbunge wa Igunga na mwanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM), alialikwa kwenye Usharika wa KKKT Kinondoni kushiriki uzinduzi wa kwaya ya Kanisa uliokwenda pamoja na hafla ya kuchangisha fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Hapohapo, Rostam alipopanda jukwaani, alijitangaza binafsi kama mtu msafi asiye doa lolote bali kupakaziwa tu na watu wenye chuki naye. Alikuwa katika jitihada za kufuta tuhuma nzito za ufisadi zinazomkabili. Sasa anadaiwa kutumia jukwaa la Kanisa kujisafisha.

Hapana shaka Rostam hakuitwa kwa bahati mbaya kwani akiwa ni mtu maarufu na mwenye uwezo mkubwa kifedha, alitarajiwa kusaidia kutunisha mfuko wa Kanisa. Na kweli, alifanikisha kazi hiyo kwa kuchangia Sh. 5 milioni.

Kwamba hizo ni fedha nyingi au ndogo, si muhimu. Ila ni kuthibitisha kuwa Rostam ni mtu wa Usharika huo maana hiyo si mara yake ya kwanza kutoa ili kusaidia miradi ya usharika huo. Kwa Kinondoni, Rostam unaweza kusema ni sawa na hadithi ya zimwi likujualo!

Kwa bahati mbaya au kwa kunuia, Rostam alitumia fursa aliyopewa kusema mambo yanayomsonga moyoni kwa muda sasa. Aligusia sakala la ufisadi ambalo kwa mwaka mzima sasa, ni ajenda kubwa nchini.

Kuna ufisadi uliofanywa kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA); kwenye mkataba wa umeme wa dharura wa kampuni ya Richmond Development Corporation; kwenye kampuni ya Meremeta na Tangold. Kote huko kumekuwa na msukumo mkubwa wa kutaka watu wawajibike.

Umma unajua yote yaliyotokea kwenye uchunguzi wa mkataba wa Richmond. Kamati Teule ya Bunge ya Dk. Harrison Mwakyembe ilitoa ripoti iliyokuwa na ugunduzi makini, ambao hatimaye ulisukuma Baraza la Mawaziri kuanguka likianzia na kujiuzulu Waziri Mkuu, Edward Lowassa.

Umma unakumbuka pia kuwa pamoja na matokeo hayo, wapo mawaziri waliojiuzulu sambamba na Lowassa; nao ni wale waliopata kushika Wizara ya Nishati na Madini; Nazir Karamagi na waziri aliyemtangulia, Dk. Ibrahim Msabaha.

Rostam ni mmoja wa watu waliohusishwa na mkataba huo wa Richmond na ndio maana amekuwa akipambana kujisafisha.

Wakati wa uchunguzi, hakuhojiwa kutokana na kutofika mbele ya Kamati Teule ya Bunge. Kwa hivyo maelezo yake hayakupatikana. Lakini alisikika akisema baadaye kuwa hakutendewa haki.

Bunge lilisikia kilio chake na Spika aliamua kumpa nafasi ya kuwasilisha ufafanuzi wake kwa Spika hasa pale aliposema Kamati Teule ilifanya kazi hata baada ya muda wake kwisha.

Kwa bahati mbaya, maelezo aliyoandaa kuyatoa bungeni, hayakupewa nafasi ya haki kusikika kwa wabunge na Watanzania. Spika Samuel Sitta alisema maelezo hayo hayakuwa na jipya zaidi ya kukashifu viongozi.

Rostam pia ametajwa kuhusika kwa njia moja au nyingine na kampuni ya Kagoda Agriculture Limited, moja ya makampuni 22 yaliyothibitishwa kuchotewa Sh. 133 bilioni za EPA, akaunti iliyoko Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Kwa yote hayo, mwenye akili tulivu anajiuliza: Iko wapi busara ya Kanisa kumwalika Rostam wakati huu na kumpa nafasi ya kuzungumza ikijulikana wazi ana mawaa na hayajasafika?

Mwanasiasa mmoja amepata kusema Kanisa linasita kukemea ufisadi. Amethibitishwa hakukosea. Kwa kuwa viongozi wa Kanisa wanaamini fedha hazina rangi wala uchafu, hawajali anayezitoa yukoje mbele ya macho ya umma.

Hali halisi ni kwamba Kanisa limejifikisha mahali pa kupokea fedha kutoka kwa mtu yeyote – hapa nachelea kusema kuwa hata fedha za shetani sasa zinaweza kupokelewa na viongozi wa Kanisa wakazikubali.

Mbali na ukweli wa uharaka huu na Kanisa kukosa uvumilivu kwa kiwango hicho kwa sababu tu ya kutaka fedha, kwa namna lilivyoshughulikiwa suala hili, kumejengeka picha kuwa Kanisa ni taasisi inayotetereka.

Kanisa ni kimbilio la wenye shida, ni taasisi inayobariki na kulea maridhiano baina ya watu waliofarakana, Kanisa linaloabudu umaarufu wa nje kwa kukimbilia kutoa taarifa kalikali kama hiyo ya kumlaani Rostam, ni Kanisa lililopoteza subira.

Kwani kulikuwa na ulazima gani hasa wa uongozi wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani ya KKKT kutoa tamko la kumkana Rostam? Mbona huko nyuma kuna matukio makubwa tu yaliyoonyesha ukiukaji wa utaratibu wa kualika watu kanisani na wakubwa wakafunika kombe mwanaharamu apite?

Je, safari hii Kanisa limefanya kinyume cha utamaduni wake wa kuvumilia na kulea watu ili tu lionekane linapiga vita ufisadi?

Kanisa linataka kusadikisha umma kuwa eti katika orodha ya mafisadi ambayo tangu mwaka jana ilianikwa hadharani kwenye viwanja vya Mwembe Yanga jijini Dar es Salaam hakuna kiongozi anayestahili kutolewa tamko?

Kwa nini Kanisa halijachukua orodha ile na kuitaka serikali iwawajibishe kulingana na tuhuma walizoelekezewa hao waliotajwa? Kwa nini linamchagua Rostam tu kwa sasa?

Sina sababu ya kumtetea Rostam, lakini pia sina moyo wa kusimama upande wa Kanisa kwa hapa. Ukweli ni kuwa siamini kama limetumia vema vipaji vya kiuongozi viliopo miongoni mwa viongozi wake.

Kila mtu anajua kwamba hatua ya KKKT limeshughulikia suala la mwaliko wa Rostam kwa makeke, pakikosekana uvumilivu na maadili ya kiroho kukabili majaribu yaliyoko mbele yake.

Kikubwa zaidi, Kanisa limejitahidi mno kujitenga na wanasiasa wa Kambi ya Upinzani na kuacha yote wanayoyaeleza kuhusu kuangamia kwa taifa kunakotokana na vitendo vya kifisadi vinavyoota mizizi.

Badala yake, linajitokeza kuwa mstari wa mbele kukumbatia viongozi wachafu na waovu ambao wameipiga nchi hii mnada. Ndio maana nathubutu kusema kuwa Kanisa limekosa ujasiri siku nyingi, haliwezi tena kuikomboa nchi.

0
No votes yet