KKKT na mzimu wa Richmond


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 08 December 2010

Printer-friendly version
Jamvi la Weledi

MKUTANO mkuu wa Kanisa la Kiinjili na Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, umemalizika mjini Bagamoyo kwa staili ya aina yake. Ni fedha chafu kushindwa kufanya kazi kwa waliomtanguliza Mungu mbele.

Wajumbe wa mkutano mkuu wa Dayosisi waliombwa kupiga kura ya kutokuwa na imani na mkuu wa Kanisa hilo, Askofu Dk. Alex Malasusa ili aondolewe katika wadhifa wake. Hilo limeshindikana.

Kwa zaidi ya miezi miwili mfululizo, magazeti kadhaa yanayomilikiwa na mmoja wa watuhumiwa wa ufisadi nchini, yalikuwa yakichapisha makala mbalimbali za kulichafua Kanisa na Askofu wake mkuu Dk. Malasusa.

Kujihusisha kwa magazeti hayo na siasa za ndani ya KKKT kuliendana na tuhuma nzito kuwa mmiliki wa magazeti hayo alikuwa akigawa fedha katika makanisa ya Lutheran ili kushinikiza kuondolewa kwa Askofu Malasusa. Hili lilizusha mjadala mkali katika ukumbi wa mikutano jioni ya Jumapili iliyopita.

Hoja iliibuka pale wajumbe wa mkutano mkuu walipoamua kujadili kilichoitwa na magazeti hayo, “Kashfa za kiongozi wao mkuu.”

“Nikiwa miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo, nilishuhudia wajumbe wa mkutano wakisimulia waziwazi, kuwa kuna waliopiga kambi katika Hotel Sharrif mjini Bagamoyo, ambao wanagawa fedha kwa wajumbe ili kushinikiza kuondolewa kwa Askofu Malasusa,” ameelezammoja wa wajumbe.

Baadhi ya wajumbe wa mkutano walikuwa wawazi ndani ya mkutano na kueleza kuwepo kwa fedha hizo na hata mmoja wa wajumbe alikwenda mbali na kuomba sala ili Mungu aondoshe watu hao “wenye husuda.”

Kanisa la Lutheran makao makuu Arusha, lilimtuma Askofu Bagonza wa Dayosisi ya Karagwe ili awepo mkutanoni kusimamia taratibu zote za mkutano huo akiwa mwakilishi maalum wa kanisa.

Askofu Bagonza, kwa hekima kubwa na ukomavu wa mambo ya kanisa, aliuambia mkutano huo kuwa yeye ni “mkuu wa kanisa wa zamu” kwa vile mkuu wa kanisa Dk. Malasusa alikuwa anaendesha mkutano huo “nyumbani kwake.”

Aliwataka wajumbe wa mkutano kutoruhusu kabisa kanisa kupangiwa ajenda na wanasiasa au matajiri wanaomiliki vyombo vya habari.

Katika hali ambayo haikutegemewa, Askofu Bagonza aliueleza mkutano huo kuwa kura ya imani kwa Askofu Malasusa, si kuchagua Askofu kama ambavyo magazeti yamekuwa yakilazimisha wakristo kuamini.

Alisema kura ya imani ni hatua ya kutathmini kazi na utendaji kazi wa Askofu ili anapoendelea ajue ni maeneo gani anahitaji kuyafanyia kazi.

Bagonza alisema Malasusa ni Askofu tayari na ataendelea kuwa Askofu na hata kama kungekuwa na matatizo fulani si kazi ya vyombo vya habari, hasa magazeti yanayomilikiwa na watuhumiwa wa ufisadi kufanya kazi hiyo.

“Mtu yeyote, asiye mwenzetu kiimani, hana mamlaka ya kuliamulia kanisa namna ya kushughulikia kasoro za kanisa, kama zipo, na viongozi wake,” alieleza Askofu Bagonza.

Askofu Bagonza ambaye anaonekana kuwa ni mtaalam wa katiba na kanuni za makanisa, alisoma katiba ya Dayosisi ya Mashariki na Pwani na kuelekeza, “Kura ya imani kwa Askofu itapigwa kwa uwazi badala ya siri kwa kuwa katiba hiyo haisemi kuwa kura hiyo ipigwe kwa siri.”

Akizungumza kwa njia ya mahubiri, Askofu Bangoza aliwambia wajumbe wa mkutano mkuu wa Dayosisi, kwamba anayeshinikiza kanisa kumfukuza mkuu wake, si muumini wa kanisa hilo…

“…Huyu bwana si mkristo. Sasa, huu uchungu kwa kanisa letu unatoka wapi,” alihoji.

Alitaja vifungu kadhaa vinavyopigiwa kura kwa siri na kwamba vimo ndani ya katiba hiyo lakini kundi la “wachochezi” na wenye magazeti, hawakuwa wamevisoma.

Dk. Malasusa alipigiwa kura na kupitishwa kwa asilimia 96.6. “Wachafuzi na wenye magazeti waliondoka Bagamoyo usiku huohuo kwa hasira na kukata tamaa,” ameeleza mmoja wa maaskofu.

Sasa gumzo linaloendelea ndani ya KKKT ni kuhusu uamuzi wa mmiliki wa magazeti kuingilia masuala ya ndani ya kanisa hilo. Taarifa zilizotolewa katika mkutano huo na wajumbe mbalimbali zinadai kuwa hii ni ajenda ya mkataba tata wa Richmond inayoendelea kulitafuna taifa hili.

Mmoja wa watuhumiwa wa Richmond, Rostam Aziz aliwahi kuingia katika kanisa moja la KKKT jijini Dar es Salaam na kutumia nafasi hiyo kutoa mchango mkubwa kwa kwaya ya kanisa.

Rostam alitumia fursa hiyo kuhutubia waumini; akijitahidi kujisafisha kutokana na tuhuma za ufisadi zinazomkabili, huku akiwatuhumu baadhi ya wanasiasa wanaosali katika kanisa hilo.

Baada ya tukio hilo, Dayosisi ya Mashariki na Pwani ilitoa tamko la kukana kumwalika kanisani kwake na hatimaye dayosisi iliamua kumrudishia mchango wake.

Katika tamko hilo, dayosisi ilisema wazi kuwa haitatumika kusafisha ufisadi wa mtu yeyote. Kitendo cha kutoa tamko inadaiwa kuwa kilimuudhi sana Rostam na watu wengi wanadhani hatua hiyo ilimletea kinyongo.

Katika harakati za kampeni za uchaguzi mkuu uliomalizika, Askofu Malasusa alihimiza wananchi kuchagua mtu badala ya chama.

Baadhi ya wajumbe wa mkutano unaoendelea Bagamoyowamesema ni imani yao kuwa magazeti hayo yanachochea suala hili ili kujipendekeza kwa chama fulani,  bila kujua kuwa utetezi wa mafisadi kwa chama hicho unakipotezea sifa.

Kingine kilichojionyesha katika mkutano wa Bagamoyo, ni siasa za makundi kuhamia ndani ya kanisa hili kubwa nchini.

Wapo wanaodai kuwa hata uamuzi wa kulichafua kanisa na baadhi ya viongozi wake, umetokana na shinikizo la makundi fulani ndani ya vyama na hata serikali.

Wengine wamesema waziwazi kuwa kile kinachokaririwa na watawala kuwa ni “udini,” hakika ni ajenda inayofichwa ndani ya kashfa hizi, ikiwamo misuguano ya kumtafuta mgombea wa nafasi ya urais mwaka 2015.

Yawezekana kuna ukweli katika jambo hili kwa sababu baadhi ya vigogo serikalini na kwenye chama wanaopigana vikumbo kuwania urais 2025 wanatoka katika KKKT na sasa wanaonekana kuliingiza kanisa katika mgogoro wa ndani ya serikali na chama kilichopo madarakani.

Kimsingi katika mkutano huu, mengi yamejadiliwa. Lakini kubwa ilikuwa ni hatua ya wajumbe wa mkutano mkuu “kushinda shetani kwa kukataa fedha za watuhumiwa wa ufisadi kufanya kazi ya kusambaratisha kanisa lao,” ameeleza mmoja wa maaskofu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: