KKKT watuhumiwa kupora nyumba


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 05 January 2011

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii
Askofu Mkuu wa KKKT, Malasusa

KANISA linatarajiwa kuwa ni kimbilio lililo salama kwa waamini na wananchi wa kawaida wanaopatwa na shida au matatizo ya kimwili au kiroho.

Lakini dhana hiyo inakinzana na hali halisi. Uongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Mashariki na Pwani (KKKT-DMP) si kimbilio salama kwa wenye shida.

Mwanzoni mwa mwezi uliopita uongozi wa KKKT-DMP unadaiwa kufanya jambo la kinyama kula njama za kutaka kuitoa familia kwa nguvu na kutwaa nyumba ya mchungaji aliyewahi kulitumikia, marehemu Readwell Mordecai Sinyangwe.

Mchungaji huyo ambaye baadaye alihama kanisa hilo na kujiunga na kanisa la Presbyterian, alifariki dunia miaka miwili iliyopita akiwa na umri wa miaka 80. Mgogoro wa nyumba ulianza akiwa hai na hadi anafariki dunia ulikuwa haujapatiwa ufumbuzi.

Njia ambayo kanisa uliona inafaa ni kutumia nguvu. Hivyo alfajiri ya 2 Desemba 2010 ikawa ya kilio na kusaga meno pale kundi la vijana wapatao 20 wenye miraba minne (mabaunsa) kuvamia nyumba hiyo Na. 135/C iliyopo Mwananyamala jijini Dar es Salaam na kutembeza kipigo.

Kwa mujibu wa Grace Bwemelo ambaye ni mtoto wa hayati Sinyangwe, mabaunsa hao walivunja mlango na kuingia ndani ya nyumba hiyo, na kuanza kuwapiga yeye, mumewe William Bwemelo na mtoto wao George Bwemelo. Grace ndiye msimamizi wa mirathi ya hayati baba yake.

“Mimi nilikabwa koo na kukandamizwa chini kiasi kwamba kwa wiki nzima baada ya tukio sikuweza kuzungumza vizuri. Tulivamiwa na kutendwa kama wezi. Awali nilidhani ni majambazi lakini sikuamini nilipoambiwa ni watu waliotumwa na kanisa,” alisimulia Grace.

Anasema mabaunsa waliharibu vitanda, meza, viti na sehemu za kuwekea mapazia, huku wakichukua vitu kama vile simu na vifaa vingine.

George (21) alisema,  “Ilikuwa ni siku ya kutisha sana kwangu. Watu mmelala na ghafla kundi la watu linaingia kwa nguvu na kuanza kuwapiga pasipo kosa. Hii nchi inakwenda kubaya sasa. Watu hawajali tena utawala wa sheria.”

Grace akaongeza, “Tulipigwa sana na hatukuweza kujitetea maana wavamizi wenyewe walikuwa wengi na walikuja kwa shari. Walikuja wakidai kuwa wameelekezwa na mwanasheria kuchukua hatua hizo kwa vile sisi (familia ya mchungaji) tumekuwa wakaidi.”

Kwa hiyo, kama mabaunsa walitumwa na mwanasheria wa kanisa moja kwa moja walitumwa na kanisa.

Utetezi wa KKKT

Msemaji wa Kanisa hakupatikana, lakini kiongozi mmoja alidokeza kwamba huenda waliowavamia ni kampuni ya udalali ambao huenda walipewa idhini na mahakama.

Kiongozi huyo, ambaye hakutaka jina lake litajwe wazi kwa vile si msemaji alisema kanisa linamiliki nyumba hiyo tangu mwaka 1977 lilipoinunua kihalali kutoka kwa mchungaji Sinyangwe.

Kiongozi huyo ambaye pia ni mchungaji alisema, “Hiyo nyumba tuliuziwa na mchungaji Sinyangwe tangu mwaka 1977 na ushahidi tunao.”

Mwaka unaotajwa na mchungaji huyo kwamba kanisa lilinua nyumba hiyo una utata. Kwa mujibu wa nyaraka ambazo MwanaHALISI limeziona Sinyangwe aliuziwa nyumba hiyo yenye thamani ya  Sh. 10,587 mwaka 1966 na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa mkataba wa kulipa kidogo kidogo na kwamba alimaliza kulipa mwaka 2000.

Kwa hiyo, kanisa linaeleza kwamba mchungaji aliwauzia nyumba hiyo wakati kisheria bado ilikuwa mali ya NHC. “Cha msingi sisi tuna ushahidi kuwa tuliinunua nyumba hiyo,” alisisitiza mchungaji huyo akisimamia hoja yake kwamba wanamiliki nyumba hiyo tangu mwaka 1977.

Chimbuko

Grace anasema mzozo kati ya familia ya mchungaji Sinyangwe umedumu kwa miaka tisa sasa. Ushahidi wa maandishi unaonyesha kuwa nyumba hiyo ilinunuliwa na marehemu baba yake kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

“Nyumba hii ilikuwa mali ya NHC lakini baba aliinunua kwa malipo ya taratibu kwa thamani ya Sh. 10,587. Alianza kulipa deni hilo mwaka 1966 na kulimaliza mwaka 2000 na shirika la nyumba likamkabidhi rasmi nyumba hiyo,” anasema Grace.

“Kilichotokea ni kuwa, katika miaka ya 1970, KKKT-DMP, ilimwomba baba awaruhusu waitumie nyumba hii kuwaweka wachungaji wao wanaolitumikia kanisa.

“Baba alikubali kwa vile alikuwa amepata uhamisho kwenda Mafia na baadaye Rufiji hivyo yeye asingeweza kukaa tena hapo. Hivyo aliliachia kanisa nyumba kwa nia njema kabisa ya kuhakikisha watumishi wa Mungu hawapati shida,” anaeleza huku akibubujikwa machozi. 

Lakini katika mazingira ya kutatanisha, kanisa lilianza kufanya mbinu ili lipate hati ya umiliki wa nyumba hiyo kupitia NHC. Shirika hilo lilikataa kwa maelezo kuwa nyumba hiyo si mali yake tena ila ni mali ya mchungaji.

Katika mawasiliano ya barua baina ya KKKT na NHC ambayo MwanaHALISI limefanikiwa kuyaona, shirika hilo la nyumba lilishauri kanisa kwenda katika ofisi za manispaa kwa ajili ya kupatiwa hati za umiliki kama itaona inafaa.

NHC ilishauri pia kuwa kama kuna mauzo ya nyumba yamefanyika baina ya mchungaji Sinyangwe na KKKT, basi ushahidi utakuwapo Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni na si  katika shirika hilo kwa vile wao walikwishauza nyumba hiyo.

Barua ya NHC ya Februari 2001 yenye Kumb. Na. NHC /KIN/TP/ 1/ 35C/ 18/ N2N, inasema tayari mchungaji Mordecai amemaliza deni la nyumba yake hiyo tokea mwaka 2000.

Grace anadai kuwa baada ya uongozi wa kanisa kupewa majibu hayo haukufurahishwa na hatua hiyo na ndipo ukaanza harakati za kutaka kuwaondoa kinguvu kutoka katika nyumba yao.

“Sisi ni watoto wa mchungaji aliyelitumikia kanisa kwa moyo wake wote. Tumelelewa katika misingi ya kanisa. Tunajua kanisani ndiyo pa kukimbilia iwapo mambo yatakuwa magumu. Inakuwaje kanisa leo lianze kunyanyasa watu wake?” anahoji Grace.

Baada ya baba yao kumaliza utumishi wa kanisa alirudi kwao Mbeya huku Grace ambaye alikuwa ameolewa akiishi nyumba ya kupanga karibu na nyumba yao.

Grace anasema walihamia katika nyumba hiyo mwaka 2009, wakati mgogoro wa umiliki wa nyumba ukiwa umepamba moto.

“Mimi nilikuwa naishi hapahapa Mwananyamala ila katika nyumba ya kupanga na mume wangu. Baba alipoanza kuugua tulikuwa tunapata shida kumuuguza kwa sababu nyumba ilikuwa ndogo na watu waliotaka kuja kumwona akija kutibiwa huku mjini walikuwa wengi.

“Ndiyo tukaona afadhali tuhamie katika nyumba hiyo ya baba. Tulihamia Septemba mwaka 2009 baada ya kanisa kuondoa watu wake. Tunaishi hapo hadi sasa,” anasema Grace ambaye amefungua jalada polisi.

Hatua za kisheria

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, amethibitisha shauri hilo kufikishwa kwake na amesema amekutana na pande zote mbili kuzungumzia suala hilo.

“Mimi nalijua hilo suala vizuri. KKKT wanadai nyumba hiyo ni yao na wana familia nao wanasema nyumba ni yao.Kazi ya polisi si kuamua mambo ya kisheria. Sisi kazi yetu ni kusimamia sheria. Kwa hiyo nikawaambia KKKT waende mahakamani kudai haki yao kama wanaona hawatendewi haki,” alisema Kinyela.

“Kosa lililofanywa na DMP ni hilo la kutaka kuwatoa watu kwenye nyumba kinguvu. Nchi hii inaongozwa na utawala wa sheria na si mabavu. Waende mahakamani na haki itatolewa huko na si polisi. Sisi tutasimamia maamuzi ya mahakama.”

0
No votes yet