Kova kaipaka matope serikali


Nyaronyo Kicheere's picture

Na Nyaronyo Kicheere - Imechapwa 18 July 2012

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

WAKATI nchi nzima imezizima kwa mgomo wa madaktari, kutekwa na kuteswa  Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka  na sinema ya bure ya vituko vya wabunge huko Dodoma, kajitokeza kamanda wa polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kufanya yale yasiyotarajiwa.

Kamana huyo Suleiman Kova hajulikani anamwakilisha nani kwa hayo anayoyafanya. Mtu muhimu, mtu mkubwa tena mtu ambaye ni kiongozi wa watu katekwa na mtu au watu wasiojulikana; kateswa na kesho yake kapatikana akiwa hoi bin taaban na sasa nchi nzima inataka maelezo.

Bila kuathiri shauri lililopo mahakamani, tunasema kuwa, badala ya kupata maelezo, wanachokipata raia wa nchi hii ni vituko mithili ya sinema za Holiwudi huko Marekani na kuwafanya wale, waliokuwa wakiitilia mashaka serikali yao kuwa ilihusika kwa njia moja au nyingine na utekeaji huo wazidi kuamini hivyo.

Eti siku ya Ijumaa Kova akawaita waandishi wa habari na kuwatangazia kuwa mtu mmoja raia wa Kenya kakamatwa na Jeshi la Polisi akihusishwa na utekaji na utesaji wa Dk. Ulimboka na kwamba tayari mtu huyo alikuwa kapandishwa kizimbani akikabiliwa na mashitaka ya utekaji na utesaji huo!

Sasa sisi wengine tunalazimika kulijadili jambo hili kwa makini sana kwa sababu jambo lenyewe tayari liko mahakamani. Na hoja ya kwanza kuikabili ni hii: kulikuwa na uharaka gani kiasi cha kumkamata mtu ijumaa na saa mbili au tatu badaye akafikishwa mahakamani?

Hapa ndipo tunaposema kuwa Kova kaitukanisha serikali na raia wake. Na raia wanasema kuwa Kova na wenzake wamekimbilia kufungua kesi dhidi ya Mkenya huyo ili kuzuia mjadala bungeni na kwenye vyombo vya habari kwa kisingizio kwamba tayari shauri lipo mahakamani!

Kwa muda Kova na wenzake wameonekana kushinda kwa sababu bungeni hawajadili habari ya Mkenya mtesaji kwa sababu eti shauri lipo mahakamani. Kwenye runinga na redioni nako waandishi wamefyata mkia hawaandiki wala kutangaza Mkenya au Ulimboka kwa sababu eti shauri lipo kortini!

Na kweli mitandao ya habari kuanzia Ijumaa ilijaa taarifa za Mkenya kukamatwa na masikitiko ya wananchi kuwa hawawezi kulijadili au kuliandika sakata hilo magazetini kwa sababu tayari limefikishwa mahakamani. Lakini ni kweli kufungua shauri kunazuia wananchi na hata waandishi kuandika na kujadili jambo lenyewe?

Mie nasema si kweli. Sidhani kwamba kufungua shauri mahakamani kunazuia, kwa mfano, wananchi kuhoji kwamba ilikuwaje mtu aliyetenda kosa kubwa la utekaji na utesaji atake kutubu ugenini asikojua mtu badala ya kurejea kwao Kenya.

Hapa yabidi kuelekezana kama kudharau mahakama maana yake nini. Hivi raia kuuliza kama ninavyouliza sasa, kuwa ilikuwaje jambazi au gaidi lililokubuhu liingie nchini na wenzake 12 lakini baada ya kuteka na kutesa, kama ni kweli lilihusika, lenyewe libakie nyuma?

Je, kuuliza hivyo ni kudharau mahakama kwa vile kesi imeshafunguliwa?

Naomba majaji, mawakili wakongwe na wanasheria wengine watueleze kama raia kuhoji na kujadili kama ninavyofanya mimi, eti ni kwa nini mchungaji wa kanisa la uokovu atoe siri ya muumini wake aliyefika kwake kutubu? Hivi hapo nadharau mahakama? Mie sidhani hivyo.

Mimi nadhani sisi raia na hasa waandishi wa habari tunayo haki ya kulijadili jambo hili alimradi tu hatuwaelekezi wasomaji na wasikilizaji wa taarifa zetu kuamini au kuuona upande mmoja katika shauri lililopo mahakamani kuwa ndio wenye haki.

Je, inapotokea kwamba mchunguaji wa kanisa la uokovu kajitokeza kupinga maneno yaliyotolewa na Kamanda Kova, akisema si kweli kuwa mtu yule alikwenda pale kanisani kuungama sie raia na hasa waandishi wa habari waendelee kutoandika habari ile eti kwa sababu shauri lipo kortini?

Mimi nasisitiza kuwa, katika sakata la Ulimboka, yapo mambo ambayo inafaa kuyajadili tena kikamilifu lakini mjadala wenyewe ufanyike bila kuathiri kesi iliyopo mahakamani, kesi ambayo ipo ngazi ya mahojiano ya wali kujua ukweli kabla ya kuipeleka mahakama kuu kusikilizwa.

Wananchi wanayo haki kumjadili mgeni wao anayedai kuhusika kuteka na kutesa kiongozi wa madaktari wakijiuliza kama kwa nini akamtafute kiongozi wa dini ambaye hamjui ili akaungame na siyo kurejea kwao akaungame huko Kiambuu, Nyahururu, Nakuru, Nyeri au Thika Town alikozoeleka?

Waandishi wanayo haki, bila kuathiri kesi kama ipo kortini, kuandika, kujadili na kutangaza habari za mgeni jambazi kutoka Kenya asiyeeleweka kalijuaje Kanisa hili la Uokovu na akataka kuungama huko na siyo Kanisa Katoliki, Kilulutheri au Pentekoste yanayofahamika kwa wengi na yaliyosambaa hadi Kenya?

Narudia tena, kwamba bila kuathiri kesi iliyopo mahakamani, wananchi na hasa waandishi wa habari wanayo haki ya kujiuliza na kujadili kwamba maneno ya kuungama ambayo sasa kiongozi wa Kanisa la Uokovu ameyakana kuwa si ya kweli, yeye Kamanda Kova kayapata wapi? Intelejensia ya Polisi?

Kitendo cha Kova kusema mambo ambayo hayaingii akilini kuwa ni ya kweli na hapo watakuwa hawadharau mahakama. Watu wajiulize na wahoji magazetini kuwa mbona Ulimboka hakusikia na kukumbuka Kiswahili cha Kenya kikizungumzwa pale msitu wa Pande?

Raia wanapswa kuandika na kutangaza habari za urahisi huu wa ajabu wa mtu anayedai kuwa ni gaidi kukiri kirahisi kuhusika na utekaji na utesaji kana kwamba mtu huyo katuhumiwa kuiba karanga. Hili jambo la Kova kudai mtu kakiri kuhusika kunatia shaka na ni wachache watakaoamini kuwa ni kweli.

Waswahili wanasema ndege mjanja hunaswa na tundu bovu. Ingekuwa taarifa zenyewe zimetokana na intelejensia ya polisi angalau zingepata mashiko lakini kudai eti mtuhumiwa au mshukiwa kaenda mwenyewe kanisani kutubu, halafu wahusika wakatae halikuwapo jambo la kutubu, Kova kasema uongo.

Mbaya zaidi serikali inatiliwa shaka kuhusika katika sakata hili na Kova naye anazidi kuipaka matope serikali yake kwa kudai mambo ambayo hata kiongozi wa kanisa husika kadai ni za uongo. Sasa tujiulize bila kuathiri kesi iliyopo kortini kuwa nani anamtuma Kova kuongopa?

Na uharaka wa kufungua shauri uliotoka wapi? Na je, ni kwaida kulingana na habari za kiinteleijensia kukuta mtu anakabiliwa na kosa kubwa ambalo adhabu yake ni pamoja na kifungo maisha akijitokeza kutubu kirahisi rahisi hivyo?

Wengine mpaka wateswe, waminywe ‘kengele’, wachomwe na umeme, wanyofolewe kucha na wang’olewe meno bila ganzi ndipo waseme lakini huyu Mkenya wa Kova amekuwa rahisi hivi? Mwepesi kama maharage ya Mbeya? Hapana inatia mashaka. Tujadili.

0
Your rating: None Average: 5 (2 votes)