Kuanzisha Azam FC, Bakhressa kaonyesha njia


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 12 August 2008

Printer-friendly version

KAMA kuna jambo la ujasiri analopaswa kupongezwa mfanyabiashara maarufu nchini, Said Salim Bakhressa na familia yake, basi ni kuanzisha, kuisimamia na hatimaye kuifikisha katika Ligi Kuu Bara timu ya soka ya Azam FC.

Azam itashiriki kwa mara ya kwanza katika ligi hiyo yenye mvuto mkubwa zaidi katika medani ya soka nchini.

Licha ya kupanda msimu huu ikiwa na Villa Squad ya Magomeni, wilayani Kinondoni, Azam imeonyesha kupania kufanya kweli, kwanza kwa kufanya usajili uliothibitisha ni makini, na pili, kuleta kocha mahiri.

Imetangaza kuibuka na kocha aliyeikimbia Simba, Neider dos Santos kutoka Brazil, huku kwa upande wa wachezaji ikisajili wakongwe na damu changa wa nyumbani, imekwenda Nigeria, Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Hapana shaka, dhamira ya uongozi wa timu hii inaweza kuleta mapinduzi makubwa katika soka nchini.

Nikirudi katika hoja ya msingi, ninampongeza Bakhressa na familia yake kwa mambo kadhaa. Kwanza, ni ujasiri wa kuamua kuachana na ubabaishaji wa klabu kubwa za nchini na kuangalia ustaarabu wake.

Itakumbukwa Bakhressa ni miongoni mwa wakereketwa wakubwa wa Simba waliokuwa wanajitolea kwa hali na mali kusaidia klabu hiyo miaka ya nyuma.

Lakini kutokana na dosari za hapa na pale zinazoendelea kudunisha maendeleo ya klabu hiyo, aliamua kujiweka kando na kutosikika kwa miaka kadhaa hadi yeye, au vijana wake walipoamua kuibuka na Azam FC.

Ujasiri wake huo unapaswa kuigwa na matajiri wengine wanaojitutumua kila kukicha kuzimwagia fedha nyingi Simba na Yanga bila ya kupima mafanikio yanayotokana na misaada yao. Hizi ni klabu ambazo hazikionekani kuwa na mwelekeo, zaidi ya migogoro isiyokwisha.

Yussuf Manji kwa mfano, pamoja na kuisaidia Yanga kwa kutoa mamilioni ya fedha, angepaswa kuona mbali na kuamini kuwa misaada yake haijasaidia kubadilisha fikra za viongozi na wanachama wake ili kuona njia ya maaendeleo. Alitakiwa kuangalia mfano wa waanzilishi wa Azam FC.

Kiasi cha Sh. 500 milioni alizotumia Manji kwa usajili msimu huu pekee, achilia mbali gharama za kambi kiasi cha Sh. 75 milioni kwa mwezi, mishahara ya wachezaji na makocha watatu wageni kutoka Ulaya na mambo mengine, ni mtaji wa kutosha wa kuanzisha timu hadi kuifikisha Ligi Kuu.

Kama hili likiwezekana, naamini nguvu zake za kiuchumi zitabaki katika kuisimamia klabu yake, ikiwa na maana ataikatia mirija Yanga.

Na kama staili hiyo itafuatwa na matajiri wengine, hakuna shaka yatazishitua Simba na Yanga na hivyo kujibadili na kukubali ukweli wa kubadilika.

Ndiyo, Simba na Yanga tunazozizungumza leo hazikuwa timu za kuhangaika na wafadhili, zilipaswa kuwa tajiri, zinazopapatikiwa na makampuni makubwa ya biashara kwa lengo la kuzidhamini.

Inashangaza kuona viongozi wa sasa waliodhaniwa wana mawazo ya kisasa, badala ya kuziinua klabu zao, wanaziacha ziangamie na kupoteza mwelekeo tofauti na yaliyokuwa malengo ya wazee wa klabu hizo miaka ya 1970 waliozianzisha.

Wazee wa klabu hizo waliona mbali kwa kujenga majengo ya kisasa, kwa ajili ya makao makuu. Yanga walikwenda mbali zaidi kwa kujenga uwanja wao wa Kaunda. Na hata usajili waliufanya kisasa zaidi tofauti na sasa, huku kambi kwa ajili ya michuano ya kimataifa zikiandaliwa wa umakini ikiwemo kupeleka timu Ulaya na hata Brazil!

Lakini leo, ukifika makao makuu ya Yanga au Simba, utajuta kwa utayoyaona. Majengo yamechakaa, huduma ya maji, umeme na simu zilizotandikwa miaka ile, hazipatikani. Hakuna usafishaji wa maana unaofanywa. Klabu sasa zinaendeshwa kupitia ofisi za mifukoni badala ya kwenye majengo yake. Zimepoteza kabisa mwelekeo.

Majengo yamebaki kuwa magofu, kwani hayatumiki kwa ofisi, wala kambi kwa wachezaji kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Badala yake, zimebaki kuwa timu za kubadilisha hoteli kwa ajili ya kambi na pia kuhamahama uwanja mmoja kwenda mwingine kwa ajili ya mazoezi. Maamuzi yao yanategemea mazingira yaliopo si utaratibu waliojiwekea. Aibu gani hii?

Simba na Yanga zimeua timu za vijana, viongozi hawakuni tena vichwa kujua jinsi ya kuziinua klabu zao kiuchumi, kwani yote yanarahisishwa na fedha za wafadhili.

Tujiulize, kwa miaka mingapi Simba na Yanga zitawaganda wafadhili mithili ya kupe, badala ya kupasua vichwa na kuanza kijitegemea? Kama viongozi wameshindwa kuona mbali, njia rahisi ya kuwazindua ni kwa matajiri kuanzisha klabu zao.

Kwa mtaji huo, viongozi wa Simba na Yanga wataamka kutoka lepe la usingizi na kufikiria njia za kusaidia na kuziendesha kwani wafadhili wa kupita hawatakuwepo wakati huo.

Ndiyo maana nashauri, kwa staili iliyotumiwa na Bakhressa na watoto wake, Simba na Yanga watachangamka kujitafutia kilicho chake, mtaji mkubwa ukiwa ni utitiri wa washabiki waliotapakaa pembe zote za nchini. Mapinduzi ya soka ya Tanzania yatakuja kama matajiri wataacha kukumbatia Simba na Yanga.

0
No votes yet